Ads (728x90)

Powered by Blogger.



Wataalamu wa  Elimu ya falsafa juu ya mtu, Saikolojia na sayansi nyingine zinazoshughulikia binadamu hutuambia kuwa binadamu ni kiumbe aliye kwanza katika jamii (geneus) ya wanyama na katika biologia tunaita (animal kingdom). 

Lakini katika kundi tengefu (species) binadamu ana utashi na akili. Hii akili na utashi ni vipaji viwili vinavyotokana na roho yake.
Kutoka roho ambayo ina akili na utashi vinamfanya mwanadamu awe kiumbe pekee akitofautiana na viumbe kama vile wanyama, wadudu, mimea n.k.

Biblia inatuambia kuwa mwanadamu hutofautiana na viumbe  vilivyotajwa hapo juu hasa kwa sababu binadamu ameumbwa kwa mfano wa mwenyezi Mungu (Mwanzo 1;26-27), maana yake ni kwamba yupo katika hali ya kushirikiana na Mungu na kuwa na wajibu mbele ya Mungu.

Mwanadamu mzima akiwa mwenye roho na mwili, akiwa katika hali ya nafsi yake yote anaishi akiwa mfano wa Mungu.
Mungu alimweka Mtu awe mtawala wa dunia kuhusu vitu vilivyoumbwa (Mwa 1:27-28). Mungu alipomwumba mtu kwa mfano wake na  awe wa pekee miongoni mwa viumbe wengine (Zab 8:3-8, Mt 10:31, 12:12).

Mwanadamu si Mungu, anatakiwa aishi hapa duniani kama mfano wake tu! Mwanadamu asiishi mbali na Mungu, hata akiwa na dhambi bado aendelee kuwa mfano wa Mungu  (Mwa 9:6, I Kor 11:7, Yak 3:9) ni mfano wa Mungu ndani yake unaomfanya awe mwanadamu.

Habari za Adamu na Eva zinaonyesha sehemu ya heshima na madaraka ya mwanadamu
Mjumbe wake Mungu mwanadamu ana madaraka juu ya viumbe wengine walio chini yake (Mw 1:28-30, 2:15, 19-20). 

Mungu alimweka mwanadamu katika ulimwengu alipoweza kujiendeleza na kuzoeza akili na mwili kwa njia ya kufanya uamuzi wa hekima na kutumia akili zake kwa kufanya kitu cha maana.
Mungu alitaka afurahie maisha yake ya pekee kwa ukamilifu wake, lakini lazima  hivyo katika ushirika na utii kwa Mungu. 

Binadamu kutokana na kujaliwa kipaji cha akili kutoka kwa Mungu analazimika kukitumia kipaji hicho vizuri na hivi kutakatifuza malimwengu. 

Hata hivyo mwanadamu huyo haruhusiwi wala hana haki yoyote kutumia kipaji hicho  apendavyo wala kuwa mwamuzi mkuu wa mambo yaliyo mema au mabaya (Mwa 2:15-17)
Mkristo katika ulimwengu wa Uovu na jinsi ya kuepuka Dhambi
Katika Biblia neno ulimwengu linaweza kuhusika na ulimwengu ulioumbwa na Mungu au watu wanaoishi katika ulimwengu huu (Zab 90:2, 98:7, 9, Mt 25:34, yoh 3:16, Rum 10:18). 

Kwa sababu ya dhambi ulimwengu ulikuwa ni sehemu ambamo shetani anatawala katika maisha ya watu (Yoh 12:31, Rum 5:12, 2Kor 4:4, 1 Yoh 5:19). 

Katika hiyo Biblia mara nyingine husema juu ya jambo lililo na uovu au kinyume cha Mungu (Yoh 7:7, 17:25, yak 4:4, 1yoh 2:15). Ulimwengu katika maana hii ni jambo la wanadamu wenye dhambi pamoja na tabia mbaya zilizo alama za wanadamu wenye dhambi.
Ziko alama kuu zionyeshazo kuwa watu hawamwamini Mungu, ndizo Uchoyo na kiburi. 

Maisha ya watu hao yanatawaliwa kufuatana na mambo wanayotaka kuyapata na kuyatenda bila kumjali Mungu(1 yoh 2:16). Hii ni tabia ya kupenda mambo ya anasa ya dunia na Biblia inawaonya wakristo wasiwe nayo. 

Maisha ya mkristo yanatakiwa yatawaliwe na tabia inayomtegemea Mungu wala si mali na tamaa binafsi. Mtu akihangaikia kuhusu mambo haya daima huonyesha tabia ya watu wasioamini wala si tabia ya wakristo.

Majaribu ya tabia ya anasa ya dunia si lazima kuwa katika vita au mambo ya dhambi yanayoonekana wazi yaweza kuwa hata katika vitu vya kila siku visivyokuwa vya dhambi kama vile  chakula, kazi, mali na kujisumbua juu ya mambo yajayo. 

