Na Padri Titus Amigu
Vijana tunaendelea na mada zetu.
Nadhani nimewapeni muda wa kutosha kutafakari mada yetu ya mwisho, yaani juu ya
imani inayotudumaza ya “uchawi” au “ushirikina”.
Leo nina mada ya ajabu kidogo,
lakini ndiyo itakayoweza kuweka wazi sababu ya malumbano yanayojitokeza au
pengine yanayoendelea kati yetu Wakristo. Kifupi, mzizi mkuu wa malumbano yetu
ni kuwapo kwa Biblia kubwa na Biblia ndogo na hivyo kuwa na Mungu mkubwa na
mungu mdogo.
Wakristo tuna Biblia mbili na hivyo
inaonekana tuna miungu miwili, Mungu mkubwa wa Biblia kubwa na mungu mdogo wa
Biblia ndogo. Hiki ni kisa cha kushangaza, lakini ndivyo kilivyo, na leo
nitasema ukweli ili mambo yawe bayana kwetu sote.
Hiki ni kisa cha Kanisa Katoliki
kuwa na Biblia kubwa na hivyo kuwa na Mungu mkubwa kuliko mungu wa makanisa
mengine.
Hebu nianze na jambo lililo dhahiri
zaidi. Wala hatuna mashaka, tuna Biblia mbili tofauti, Biblia kubwa (vitabu 72
au 73) na Biblia ndogo (vitabu 66).
Kumbe, kwa vile makanisa mengine
yana Biblia ndogo, yaani ya vitabu 66 tu, yana Mungu mdogo. Nahukumu kwa
kufuata maweza yao. Yupo mungu mdogo kwa sababu hajui na wala hawezi mengi
sana.
Mungu mdogo hatofautiani sana na
mimi Pd. Titus Amigu. Atakuwa hajui mengi ya kesho. Atakuwa hakumbuki
alichosema. Atakuwa mwongo. Ataweza kusingiziwa mengi na kadhalika. Mkasa huu
unatokeaje? Unatokea kwa sababu Biblia ya vitabu 66 ni ndogo.
Udogo huu ni pendekezo la mwanadamu
mmoja tu. Ni hivi, udogo huo umetokana na Martin Luther, hapo mwaka 1517
kuchagua kuwafuata Wayahudi wa Palestina ambao walivikataa vitabu vya Wayahudi
wenzao waliokuwa wakikaa huko Aleksandria, Misri.
Wayahudi waliokuwa wakikaa nje ya
Palestina (Diaspora) walikuwa na vitabu vingi zaidi. Inaonekana jamii yao
ilikuwa na waandishi wengi hodari.
Jambo hilo si ajabu. Wamakonde,
Wandonde, Waigbo, Wanubi, Wajerumani, Wamarekani au Wachina wanaokaa nje ya
nchi yao wanaweza kuwa hodari zaidi kuliko watu waliobaki kwao.
Kumbe, Wayahudi waliokuwa wakikaa
nje ya Palestina, ndio Diaspora, waliandika vitabu vingi vizuri. Ndiyo kisa
walipovitafsiri vitabu hivyo katika Kigiriki wakatoka na vitabu vingi zaidi
kuliko wenzao waliobaki Palestina.
Tafsiri hii ya Maandiko ilifanywa
huko Misri chini ya ushauri wa Mfalme Philadelphus (Ptolemy II) katika miaka ya
285 -247 Kabla ya Kristo.
Kwa taarifa yako, Wakatoliki
wanafuata orodha yenye vitabu 45 au 46 katika Agano la Kale na vitabu 27 katika
Agano Jipya. Agano la Kale lina vitabu 45 au 46 kutokana na kusigana katika
kuvihesabu vitabu viwili, kitabu cha Nabii Yeremia na kile cha Maombolezo.
Baadhi ya watu huvihesabu kama vitabu viwili kutokana na kusadiki kwamba
vimeandikwa na waandishi wawili tofauti wakati watu wengine husema vitabu hivyo
vimeandikwa na mwandishi mmoja na hivyo ni kitabu kimoja tu. Kumbe, vitabu
hivyo vikihesabiwa kama viwili, Agano la Kale linakuwa na vitabu 46 wakati
vikihesabiwa kama kimoja , idadi ya vitabu vya Agano la Kale hushuka kwa kitabu
kimoja na hivyo kuwa 45 tu.
Makanisa ya Kiprotestanti hufuata
orodha iliyokuwa au inayofuatwa bado na Wayahudi huko Palestina, orodha yenye
vitabu 24 katika Agano la Kale kutokana na kuvihesabu vitabu vyote 12 vya
manabii wadogo (Hosea, Yoeli, Amosi, Obadia, Yona, Mika, Nahumu, Habakuki,
Sefania, Hagai, Zekaria na Malaki) kama kitabu kimoja. Lakini, vitabu hivyo
vikitenganishwa na kuhesabiwa kimoja kimoja, orodha hiyo hutanuka na idadi ya
vitabu kupanda hadi 39 katika Agano la Kale.
