Ads (728x90)

Powered by Blogger.




UTANGULIZI

Wataalamu wa elimu ya nafsi ya mtu au roho (Psychology) pia elimu inayochunguza habari zinazohusu asili na maendeleo ya binadamu tangu awali (Anthropology) hutuambia kwamba binadamu licha ya kumwogopa, kuhofu na kumwabudu Mungu aliye muumba wake, binadamu huyo kimaumbile anayo tabia ya kuvihofu viumbe vinavyomzidi nguvu kama vile radi, umeme, mito mikubwa, milima, mapango, mawe, wanyama, mizimu, mashetani na hata vitu vinavyoitwa “majini”.

Kutambikia vitu hivyo, hata kuvitolea sadaka ni kudhihirisha hofu waliyonayo wanadamu kwa viumbe hivyo, badala ya kumwabudu Mungu mmoja muumba wa vitu vyote ambaye kadiri ya falsafa ya kweli na maandiko matakatifu tunahakikishiwa kuwa yupo. 

Majini ambayo huogopwa na watu wengi katika Afrika na sehemu nyingine duniani, kwa kufikiria kuwa wasipo yaheshimu na kuyaabudu au kuyatolea sadaka yanaweza kuleta hasara kwa watu mfano kupagawa kwa wanawake na watoto, kuleta mabalaa, kuleta mikosi, magonjwa, vifo, kupotelewa na mali n.k.

Kadiri ya ufunuo wa Mungu kutoka maandiko matakatifu pia elimu ya kweli ya falsafa kuna Mungu mmoja tu anayetakiwa aabudiwe, kuna viumbe ambavyo ni rafiki za Mungu na wanadamu ndio “Malaika” yaani malaika wema, na maadui wa wanadamu ni mashetani, pepo wabaya au malaika wabaya. Hakuna viumbe waitwao majini kadiri ya maandiko matakatifu. 

Kama watu wanayaheshimu majini, wanayatolea sadaka kama miungu, wanayaomba basi hapo binadamu wamedaganyika na kupotea. Wasije wakafikiri wanayaheshimu majini kumbe ni yaleyale mashetani kwa kutofahamu kuyaainisha au kuyatofautisha kwa kukosa ufunuo wa kweli juu ya viumbe hao waitwao “Majini”
 
HISTORIA YA MAJINI KATIKA MATAIFA MBALI MBALI

Ukitazama historia ya mataifa mbali mbali hapo kale unaweza kugundua na kuona vitu vichache vinavyoonyesha mwelekeo unaoashiria kuwa watu wamewahi kuyaabudu  hayo majini pengine hata kuyaheshimu kwa vikubwa kama vile miungu, hasa pale unapozisoma hadithi za makabila, mataifa, koo mbalimbali zinazowakilisha umaarufu wao, chimbuko lao au matendo ya umashuhuri, ujasiri, nyakati n.k. 

Hadithi hizo ni (fictitious) za kubuni na hata mara nyingine zinaogofya. Kwa lugha ya kizungu zinaitwa “Myths”. Hadithi hizo zilihadithiwa kwa kitambo kirefu na hivyo kuonekana kama ukweli. Baadhi yake 
zinahusika na miungu ya kike au kiume. Zipo hadithi kama vile:
Faun: Mmoja wapo wa miungu ya vijijini ya huko Roma, mwenye sura ya mtu binadamu, mwenye pembe na mkia. Yeye hufananishwa na mungu wa vijijini ahusikaye na Roho ya maumbile, upagani n.k. mahali pengine Faun huonyeshwa akiwa na kiwiliwili cha nusu mwanadamu mwenye pembe na kuanzia kiunoni ana sura ya mbuzi, miguu na kwato.

Sphynx: ni mnyama mkubwa (Monster) mwenye sura ya Simba , mabawa na kichwa cha mwanamke Sphynex wa Thaebes aliwatega watu wa mahali hapo kitendawili, wale wote walioshindwa waliuawa.
Oedipus aliyekuwa ameketi katika mwamba ambao huyo Sphynx alikalia  alipotegua kitendawili hichoalimteremsha kutoka mwamba huo na kumwangusha akaanguka anguko la kujiua. 

Hivyo ndivyo Oedipus alivyopata kuwa mfalme wa Thaebes. Kitendawili chenyewe kilikuwa hiki; “ni kiumbe gani kinachotembea asubuhi kwa miguu minne, mchana kwa miguu miwili, na jioni kwa miguu mitatu?”
Satyr: ni moja wapo wa miungu ya kigiriki wa msituni. Anaonekana akiwa na kiwiliwili cha mwanadamu na masikio ya farasi pia na mkia. Waroma nao wanamwonyesha akiwa na kiwiliwili cha mwanadamu mwanaume na masikio ya mbuzi, mkia, miguu na pembe zilizokunjika. Ni mojawapo wa Miungu inayohusika na ashki na ufuska wa kila aina kama tunavyoona duniani hivi leo.

