Na Seleman Juma- Songea
Katika mwambao wa ziwa Nyasa, mamba walikuwa tishio kwa
wananchi wanaozunguka ziwa hilo kutokana na ukweli kwamba watu wengi walipoteza
maisha kwa kuliwa ama kuuliwa na mamba pindi wanapoogelea au kuvua samaki.
Jambo la mamba kushambulia watu, lilihusishwa na Imani za
kishirikina, wakati mwingine walikuwa wakitishiana kwamba ukinizingua
nitakutumia mamba akuue. Kwa kweli mamba waliweka hofu kubwa miongoni mwa
wanajamii.
Wataalamu wanasema kuna aina kumi na tano (15) za mamba.
Inadaiwa kuwa mamba anaweza kuishi kati ya miaka sabini (70), mia moja na
hamsini (150) na pengine hadi mia tatu (300).
Wataalamu wanasema kuwa, mamba ana urefu wa mita saba (7) na
ana uzito wa zaidi ya kilo elfu moja 1000 na anakula mara moja kwa wiki kati ya
kilo ishirini (20) hadi ishirini na tano (25).
Sambamba na hilo, mamba akiwa majini ana nguvu sana hata
kama mtu au mnyama akawa na kilo nyingi lakini anakuwa mwepesi anapokamatwa na
mamba majini. Pengine watu wanaoishi karibu na maziwa kama vile; Vikitoria, Tanganyika,
Rukwa, Nyasa bila shaka wanamjua Mamba kwa usahihi zaidi.
Habari hii ya mamba inanirudisha nyuma nikiwa nasoma pale
Kantalamba Sekondari Sumbawanga mwaka 2007-2009 maana tulikuwa tukisimuliwa na
wenyeji jinsi mamba wa Ziwa Rukwa walivyokuwa wakiua watu. Sasa nipo mkoani
Ruvuma bado Habari ni ileile.
Lakini tatizo la mamba kuua watu mwambao wa Ziwa Nyasa
lilikomeshwa na Mzee John Mpembo mstaafu wa Jeshi la Wananchi la Tanzania
(JWTZ) ambaye ni marehemu kwa sasa. Mungu aiweke Roho yake mahali pema peponi
amina!
Pamoja na kwamba mzee Mpembo hatunae tena Duniani,
atakumbukwa zaidi kwa kazi ngumu, nzito na ya hatari ya kuua mamba katika Ziwa
Nyasa ambao walikuwa tishio kwa wananchi wanaolizunguka Ziwa hilo.
Mzee Mpembo, maarufu kwa jina la ‘Mrema’ hawezi kusahaulika na
wananchi wa mwambao wa Ziwa Nyasa mkoani Ruvuma baada ya kufanikiwa kukomesha
tatizo la mamba kuua watu lililohusishwa na imani za kishirikiana ambalo
lilikithiri hasa katika maeneo ya Liuli na Mbambabay.
Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa Habari wa Manispaa ya Songea,
Albano Midelo ambaye alifanya mahojiano na Mzee Mpembo kabla hajafari,
inaonesha kuwa mnamo mwaka 1992, mzee Mpembo alianza jukumu la kupambana na mamba
katika ziwa Nyasa.
Taarifa inaonesha kuwa, Mzee Mpembo alianza operesheni ya
kuua mamba baada ya kupata kibali toka Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 1991
baada ya mauaji ya mamba kukithiri mno na kutishia usalama wa maisha ya watu wanaofanya
shughuli zoa katika Ziwa Nyasa.
Mauaji ya Mamba kwa raia wawili (2) wa kigeni ya mwaka 1991 yalimfanya mzee Mpembo kuomba
kibali wizara ya Maliasili na Utalii ili kunusuru maisha ya watanzania pamoja
na raia wa kigeni wanaozuru Ziwa Nyasa
kwa ajili ya utalii.
Baada ya kupata kibali, Mzee Mpembo alianza operesheni yake
kwa kutumia ndoano maalum iliyowekwa nyama ya mbwa na alifanikiwa kuwaua mamba 607 na kukomesha tatizo hilo.
Kwa sasa matukio ya mamba kuuwa watu yamepungua katika
mwambao wa Ziwa Nyasa jambo ambalo litaongeza chachu ya utalii katika Ziwa
Nyasa.
Kwa mjibu wa Wikipedia, Ziwa Nyasa ni kati ya maziwa makubwa
ya Afrika ya Mashariki likiwa na nafasi ya tatu baada ya Ziwa Viktoria na Ziwa
Tanganyika ya nchini Tanzania. Lina urefu wa km 560 na upana wa km 50-80.