Vitabu saba na sehemu za vitabu
zinazoleta tofauti hiyo ni vitabu vya Tobiti, Yudithi, 1 na 2 Makabayo, Hekina
ya Sulemani, Yoshua ben Sira, Baruku na Barua ya Yeremia pamoja na sehemu
zifuatazo: Wimbo wa Vijana Watatu kwenye Tanuru (Dan 3:24-90), Simulizi la
Susana (Dan 13) na Hadithi ya Bel na Joka (Dan 14).
WAYAHUDI WA DIASPORA WALIKUWA NA
VITABU ZAIDI: Tunaulizana. Kwa nini Wayahudi wa Diaspora walikuwa na vitabu
zaidi?
Asili ya tofauti hii ni ukweli
kwamba hapo zamani kabla ya orodha ya vitabu (canon) vya Agano la Kale, yaani
Biblia ya Kiyahudi haijafungwa rasmi, Wayahudi waliokuwa wakiishi uhamishoni,
yaani nje ya Palestina (Diaspora), walikuwa na vitabu vingi zaidi kuliko vile
walivyokuwa navyo Wayahudi wenzao waliokuwa wakiishi bado huko Palestina
(Israeli au Uyahudi).
Nimeshaomba jambo hili lisichukuliwe
kama ajabu ya pekee sana kwani uandishi waweza kustawi popote pale hata nje ya
nchi fulani. Kwa hali hii, tunaweza kusema kwamba huko nje ya Palestina
walikuwepo Wayahudi waandishi wazuri wengi zaidi.
Ukweli huu unashuhudiwa na taarifa
iliyotufikia kwa kumbukumbu ya Barua ya Aristes. Barua hiyo inasimulia kwamba
Wayahudi wa huko Aleksandria (Misri) walipoonekana wakishindwa kusoma vitabu
vyao vya dini katika lugha ya Kiebrania, mfalme Philadelphus (Ptolemy II)
aliyeishi kati ya 285 na 247 K.K. aliamua kuwasaidia kuvitafsiri vitabu vyao
katika lugha ya Kigiriki kilichotawala katika Diaspora.
Basi, waliitwa watafsiri kutoka
Israeli sita sita kutoka kila kabila la Israeli. Hivi, jumla yao kutoka
makabila 12 ilikuwa 72 (au 70 kwa makumi ya karibu). Barua ya Aristes inasema
watafsiri hao walifungiwa katika vyumba 72 tofauti kila mmoja na kutafsiri
vitabu alivyopewa katika siku 72.
Barua inatangaza ajabu kubwa kwamba
mwishoni mwa kazi yao, tafsiri zao zilipolinganishwa, zilifanana neno kwa neno.
Kumbe, hii ndiyo tafsiri maarufu ya Agano la Kale inayojulikana kwa Kilatini
hadi leo hii kama Septuaginta (yaani 70 ambayo kwa Kilatini huandikwa hivi
LXX).
Lakini ajabu kubwa zaidi ilikuwa
kwamba, kiidadi, vilipolinganishwa vitabu vya Agano la Kale la Septuaginta,
ilizidi vile vilivyokuwa vikisomwa huko Palestina (Israeli au Uyahudi) kwa
vitabu saba na sehemu za vitabu nilizotaja hapo juu.
JE, WAKRISTO WA MWANZO WALIPOKEA
TAFSIRI YA SEPTUAGINTA? Ndiyo, tena ndiyo kubwa, kwani tangu enzi hizo, ndiyo
karne ya kwanza na ya pili, Agano la Kale la tafsiri ya Septuaginta ndilo
lililopokelewa na Kanisa la Kristo.
Hiyo ndiyo tafsiri iliyopokelewa na
kutumika sana na mababa wa Kanisa, kama vile, Tertuliani, Ambrose, Augustino wa
Hippo na kadhalika hasa kwa vile walikuwa weledi wa Kigiriki na hawakujua
Kiebrania cha kutosha.
Zaidi ya hayo, tafsiri ya
Septuaginta ambayo ilikuwa katika Kigiriki ilioana vyema na vitabu vya Agano
Jipya (27) ambavyo tangu mwanzo viliandikwa katika Kigiriki cha kawaida (ndiyo
koine, yaani Kigiriki cha kawaida) wakati vitabu vya Wayahudi huko Palestina
vilikuwa bado vikitumiwa katika Kiebrania, tena Kiebrania cha zamani.