Cyclops: hayo ni majitu makubwa yenye sura ya watu lakini wana jicho moja katikati ya uso. Hadithi yao imehusika na kisiwa cha Sicilly, wakiwa wachungaji chini ya mlima Etna Laocoon: wale waliosoma riwaya za kilatini kuhusu Trojan Horse wanafahamu sana habari hiyo. Yule kasisi aliyekuwa amepelekwa na Athena. Athena: ni mojawapo wa miungu ya kike ya olympia, mashuhuri kwa siasa, utendaji, vita na amani. 

Anao uhusiano na Minerva. Minerva: ni mmoja wapo wa miungu ya kike ya kiroma ahusikaye na hekima. Mrille: ni mojawapo ya hadithi za wachaga  pamoja na Mregho. Hadithi hizi mbili za wachaga zinaongea juu ya wivu na ukombozi, tambiko na msaada safi na ya kumtuliza Mungu. Sadaka yenye kukubalika (Effecacious). 

Hizi nazo nyingi nyinginezo zinaonyesha machimbuko ya vitu fulani fulani, nyinginezo zina mafundisho ya aina moja au nyingine. Kumekuwako na waliothubutu kusema yale yaliyoandikwa katika kitabu cha Mwanzo ni “Myth”, Sio ajabu basi kwamba wengine walivutwa na hadithi hizo wakazipa hadhi na mtazamo wa kuwa na ukweli, na hata wakashikwa na jinamizi walipozipanga majina ya “Majini”.

FALSAFA YA KWELI NA UWEPO WA MUNGU

Falsafa ni neno litokanalo na maneno mawili ya kigiriki yenye maana ya “upendo” na “hekima”. Kwa hiyo neno “Falsafa” lina maanisha “upendaji hekima” falsafa  hujishughulisha na utafutaji wa ukweli katika mambo yote na jinsi ya kushikamana na ukweli katika mambo yote. Falsafa huanza kwa njia ya mshangao yaani kitu cha kushangaza kwetu sisi falsafa hukiona cha kawaida tu.

Falsafa inakufanya uwe huru kufikiri na kujitegemea kimawazo na kimaoni. Binadamu asipokuwa na falsafa yoyote humfanya aonekane  kama hana faida katika jamii. 

Falsafa humsaidia mtu kushinda ndoto zake  za mambo fulani. Ni kweli kuwa jinsi kila mmoja anavyofikiria hutegemea jamii, elimu, mazingira, utamaduni, dini, uchumi, tabia na siasa inayomzunguka.
Lakini falsafa inajishughulisha na mambo makuu matatu: yaani Mungu, binadamu na Dunia. Falsafa humsaidia mtu kuwasilisha mawazo yake katika mtiririko wa mawazo mantiki 

inatuonyesha kwamba haiwezekani pakawepo na Miungu mingine kama yule mmoja wa kweli, pia binadamu ameumbwa na Mungu, katika falsafa hakuna mahali panapoonyesha miungu ilimwumba binadamu.
Plato na Socrates walikuwa katika kipindi ambacho watu wengi wa ugiriki walikuwa wakiabudu miungu mingi,  halikuwepo wazo la Mungu mmoja kama tuelewavyo siku hizi. Lakini wanafalsafa hao waliamini juu ya kiumbe kilicho “kikuu” na “kikamilifu” kuzidi vyote. 

Socrates aliamini kuwa kuna Mungu mmoja anayezidi miungu mingine yote.
Plato naye aliamini juu ya Mungu mkuu aliyemwita Demiurge, Mungu huyo alifikiriwa  kuwa na uzuri na ukamilifu wote. Zaidi ya hilo wanafalsafa wote waliojua kuwa Mungu yupo na wale waliojidai kukanusha kuwa Mungu hayupo walijikuta wanafafanua uwepo wa Mungu kwa namna moja au nyingine.

MAJINI NI MASHETANI, PEPO WABAYA AU MALAIKA AMBAO YESU ALIWAWINGA

Katika Biblia upande wa Agano la Kale na Agano Jipya husema ukweli wa ulimwengu wa roho katika ulimwengu huo usioonekana kuna viumbe vya kiroho visivyohesabika.