Vilindi vyake vinaelekea hadi mita 704 chini ya uwiano wa maji yake.
Ziwa Nyasa linapatikana kati ya nchi za Tanzania, Malawi, na
Msumbiji. Kusini mwa Ziwa unatoka Mto Shire unaopeleka maji kwenye Mto Zambezi
na hatimaye Bahari Hindi. Kijiolojia ziwa ni sehemu ya Bonde la Ufa la Afrika
ya Mashariki.
Ziwa Nyasa linajulikana kuwa na aina nyingi za samaki (zaidi
ya 1500). Aina chache tu zinavuliwa kama chakula, lakini aina mbalimbali
zinakamatwa na kuuzwa nje ya Afrika kwa wapenzi wa samaki wa rangi.
Kwa mantiki hiyo, Ziwa Nyasa sasa ni sehemu nzuri ya utalii,
hivyo watanzania hatuna budi kufanya utalii wa ndani kwa lengo la kukuza uchumi
wa nchi yetu. Lakini pia, usalama uliopo katika Ziwa Nyasa ni chachu ya utalii
kwa wageni wanaotoka nchi za nje.
Shughuli za kiuchumi katika mwambao wa Ziwa Nyasa kwa sasa
zitakuwa kwa kasi zaidi baada ya kukamilika kwa uundaji wa meli mbili za mizigo
maarufu kama ‘MV Ruvuma’ na ‘MV Njombe’ ambao umekamilika kwa asilimia 99% zitasaidia
kuchochea uchumi wa nchi.
Hivi karibuni
tumeshuhudia Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Transport Bw. Salehe
Songoro akiwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin
Ngonyani wakikagua ujenzi wa meli hizo mbili za mizigo katika bandari ya Itungi
Ziwa Nyasa.
Mantiki hiyo, wafanyabiashara wa Mbeya, Njombe, Iringa,
Ruvuma na nchi jirani za Msumbiji na Malawi hawana budi kutumia Ziwa Nyasa
katika usafirishaji wa bidhaa zao kutokana na uwepo MV Njombe na MV Ruvuma.
Maoni ya wakazi wa Ruvuma
Maoni haya yalitolewa na wakazi wa Mkoa wa Ruvuma kwa njia
ya Mtandao wa kijamii maarufu kama “Facebook”.
Rehema Mapunda anasema kuwa,
kweli imebaki Story, wakati akiwa shule hizo habari za mamba kula watu,
zilikuwa zinatisha mno, na kila mtu aliyekuwa anatoka Nyasa (mnyasa) alimuona
kuwa mchawi, aliamini kuwa ukimuudhi Mnyasa
anaweza kukutumia mamba.
“Kweli Mzee Mpembo (Mrema)
aliutumia vizuri ujuzi wake wa kijeshi kutatua tatizo la mamba kuua watu ziwa
Nyasa, hongera sana mzee wetu na Mungu akulaze mahali pema peponi amina!”,
alisema Mapunda.
Emanuel Liganga anasema kuwa huyo Mzee Mpembo anamkumbuka
sana na alikuwa akishirikiana naye
kutafuta mbwa wa chambo kwa kunasia Mamba, tangu miaka ya1990's.
“Mzee huyu namkumbuka sana mimi, kumbukumbu yangu inaonesha
kuwa mwanzoni mwa mwaka 2002 aliua mamba wawili pale Mbamba Bay baada ya
kuuliwa rafiki yangu na mdogo wangu kipenzi Freddy Mponda. Lakini hiyo idadi ya
mamba aliyoitaja ina ukakasi, sijaiamini, labda aliteleza kwenye kuitaja”,
alisema Liganga.
Kwa upande wake, Nyimbi Ernest alisema kuwa, Habari ya mzee John Mpembo
inamkumbusha mbali sana maana kipindi cha nyuma Nyasa ilisifika kwa uchawi wa
kutumia Mamba kumbe ilikuwa ni Imani
potofu tu. “Siwezi kumsahau mtu maarufu kama John John, hongera kwa kuweka
kumbukumbu muhimu kama hii”, alisema.
Mariot Salimu alisema kuwa, alisikia habari za mzee Mrema na
baadae alifanikiwa kumwona kwa macho yake mawili eneo la LUNDO akiua mbwa kwa
ajili ya shughuli ya uwindaji wa mamba katika Ziwa Nyasa.
(0759 388023)
Post a Comment