Basi, Agano la Kale la tafsiri ya
Septuaginta likapata kuwa sehemu ya Biblia ya Kanisa la Mungu hata ikatafsiriwa
pamoja na Agano Jipya katika Kilatini cha kawaida (ndiyo Vulgata) na akina Mt.
Jerome, msimamizi wa taaluma ya Biblia.
Kumbe, ndiyo Biblia (LXX na Agano
Jipya) hii iliyotumika na Kanisa na Wakristo wa Magharibi (kwani Wakristo wa
Mashariki, ndio Waorthodoksi wana orodha ya vitabu vya Biblia kubwa zaidi,
yaani vitabu zaidi ya 73) hadi karne ya 16. Septuaginta ilikuwa na vitabu 45 au
46 kujumlisha vitabu 27 vya Agano Jipya na hivyo kufanya Biblia ya Kanisa la
Mungu kuwa na jumla ya vitabu 72 au 73.
Lakini, ajabu ya kupinduka chali
ikatokea katika karne ya 16. Ni katika karne hii, Martin Luther aliposababisha
mtengano wa Kanisa naye kuifumua Biblia kwa kuviondoa vitabu vile saba na
sehemu za vitabu nilizowatajia, yaani, Tobiti, Yudithi, 1 na 2 Makabayo, Hekima
ya Sulemani, Yoshua bin Sira, Baruku na Barua ya Yeremia pamoja na Wimbo wa
Vijana Watatu kwenye Tanuru (Dan 3:24-90), Simulizi la Susana (Dan 13) na
Hadithi ya Bel na Joka (Dan 14).
Ndiyo kusema basi, tangu wakati wa
Martin Luther, Wakristo wote wanaojitenga na Kanisa Katoliki huamua kumsikiliza
Martin Luther na hivyo kuiacha orodha ya Septuaginta (yaani Biblia ya Wayahudi
wa uhamishoni) na kuifuata ile ya Palestina, yaani ile yenye vitabu pungufu kwa
saba na ushehi. Ndiyo kisa basi, hadi leo hii, makanisa yote ya Kiprotestani na
madhehebu yake mapya yanayozaliwa kila kukicha, hufuata orodha yenye vitabu
vichache wakati Kanisa Katoliki likiendelea na orodha ile asilia kwa Wakristo
yaani Septuaginta.
Hivi, kuhusu idadi ya vitabu kwenye
Biblia, asikudanganye mtu yeyote yule, iwe amekujia na “suitcase” au na mkoba
wa ngozi ya mbuzi.
Si kwamba WAKATOLIKI WAMEONGEZA
VITABU kwenye Biblia isipokuwa ni kinyume chake kwani ukweli ni kwamba Martin
Luther AMEVIPUNGUZA VITABU kwenye Biblia.
Usinikodolee macho! Unashangaa nini?
Hii ni hesabu ya kawaida, hata chekechea haiwashindi kuilewa. Kama ukianza na
namba 72 au 73 ukashuka hadi 66 maana yake umetoa au umepunguza.
Ingekuwa kwamba mtu ameanza na namba
66 na kupanda nayo hadi 72 au 73 ingekuwa kweli ameongeza. Kumbe, haikuwa
hivyo, katika historia ya orodha rasmi ya vitabu vya Biblia, yaani canon.
Nadhani tumeelewana kabisa. Haya
tuendelee. Hoja ya kufuata orodha ya vitabu vichache ni kwamba makanisa
yaliyojitenga, kwa kadiri ya mawazo ya Martin Luther, huona kwamba vitabu vile
vya ziada na sehemu zile za nyongeza havikuvuviwa, yaani havikuangaziwa na Roho
Mtakatifu katika uandishi wake.
Ndipo, basi, Wakristo wote
wanaomsadiki, kumsikiliza na kumfuata Martin Luther, huita vitabu hivyo na
sehemu za Maandiko nilizozitaja kwa msamiati wa Kigiriki ‘apokrifa’.
Kumbe, Kanisa Katoliki, kwa upande
wake, linavitambua bado vitabu hivyo pamoja na sehemu zile za nyongeza kwamba
vimevuviwa na kwamba vinastahili kuitwa orodha ya nyongeza, ama kwa maneno
mengine, ORODHA YA PILI ya vitabu vitakatifu, maana vimetoka kwa Wayahudi
wenyewe tena wakati ule ule waandishi wengine wa kimungu walipokuwa
wakiyaandika Maandiko Matakatifu katika nchi ya Palestina (Israeli au Uyahudi).
Ndipo basi, Kanisa katoliki huviita
vitabu hivyo na sehemu nilizokutajia kwa jina lililotoholewa kutoka Kigiriki,
‘DEUTEROKANONI’, yaani ‘ORODHA YA PILI’.