Mambo hayo yanaweza yakawa mabaya kama watu wana nia isiyo sawa juu ya mambo hayo (Taz Rum 1:25)
Mkristo anapaswa kuishi katika ulimwengu wenye uovu, lakini ajihadhari asije akashiriki dhambi ya ulimwengu. Mkristu yampasa kudumu katika uaminifu kwa kristo na kujihadhari asije akapotezwa na uovu wa ulimwengu. Kwa njia hii tu anayoweza kutimiza wajibu wake wa kuokoa uharibifu wa dhambi (Mt 5:13-16, Yoh 17:18, Yak 1:27)
Wakati huo huo mkristo ameitwa kuutakatifuza ulimwengu anapokaa kati ya watu na ana wajibu wa kueneza kazi ya Bwana anapofanya shughuli zake za kila siku kwa kuishi maisha mema, kukemea uovu na kuhimiza mapendo.

Maisha ya Mkristo ya kila siku katika kushuhudia imani na kutakatifuza ulimwengu
Mkristo anaangalishwa kuwa asitenge imani yake na matendo ya maisha yake ya kila siku. Ukisoma Barua ya mtume Paulo kwa Timoteo tunaambiwa hivi; “wanakiri kwamba wanamjua Mungu bali kwa matendo yao wanamkana” (Tim 1:16). 

Hapa tunafundishwa kuwa imani iliyo hai kwa mkristo ni ile inayoonekana katika maisha yote; kazini, nyumbani, safarini, likizoni na kwa ujumla katika uhusiano wake na watu wengine. 

Ndiyo sababu kuna msemo usemao: “maisha ya Mkristo ndiyo Injili ya Tano” hii ina maana kuwa labda wale wasiokuwa wakristo hawasomi Biblia, lakini husoma na kutazama maisha ya mkristo. Upendo ndiyo kiini cha maisha mapya ya mkristo.

Neno Mkristo raia (layman) linatokana na kiyunani “laos” my “taifa”. Maana kuu ya laos katika Agano Jipya ni “Taifa la Mungu” yaani wale wote wamwaminio Yesu Kristo na kumkiri kama mkombozi na Bwana. Katika lugha ya kiingereza “layman” hutumika pia kwa maana ya mtu wa taifa la Mungu.

Hata ingawa si Padre au Katekista anao wajibu wa kueneza kazi ya bwana iwezekanavyo kwa kutumia akili na hekima yake, pia busara kati ya watu kushuhudia mapendo ya Bwana “Wakristo raia” ni tawanyiko la Taifa la Mungu ulimwenguni humu. 

Kwa kweli wakristo hao wako popote katika viwanda na biashara, mashule, mashamba na kwenye vijiji. Mapadre na Makatekista hawana nafasi ya kutembelea sana.

Lakini wakristo raia kwa ajili ya kazi yao ya kila siku tayari wapo mahali pote. Wajibu wao wa kijamii upande wa ukristo wao ni kuonyesha upendo, kuishi na kutenda kikristo, kueneza habari njema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kukemea maovu, kuacha dhambi, kuwa mwanga na chumvi ya dunia (Taz mt 5:13-16) anatakiwa kutimiza wajibu serikalini n.k.

Njia nyingine ya mkristo kuutakatifuza ulimwengu na kumtukuza Mungu kwa kutumia akili
Licha ya kushiriki katika mafundisho ya Kanisa na kutekeleza, pia kutumia Vitabu, wataalamu Wakatoliki bado kuna njia ya kuyatakatifuza malimwengu nayo ni kuweka jitihada katika kutumia akili zetu kwa manufaa ya kanisa na kujiliwaza kwamba pengine kutotumia akili ni unyenyekevu.

Galileo Galilei alikuwa sahihi kutoamini kuwa Mungu aliyejalia kipawa cha akili alikusudua tusikitumie. 

Kutokutumia vema akili zetu ni kukiuka kanuni ya dhahabu tuliyopewa ambayo inatuhimiza kumpenda Mungu pamoja na mengine kwa akili zetu sote sisi ni wana wa nuru lakini kushindwa kutumia akili kunasababisha wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe kuwa na busara kuliko wana wa nuru (rej. Lk 16:86).

Bwana wetu Yesu Kristo hakutuamuru tuwe wapole kama njiwa tu, bali alitutaka tuwe na busara pia kama nyoka (rej. Math 10:16). Mara nyingi pengine msisitizo unawekwa zaidi kwenye sehemu ya upole kuliko busara.

Inawezekana ikaonekana kuwa ni rahisi zaidi kuishi bila kutumia akili kwa kuwa matumizi ya akili ni zoezi gumu ambalo wengi wetu tungelipenda kuepuka. 

“Mwanadamu atatumia kila aina ya ujanja ili kuepuka mzigo wa kufikiri” anasisitiza mgunduzi Thomas Edison. Suala la kukimbia matumizi ya akili limepelekea sisi wakristo kushiriki katika matendo mabaya ambayo hutuingiza katika dhambi na kuharibu utu wetu.