Kwa kawaida huitwa “Malaika” hao malaika wengine humtumikia Mungu kwa hiari yao, ingawa wengine walimwasi (Yuda 6) malaika wale walioasi au kuanguka wana majina mbali mbali  kama vile Majini, pepo wachafu, majeshi ya kiroho ya uovu, falme, malaika wakuu wa giza, mamlaka ya uovu ya ulimwengu wa kiroho, mashetani, malaika wa mashetani. Kiongozi wao ni Shetani (Lk 10:12, Kol 2:15, Yoh2:19, Ufu 12:9)

Katika uhusiano wa huduma ya Yesu “Majini” hayo  mara nyingi huitwa pepo wachafu (Mt 10:1,8 Mk 6:13).
Majini humpinga Mungu nalo ni jeshi la kiroho katika dini za kipagani na Miungu ya uongo (Kumb 32:17, Zab 106:37, Ikor 10:19-20, Ufu 9:20) watu wafuatao dini hizo kwa kawaida huogopa sana majini na mara nyingi hutumia uchawi ili kushindana na nguvu za shetani. 

Lakini Mungu anakataza uchawi wa aina yeyoye kwa sababu mambo hayo yanawaingiza watu katika ushirikina na nguvu zile za uovu wa kiroho (Law 19:26, 20:6, Kum 18:10-12, Gal 5:20, Uf 9:20-21, 21:8).
Shughuli ya pekee ambayo Bwana Wetu Yesu Kristo alikuwa nayo dhidi ya Majini ilikuwa ni kuwahukumu kabisa. Alileta hukumu ya Mungu juu yao na kuwaweka watu huru waliobanwa na nguvu hizo (Mk 1:27, Lk 8:2, 13:32, Mdo 10:28). Mamlaka ya Yesu juu ya majini ilikuwa ni ishara kwamba ufalme wa Mungu ulikuwa umefika (Mt 12:28).

Yesu aliwapa wafuasi wake nguvu za kufukuza au kuondoa Majini (Mt 10:1,8, Lk 10, 10:17-18, Mdo 16-18) na uwezo wa kufafanua kama manabii katika Kanisa walisema kwa ushawishi wa Majini au uongozi wa Roho wa Mungu (IKor 12:3,10, ITim 4:1, IYoh 4:1-3) si kila kazi ya kishetani iko wazi na yenye ajabu.
Majini yanashughulika katika kila sehemu ya maisha ya wanadamu nayo hupenda kufanya kazi katika Jumuiya ya wanadamu 2Kor 11:14, Efe 2:2-3, 6:12, Yak 3:15). 

Mkristo anapaswa kujihadhari sana na makusanyiko yao maovu, lakini hana haja ya kuogopa. Kristo aliyashinda kwa njia ya kufa na kufufuka kwake na Mkristo anaweza kudai ushindi huo kwa ajili yake (Kor 2:8-10, 15). 9Taz. Pia Rum 8:38-39, Efe 1:18-21)

Maonyesho ya mwisho ya ushindi juu ya Majini yatakuwa katika hukumu ya mwisho, Mungu atayaondoa kutoka jumuiya ya binadamu mpaka milele na kuyatupa mahali pa adhabu inayofaa (Mt 8:29, Yuda 6). Kadiri ya maandiko matakatifu yanatuonyesha uwepo wa malaika na mashetani ambao ni malaika wabaya.
Yatueleza pia uwezo wa malaika na mashetani. Soma katika kitabu cha Ayubu uone uwezo wa Mashetani.
Soma katika kitabu cha Ufunuo uone uwezo wa malaika wema. Maandiko matakatifu hayaongei chochote kile juu ya majini kuwa tofauti na viumbe waitwao Mashetani, pepo wabaya au Malaika wabaya walioasi na kufukuzwa na Mungu. Basi hakuna viumbe wanaoitwa majini kama Majini tofauti na Mashetani.
 
MTAZAMO WA WATU JUU YA MAJINI
 
(A) WATU WA KAWAIDA
Watu wa kawaida huongea lugha ya kakara juu ya majini bila kuainisha na hata pengine kujivuruga wao wenyewe na kupata fadhaa mara nyingi. Watu huongelea juu ya jini lenye jinsi ya kiume na kike.
Tafakari nzuri huonyesha kuwa watu hao huyatazama majini kama viumbe vyenye uhai. Mara nyingi watu hao huongelea majini kama wanadamu wenye kwato na Miguu kama wanyama na kiwiliwili cha mwanadamu, matendo yao yamekuwa ya mwanadamu, ya wanyama na hata roho wabaya.
 
(B) WATU WA IMANI YA KIISLAMU

Kwa kweli Waarabu walikuwa na imani hiyo ya Majini ambayo baadaye iliingia katika dini ya Kiislamu tangu zamani. Kwani inawataja kama viumbe wa kawaida wanaojulikana kwa wote.
Ni viumbe walioumbwa kwa ulimi wa moto (Kur 55:16) wenye kuishi katika maji na bara siyo malaika walioshushwa cheo na kuadhibiwa, lakini waliumbwa kwa moto wa upepo wenye shari (Kur 15: 28), hakuna uhusiano wowote kati yao na Mungu bali wametupwa, bila shaka watahudhurishwa (Kur 37: 159) wana jamaa zao sawa na watu (Kur 46:19). 