MASWALI MADOGO MAWILI:
Swali 1. Pd Martin Luther alitoa
hoja kuwa havikuvuviwa na Roho Mtakatifu. Lakini Kanisa Katoliki linatambua
vilivuviwa na Roho Mtatikatifu kwa kuwa vilitoka kwa Wayahudi walewale japo
walikuwa uhamishoni.
Je, wakati wa kukusanya vitabu vya
Biblia Wayahudi waliwakataa Wayahudi wenzao waliokuwa uhamishoni walipokuja na
mafundisho ya Biblia ile ile??
Jibu: Ndiyo, Wayahudi waliwakataa
Wayahudi wenzao. Kiujumla, Wayahudi wa Palestina walivikataa vitabu
tulivyovitaja pamoja na sehemu za vitabu ya Esta na Danieli. Walivikataa hasa
kwa sababu Wakristo walikuwa wanavitumia tayari katika kufafanulia mafundisho
yao.
Ndiyo kisa, kuvikataa huku
kulifanyika huko Jamnia mwaka 95 Baada ya Kristo. Kabla yake, vitabu hivyo
vilikuwa vinatumika kwa kujulikana kabisa, kwa mfano kitabu cha Yoshua ben Sira
kilikuwa kikitumika na Wayahudi wote kama kitabu cha kiada katika kuwafundisha
vijana maadili.
Swali 2. Je, Kanisa Katoliki
limezingatia hoja zipi za msingi zinazosahihisha hoja alizotumia Pd. Martin
Luther katika kuvipunguza vitabu hivyo ukiachana na hiyo ya kuvuviwa na Roho
Mtakatifu alikosema.
Jibu: Hoja ya kwanza - kukataa kwa
Martin Luther kunabainisha kwamba hakujua Maandiko Matakatifu maana nukuu za
vitabu alivyovikataa zipo kwa namna moja au nyingine katika nukuu za waandishi
wa vitabu vya Agano Jipya, kwa mfano, Waraka kwa Waebrania na nyaraka kwa watu wote
zaYakobo na Petro.
Hii inamaanisha alikataa kitu
ambacho kipo kwenye Biblia tayari. Ilikuwa kama mtu kukataa nyama iliyokaa juu
ya wali wakati mchuzi wake umeshachanganywa na wali huo huo unaokula.
Hoja ya pili: Mafundisho ya vitabu
alivyovikataa yalikuwa yanajulikana na jumuiya za Kikristo, yalikuwa
hayapingani na mafundisho yaliyokuwa kwenye vitabu alivyovikubali, yalikuwa
mafundisho yanayoweza kuhimiza imani na upendo na kadhalika, mambo ambayo kwa
yenyewe yalikuwa vigezo (criteria) vya kuteulia vitabu vilivyoingia katika
orodha ya vitabu vya Agano Jipya vilivyoandikwa na Wakristo wenyewe.
Huenda nimekuporomoshea mambo mapya
mno na huenda, kichwani na moyoni mwako, unadhani nimesahau hoja ninayoijenga.
La hasha! Nimekutaarifu kwamba Biblia ya Wakristo ilipunguzwa kutoka vitabu vya
asilia 72 au 73 hadi vitabu 66.
Kwa mkasa huo, Biblia ilifanywa
NDOGO na kwa kufanywa huko ndogo Mungu akakumbwa na balaa la kupunguzwa kutoka
Mungu mkubwa hadi kuwa MUNGU mdogo.
Kwa nini? Kwa sababu mambo anayoshuhudiwa
katika vitabu vile 7 na sehemu zilizokanwa na Martin Luther yatakanwa kwake.
Sasa hivi nitakupa mifano kusudi usipupe pupe kana kwamba nimekunasisha kwenye
mtego wa kware. Katika mada zote nakusudia kukuelimisha vyema.
MIFANO YA KUPUNGUZA VITABU SABA
KULIVYOATHIRI MAFUNDISHO YA KIKRISTO
1. KWA KUKATAA KITABU CHA TOBITI,
lazima mtu ukatae fundisho la watakatifu na malaika kuwa na uwezo wa kuwaombea
wanadamu kwa maana jambo hilo limeshuhudiwa na Tobiti 12:11-21. Hapa
pameandikwa hivi:
“‘Sasa nitawajulisheni ukweli wote
bila kuwaficheni chochote. Nilikwishawaambia kwamba yafaa kuitunza siri ya
mfalme, lakini matendo ya Mungu lazima yatangazwe kila mahali kama ipasavyo.
Tobiti! Wewe ma Sara mlipokuwa
mnasali wakati ule, mimi ndiye niliwasilisha sala zenu mbele ya Bwana aliye
mtukufu. Na kila ulipokuwa unawazika wafu, mimi niliwasilisha matendo yako
mbele yake.