Ni aibu iliyoje katika karne ya sasa kuna wakatoliki bado wanaamini imani za kishirikina zisizoingia akilini na za uongo.  Mtume Paulo anaonja juu ya kutumia akili zetu kitoto bila kufikiri kwa utulivu unaowapasa watu wazima, anawaandikia Wakorintho; “Ndugu zangu msiwe watoto wachanga, bali katika akili zetu mkawe watu wazima” (1 Kor 14:26). 

Matumizi ya akili kwa usahihi ni jambo la lazima kama tunataka kuishi maisha yenye ufanisi na kuutakatifuza ulimwengu.
Mtakatifu Yohane Paulo wa II anaandika kuhusu Imani na Akili, mwanzoni kabisa mwa “Fide et Ratio” ni kama mbawa mbili ambazo kwazo roho ya mwanadamu huinuka katika tafakari ya ukweli. 

Baba Benedicto XVI katika kipindi chake cha upapa aliweka msisitizo na kipaumbele kuhusu matumizi ya akili katika maisha yetu ya kila siku ya kiimani.

Katika kitabu chake cha “Kwa nini Wakatoliki Hawakasiriki” (2008) Padre Titus Amigu anazungumzia matumizi ya akili kwa maisha ya mkatoliki. 

Katika sehemu mbali mbali za kitabu hicho au kwa kweli kwenye vitabu vyake vingine na majibu anayoyatoa kwenye vipindi mbali mbali vya redio, anarudia wazo hili mara kwa mara.

Kusoma vitabu vya falsafa ili kukomaza akili
Wanafalsafa waliotangulia si kwamba wao walikuwa na akili kukuzidi wewe, bali wao wameyatafakari mambo mbalimbali kiundani zaidi kabla yako. 

Unaweza kukuta mambo unayodhani wewe kuwa ni pointi au hoja za nguvu, kwa wanafalsafa ni marudio au walizijadili hoja hizo zamani na kuziona ni pumba tu! Au suala unaloona kwako ni gumu sana na lisilo na jibu kabisa, kwa wanafalsafa lilikuwa ni jambo la kawaida tu.

Ukisoma vitabu mbali mbali utajikuta una ujasiri wa akili na kujiamini katika mambo mengi, kwa kuwa akili yako itakuwa na wigo mpana wa kuhukumu mambo. Imani yako juu ya mambo kadha wa kadha yahusuyo jamii yetu itakuwa ni thabiti, hivyo unaweza kutoa mchango wako wa kueleweka katika jamii.

Daima inachokisema ndicho unachokimaanisha. Mazoea ya viungo kwa mwanajeshi ili kuufanya mwili wake kuwa imara, mazoea ya akili kwa mwanafalsafa ni kuifanya akili ikomae, ili kufanyika kwa njia ya kusikiliza mawazo kutoka kwa wengine, kusoma vitabu na kutafakari. 

Socrates, Plato, Hegel, Marx, Aristotle, na wengine waliofuata baadaye wote walisoma kwanza kazi za watu wengine.
Usipende kusoma magazeti ya udaku tu, michoro ya mtindo wa mavazi, michezo na burudani, haya yanavutia hisia zako na yanadidimiza upeo wa akili yako na kufikiria mambo ya maana ya kupiga vita umaskini.

Kusadiki katika kuongozwa na akili na si utashi
Binadamu anaongozwa na mambo mawili; utashi na akili, uamuzi wa kulipa kisasi hufanywa na utashi lakini uamuzi wa kusamehe hufanywa na akili. 

Utashi haupimi matokeo ya maamuzi yake, ndiyo maana mtu akifanya uovu huamua kwa uovu na hilo ni rahisi sana. Akikupiga mtu basi ni kumpiga, amekutukana mtu basi ni kumtukana, amekuchokoza mtu basi ni kuchukua bunduki na kumuulia mbali n.k. lakini kusamehe si hivyo.

Akili hupima na kuyatekeleza. Akili peke yake inaweza kutusaidia kupima mambo na matokeo yake na hivyo kuamua na kutenda kwa hekima na busara. 

Tukipatwa na tatizo binafsi tuongozwe na akili, tukitazame au kukisoma, tukisikilize na kukichambua vyema. Kama kitu  chenyewe hakieleweki vizuri tusisite kuwauliza wengine watufafanulie.

Yesu kila mara alipopatwa na matatizo  na changamoto nyingi bado hazikuzimisha akili yake, mara nyingi alijibu na kutenda kwa kutumia akili na wala hakutumia utashi na vionjo vyake vya kibinadamu. Hiyo hiyo nawe ndugu yangu usilipuke kulipa kisasi kwa jazba kana kwamba wewe ni wa kwanza kukosewa hapa duniani.




Post a Comment