Wanaweza kutenda dhambi (Kur 72:6) ni wa kiume ama wa kike, wenye kuzaa (Kur 72:7) wanahusika na ufunuo: kundi moja la majini walisikika wakisema: “Hakika tumeisikia kurani ya ajabu (Kur 72:2).
 
(C) MAANA YA MAJINI

Kadiri ya kamusi ya Kiswahili roho za watu waliokufa hawaangaliwi kama  majini, pepo nao hawaonekani kama majini. Mizimu au kuzimuni  ni mahali ambapo vivuli vya wazee waliokufa zama za kale hukutanika na kusikiliza maombi yetu hasa watu walio hai wanapokwenda kuomba.
Mahali pa kutambikia, mahali ambapo ni makao ya pepo wakubwa kati ya pepo wote wa wenyeji sehemu fulani. 

Kwa kawaida hao huwa kwenye pango, mbuyu, mkuyu au mgandi na miti mingine kwa kuwa pepo wakitajwa tunaendelea kuuliza pepo ni viumbe wa namna gani?.
Kamusi hiyo inatuambia kwamba pepo ni jamii ya viumbe walioumbwa kwa moto na ambao hawaonekani kwa macho. Je shetani na majini ni pepo?. 

Tena linafuata swali jingine. Je pepo ni Roho? Watu hutumia maneno hayo bila kuyahainisha wanachanganya maharage na mchanga  au mchele na mtama. Hata hivyo Je majini yapo katika idadi hiyo?.
Kamusi hiyo hiyo inasema kuwa Jini ni kiumbe asiyeonekana , asiye shetani wala pepo. Hutumika katika misemo mbali mbali kwa maana ya hadithi huonyesha fisadi au maovu. 

Swali linafuata tunaweza kuwaweka wachawi wanaotazamwa kama majini. Majini yanatumika katika maana ya uovu na ubaya. Hawapewi hadhi ya wema. Basi ukweli ni kwamba najini ni Mashetani au malaika wabaya.

HITIMISHO

Katika Afrika na hata mabara mengine duniani, watu wengi huyaogopa majini eti kwa sababu yanawakamata wanawake na watoto. Wafasiri wa Kurani ya Kiahmadiyya wanaeleza kwamba majini maana yake ni nyoka au wadudu. Lakini ni nyoka gani aliumbwa na Mungu kwa moto wa upepo wenye hari (Kur 15:28)?.
Ukweli ni kwamba watu wanaogopa sana wanaishi katika mashaka na hofu, wakichanganya mashetani, Majini na pepo  huku wakijikinga nao kwa hasara kubwa ya mali zao, wakidhani labda wanao uwezo mkubwa  na kwa kuwa ni wabaya waliandikiwa adhabu ya moto. Watu wanawaita “Bilisi” na kuwafanya mamoja na shetani mwenyewe.

Waafrika wengi wanaishi maisha ya taabu na jambo linalowakataza ni kuogopa hasa mambo mawili:
(A) Ajali (gadar) yaani kila kitu kimekwisha andikwa na Mungu, wala mwanadamu hana uwezo wowote wa kujiongoza mwenyewe katika mambo ya kawaida anaogopa kufanya lolote kinyume cha mapenzi ya Mungu wala hakusudii kufanya lolote bila kutanguliza neno la “in-sha allahu” Mungu akipenda.
(B)Viumbe wote wanaompita nguvu: waafrika tangu utoto wao wanaogopa kuanzisha chochote kinachoweza kuwakasirisha mizimu au pepo. 

Wanadhani kuwa wanao maadui marafiki wenye wivu kuliko marafiki wenye msaada. Jambo hilo ni uongo.
Basi kazi ya dini ni kuwafanya watu wawe huru na mambo kama hayo : na kama ndugu zetu waislamu wanadhani kuna faida ya kushikilia  maneno hayo ya ajali na pepo (au majini), bila shaka wanadanganyika  kuna mengi ya maana zaidi katika kurani ya kuwasaidia wenzetu kuishi maisha ya starehe.
Kushikilia  mambo kama hayo ni hatari kwa miaka ijayo: wataalamu wa siku zijazo wanaweza kuyadharau mambo hayo na pengine kuidharau dini yenyewe kabisa. 

Ni faida yetu sote, waislamu na wakristo, kushikilia hayo yaliyo kiini cha dini, yenye kumsaidia mtu kuishi vema kwa ajili ya maisha ya hapa na ahera. 

Wasaidizi wapo ndio malaika, maadui wapo, nao ndio mashetani, lakini yafaa nini tuongeze hesabu ya adui zetu, hali tunapunguza idadi ya marafiki zetu?





Post a Comment