Wakati wewe hukusita hata kidogo
kuinuka na kukiacha chakula ukaenda kumzika mtu aliyekufa, Mungu alinituma
nikujaribu. Lakini pia alinituma kukuponya na kumwokoa mke wa mwanao, Sara.
Mimi ni Rafaeli, mmoja wa wale malaika saba wanaokaa tayari daima mbele yake
Bwana aliye mtukufu kumtumikia’.
“Tobiti na Tobia wakashikwa na hofu
kubwa, wakasujudu wakiogopa sana. Lakini Rafaeli akawaambia: ‘Msiogope! Muwe na
amani. Mtukuzeni Mungu milele.
Mimi nilipokuwa kati yenu haikuwa
kwa kutaka kwangu mwenyewe, bali kwa kutaka kwake Mungu. Yeye ndiye mnayepaswa
kumsifu.
Ninyi mlidhani mliniona nikila
chakula, lakini ni kwa kuonekana tu na haikuwa hivyo. Basi, sasa mtukuzeni
Bwana duniani na kumshukuru. Mimi narudi sasa kwake yeye aliyenituma kutoka
juu.
Andikeni mambo hayo yote
yaliyokukia.’ Kisha Rafaeli akatoweka, wasimwone tena. Basi, wakamsifu Mungu
kwa nyimbo, wakamshukuru kwa ajili ya matendo yake makuu aliyowafanyia malaika
wake Mungu alipokuwa amewatokea.”
Kumbe, kama huna kitabu hiki katika
Biblia yako lazima ushindwe kujua na kukubali kweli mbili: mosi, kwamba malaika
na watakatifu wanawasilisha sala mbele ya Mungu nao wanaripoti juu ya matendo
yetu mema.
Kumbe, ni kwa sababu ya ukweli huu,
Wakatoliki hawasiti kuwaomba malaika na watakatifu mbalimbali wawaombee kwa
Mungu. Hapo ndipo zinapoingia sala na ibada mbalimbali kwa Bikira Maria
AWAOMBEE wanadamu wote, wema kwa wakosefu, wazima kwa wafu.
Ukweli huu unaungwa mkono kwa
kiashirio kizuri kilicho katika maombezi ya Maria kwa Yesu ili waliokuwa
wanaishiwa divai wasaidiwe (soma Yn 2:1-12).
Pili, kwamba Bikira Maria, malaika
na watakatifu hawaabudiwi isipokuwa kupitia kazi zao na maombezi yao Mungu
anatukuzwa.
Hakika ukisoma vizuri Tobiti
12:11-21, utajua kwamba Bikira Maria, malaika na watakatifu hawaombwi kwa
wenyewe bali wanaombwa wasimame kama waombezi wa wanadamu “wanaolimbana” na
malimwengu haya yanayowachachafya.
Lakini kutokana na mtu kukataa jambo
mahali fulani, hulazimika akatae popote na chochote kitakachoelekea kupindua
msimamo wake. Kumbe, kanusho moja huzaa kanusho lingine hata kama ni kwa
kulazimisha tu.
Ndiyo kisa basi, mtu anaposhuhudia
mambo ya watakatifu kuwa na uwezo wa kuombea kwa kunukuu Ufu 5:8, 8:3-4, huwa
kama anayechota maji kwa pakacha tu.
2. KWA KUKATAA KITABU CHA HEKIMA YA
SULEMANI, lazima ukatae fundisho la Hekima (Roho Mtakatifu au Yesu Kristo) kuwa
Nafsi ya Mungu kwa maana jambo hilo limeshuhudiwa na Hekima ya Sulemani 9:
6.9-12.
Hapa pameandikwa hivi:
“Hata kama mtu yeyote akiwa
mkamilifu kiasi gani, bila Hekima atokaye kwako atakuwa bure tu. Hekima yupo
pamoja nawe, naye ajua matendo yako, alikuwa pamoja nawe wakati ulipouumba
ulimwengu.
Hekima anajua yanayokupendeza na
yaliyo sawa kulingana na amri zako. Umpeleke, basi kutoka mbingu tukufu, kutoka
kiti chako cha enzi kitukufu, ili akae nami na kufanya kazi pamoja nami, nipate
kujifunza yale yanayokupendeza, maana Hekima anajua na anaelewa mambo yote,
naye ataniongoza kwa busara katika matendo yangu, kwa utukufu wake atanilinda,
hapo matendo yangu yatakubalika, nitawahukumu watu wako kwa haki na kustahili
kuwa katika kiti cha enzi cha baba yangu.”
Basi, kama huna kitabu hiki katika
Biblia yako lazima ushindwe kuujua na kukubali ukweli kwamba katika Mungu kuna
Nafsi, Mwana na Roho Mtakatifu.
Kama hutakaidi kabisa basi utasema
Yesu alikuwa ni mwanadamu mwema tu na Roho Mtakatifu nguvu za Mungu kutendea
kazi tu. Huko ndiko kutakuwa kuzikana Nafsi mbili za Mungu kati ya tatu
tunazopaswa Wakristo kuzikiri.
3. KWA KUKATAA KITABU 2 MAKABAYO,
lazima ukatae uhalali wa kuwaombea marehemu kwa maana jambo hilo limeshuhudiwa
na 2Mak 12:38-45.
Hapa pameandikwa hivi:
“Kisha Yuda aliwaongoza watu wake
kwenda mjini Adulamu. Hiyo ilikuwa siku kabla ya Sabato, kwa hiyo wakajitakasa
kadiri ya desturi ya Kiyahudi, kisa wakaadhimisha Sabato hapo.
Siku iliyofuata waliona ni harakia
na muhimu kukusanya miili ya wenzao waliokuwa wameuawa vitani, na kuizika
katika makaburi ya wazee wao.
Lakini katika kila maiti, walikuta
zimefichwa nguoni sanamu ndogondogo za miungu iliyoabudiwa Yamnia, jambo ambalo
sheria inawakataza Wayahudi kuzivaa. Hapo kila mtu alijua kwa nini hao walikuwa
wameuawa.
“Hivyo, wakazisifu njia za Bwana,
hakimu mwenye haki, afichuaye vilivyofichika na wakamwomba Bwana awafutilie
mbali dhambi hiyo.
Kisha Yuda yule mtu mwadilifu,
akawataka watu waepuke dhambi, kwa sababu walikuwa wamejionea wenyewe
yaliyokuwa yamewapata wale waliokuwa wametenda dhambi.
Pia alichangisha kutoka kwa watu
wake fedha ipatayo drakma elfu mbili akapeleka Yerusalemu kwa ajili ya dhabihu
ya kuondolea dhambi.
Yuda alifanya tendo hilo jema kwa
sababu aliamini juu ya ufufuo wa wafu. Kama asingekuwa na imani kwamba wafu
watafufuliwa, ingekuwa ni upumbavu na kazi bure kuwaombea marehemu.
Lakinii akiwa anatazamia tuzo nzuri
waliowekewa waliokufa wakiwa waaminifu kwa Mungu hilo lilikuwa wazo jema na
takatifu. Kwa hiyo, Yuda alitolea dhabihu ya upatanisho ili wapate kuondolewa
dhambi zao”.
Kama huna kitabu hiki katika Biblia
yako lazima ushindwe kuujua na kukubali ukweli huu. Wakatoliki huwa tunawaombea
marehemu si kwa sababu tunampelekea Mungu maombi mapya la hasha, ila kwa sababu
sala zetu zilishajulikana na Mungu kabla mtu yule hajafa, wakati mtu anakufa na
baada ya mtu yule kufa.
Mungu anayejua yaliyopita, yaliyopo
na yajayo ndiye Mungu mwenyezi. Mungu asiyejua hivyo si mwenyezi, huyo ni sawa
na Pd. Titus Amigu tu.
4. KWA KUKATAA KITABU CHA YOSHUA BEN
SIRA, lazima ukatae mafundisho ya ulazima wa imani kuwekwa katika matendo kwa
maana jambo hilo limekaziwa na kitabu kizima.
Kitabu hiki kilichokuwa kikitumiwa
kama kitabu cha kiada mwanadamu anahimizwa aishi vyema maana ndilo deni kwa
akili na utashi alivyopewa kwa kutofautishwa na wanyama wafugwao na hayawani
wanaoishi kwa silika tu.
Yoshua ben Sira inazungumzia uzuri
wa kuishi kiadilifu katika kila uwanja, malezi, kazi, urafiki, heshima, ndoa na
kadhalika. Kumbe, kwa kukikataa kitabu cha Yoshua ben Sira sawa na Hekima ya
Sulemani, lazima mtu akane umuhimu wa matendo katika kumtafuta Mungu naye
ajikite zaidi kwenye misimamo ya “kwa neema tu” na “kwa imani tu” maana huna
mafundisho mazuri juu ya matendo yaliyotukuka. Kumbe, hapo ndipo alipolazimika
Martin Luther kuishia.
5. KWA KUTAA KITABU CHA YOSHUA BEN
SIRA TENA, lazima ukatae mafundisho ya uhalali wa kunywa divai kwa wakati wake
na kiasi chake kwa maana jambo hilo limeandikwa katika YbS 31:25-31. Hapa
pameandikwa hivi:
“Usijioneshe kwuwa hodari wa kunywa
mvinyo, maana mvinyo umewaangamiza wengi. Tanuru hupima ugumu wa chuma na
mvinyo hupima mioyo ya watu katika shindano la wenye kiburi. Mvinyo ni kama
uhai kwa mtu ukinywa kwa kiasi.
Maisha yafaa nini bila mvinyo?
Imeumbwa iwafurahishe wanadamu. Kunywa mvinyo wakati wake na kwa kiasi, kwaleta
shangwe moyoni na furaha rohoni. Lakini kunywa mvinyo kupita kiasi kunaleta
kuumwa kichwa, uchungu na fedheha
Ulevi huongeza hasira ya mpuumbavu
akajiumiza mwenyewe. Humdhoofisha na kumwongezea majeraha. Usimkaripie jirani
yako kwenye mvinyo, wala usimdharau anapoifurahia karamu. Usimwambie neno la
kumwonya wala umsimsumbue kwa kumtaka alipe deni”.
Kumbe, kama huna kitabu hiki katika
Biblia yako, lazima ushindwe kuujua na kukubali ukweli wa kwamba divai si
haramu ikinywewa kwa wakati wake na kwa kiasi.
Lakini, huu ndio ukweli uliomruhusu
Yesu awe anakula na kunywa anapoalikwa na vile vile uliomruhusu awape watu
waliokuwa kwenye sherehe ya harusi ya Kana divai (“oinos” siyo “gleukos”) ya
kutosha.
6. KWA KUKATAA KITABU CHA YOSHUA BEN
SIRA TENA, lazima ukatae fundisho la sakramenti ya Kitubio au Upatanisho kwa
maana fundisho hilo limedokezwa katika YbS 5:4-7. Hapa pameandikwa hivi:
“Usiseme, ‘Nimetenda dhambi lakini
nimepata balaa gani?’ Usitegemee kupata msamaha hata kuongeza dhambi juu ya
dhambi. Usiseme, ‘Huruma yake ni kubwa, yaye atanisamehe dhambi zangu nyingi’.
Kumbuka, yeye ana huruma na ghadhabu
na hasira yake huwakumba wenye dhambi. Usichelewe kumrudia Bwana wala
usighairishe kurudi siku hata siku. Maana ghadhabu ya Bwana itakuwakia ghafla
na wakati wa hukumu utaaangamia.”
Hali kadhalika, KWA KUKATAA KITABU
CHA BARUKU, lazima ukatae pia fundisho la sakramenti ya Kitubio au Upatanisho
kwa maana fundisho hilo limedokezwa vile vile katika Baruku 4:27-30. Hapa
pameandikwa hivi:
“Jipeni moyo wanangu na kumlilia
Mungu kwani yeye aliyewaleteeni jambo hilo atawakumbukeni. Kama vile
mlivyokusudia kwenda mbali na Mungu vivyo hivyo rudini na kumtafuta kwa hamu
mara kumi zaidi.
Hivyo, huyo aliyewaleteeni balaa
hizi atawaokoeni na kuwaleteeni furaha ya kudumu milele. Jipe moyo, ee
Yerusalemu, Mungu aliyekuita kwa jina lako atakufariji.”
Kumbe, kama huna kitabu cha Baruku
katika Biblia yako, lazima ushindwe kuujua na kukubali ukweli huu kwamba Mungu
alikusudia kuwaasisia wanadamu sakramenti ya Upatanisho au Kitubio.
Sakramenti hii ndiyo sakramenti
inaiyotendea haki sadaka ya msalaba aliyoitolea Yesu kwa ufanisi mkubwa.
7. KWA KUKATAA KITABU CHA YOSHUA BEN
SIRA TENA, lazima mtu ubaki katika utumwa wa kuamini ndoto hata baada ya Yesu
kuufikisha ufunuo kileleni (Mk 9:7-8, Ebr 1:1-4).
Lakini neno la Mungu lasema ndoto
zote ni upuuzi, isipokuwa zile zitokazo kwa Mungu tu (yaani zinazotokea mara
kadhaa, kuwa na ujumbe maalumu na ujumbe wake kutopingana na mafundisho ya
Kanisa). Jambo hili limeandikwa katika YbS 34:1-8.
Hapa pameandikwa hivi: “Mtu mjinga
huwa na matumaini ya bure na ya uongo. Ndoto humpa mpumbavu mabawa ya kuruka.
Kama mtu anayejaribu kushika kivuli na kufukuza upepo ndivyo alivyo mtu
anayeamini ndoto. Ndoto ni kama kioo, sura inayoukabili uso.
Ni kitu gani kiwezacho kutakaswa na
uchafu? Je, ukweli waweza kupatikana kwa uongo? Kupiga bao, ramli na ndoto ni
upuuzi, akili huwa na mawazo kama ya mama anayejifungua.
Usizitie maanani ndoto isipokuwa
kama zinatoka kwa Mungu Mkuu. Maana ndoto zimewadanganya wengi na wale
wanaozitumaini wameaibishwa. Sheria ni kamili bila udanganyifu huo, nayo hekima
ni kamilifu kwa mtu mwaminifu.”
Kumbe kwa kutumia Biblia ndogo, kwa
maana ya kwamba isiyo na kitabu cha Yoshua ben Sira mwanadamu utaendelea na
kusumbuka kutafuta maana ya kila ndoto. Zaidi ya hayo, utanunua vitabu vyote
vinavyodaiwa kutafsiri ndoto za watu na hali kadhalika kuhangaika kuwaendea
“wafasiri wa ndoto” wote ijapokuwa wenyewe ni waongo wasiojua jambo lolote la
ajabu.
8. KWA KUKATAA KITABU CHA YOSHUA BEN
SIRA TENA, lazima mtu ukatae uhalali wa dawa za asili hata kama zinatumiwa kwa
uadilifu kwa maana jambo hilo limeandikwa katika YbS 38:1-14. Hapa pameandikwa
hivi:
“Mpe daktari heshima anayostahili,
kwa sababu ya huduma zake kwako, kwa vile naye aliumbwa na Bwana. Maana kipaji
chake cha kuponya chatoka kwa Mungu Mkuu naye hupata zawadi kutoka kwa mfalme.
Ujuzi wa dakrari humfanya maarufu,
naye huheshimiwa miongoni mwa wakuu. Bwana aliumba dawa zote kutoka ardhini na
mtu mwenye nusara hawezi kuzidharau. Je, si kwa kijiti maji yaligeuzwa kuwa
mazuri ili Mungu awaoneshs watu nguvu zake?
Bwana aliwapa watu maarifa na ujuzi
ili atukuzwe katika kazi zake za ajabu. Kwa dawa huwapaonya watu na kuondoa
maumivu, mchanganya dawa hutengeneza mchanyiko wake. Kazi za Bwana hazina
mwisho, afya yote duniani hutoka kwake.
“Mwanangu, ukiugua usiwe mzembe juu
ya ugonjwa, bali mwombe Bwana naye atakuponya. Acha makosa yako, uamue kutenda
mema, na kutakasa moyo wako dhambi zote. Mtolee Bwana dhabihu ya harufu nzuri
na dhabihu ya unga safi.
Umiminie dhabihu zako mafuta kadiri
unavyoweza kupata. Kisha mengine mwachie daktari maana Bwana ndiye aliyemuumba;
usikubali akuache maana unamhitaji. Kuna wakati ambapo kupona kuwategemea
madaktari.
Maana nao pia wanamwomba Bwana ili
awape mafanikio katika uchunguzi wao na katika kuponya ili kuokoa maisha. Mtu
aliyetenda dhambi dhidi ya Muumba wake mwache aangukie mikononi mwa daktari.”
Kumbe, usipokuwa na Biblia yenye
nukuu hii, utakuwa “unapinduka pinduka tikitaka” nyingi za kiakili kutaka
kuhakikisha kwamba dawa za asili, kwa zenyewe, ni haramu.
Nakomea hapa.
Nadhani nimekujengea vyema hoja na
kukutolea mifano mizuri kwamba makanisa mengine yana mungu mdogo kwa sababu ya
kutumia Biblia ndogo. Kitendo cha kupunguza vitabu vya Biblia kutoka 72 au 73
hadi 66 kimetupa nje mafundisho mazuri ya Kanisa na kubana uelewa wa mafundisho
yanayodumishwa na Kanisa Katoliki. Matokeo yake ya jumla ni kuzaliwa kwa
mabishano endelevu kwa sababu ya kutofautiana vitabu vya rejea.
Na hili ni jambo la kawaida kama
watu wanajadiliana jambo, tuseme la Fizikia, hawawezi kuelewana ikiwa mmoja anatumia
muhtasari wa darasa la saba (yaani muhtasari mdogo) wakati mwingine anatumia
kitabu cha Sekondari kwa mfano kitabu cha A.F.ABBOT.
Kumbe, mtu anayehama kutoka Kanisa
Katoliki, Kanisa lenye Biblia kubwa na hivyo lenye Mungu mkubwa na kuhamia kanisa
lenye Biblia ndogo na hivyo kujihusisha na mungu mdogo lazima ajiunge katika
taabu ya kwanza kujielewesha na kishapo kuyatetea mafundisho madogo. Naomba
mnipate uzuri. Kwa heri kwa leo pia!
Post a Comment