Ads (728x90)

Powered by Blogger.




Nungunyane alipata matatizo dhidi ya serikali ya wareno ambao waliitawala nchi ya Msumbiji na alijiuzuru mwaka 1895.

Tukio hilo lilifunga uhuru na utawala wa Wabongoni katika nchi ya Thongaland wakati wa utawala wa Wareno ulipoenea Msumbiji yote. Machifu wote hao wa Kingoni katika nchi ya Thongaland kuanzia kizazi cha Zwide walifahamika kwa jina la ukoo la “Nyumayo” jina  jingine la Soshangane lilikuwa ni Manakuza. 

Uhusiano kati ya Wabathonga na Wangoni wa Tanganyika unaweza kutazamwa na kutambulikana kupitia majina ya kiukoo ambayo kwa asili hutokana na Wabathonga: Gomo, Makukula, Mathinya, Ngairo, Nguo, Nkuna, Ntani, Ntocheni, Silengi na Sisa.

Katika nchi ya Thongaland ukoo wa akina Nkuna walikuwa wanaishi kati ya mto Limpopo na Umkomazi, katika Tanganyika wahusika wa ukoo huu wanaishi sehemu iliyo karibu na misioni ya Namabengo. Jumbe Kangasimba na masultani wa sehemu hiyo walikuwa na majina ya ukoo walioitwa akina “Nkuna”.

Habari za Zwangendaba kuingia Afrika ya kati kutoka Thongaland

Kabila la Wangoni liliongozwa na viongozi mbalimbali tangu Thongaland. Lakini palikuwa na kiongozi aliyebobea katika masuala ya kivita na ufundi wa kutawala na kuongoza watu ambaye alifanikiwa kuingia Afrika ya Kati pamoja na watu wake bila matatizo, shujaa huyo wa Kingoni anafahamika kwa jina la Zwangendaba.

Jina hilo linajulikana sana kwa Wangoni waishio Afrika ya Kati pamoja na Wangoni wa Tanganyika. Inaelezwa kwamba Zwangendaba anatoka katika ukoo maalam unaojulikana kwa jina la Zwangedaba bin Magangata bin Magolera bin Lonyanda na bin Kali.

Asili ya jina hili la ukoo liitwalo Zwangendaba lilitokana na neno ‘Nkosi” au “Mfalme au “Tole”. Baadaye jina hilo liliachwa kutumika na badala yake likatumika jina la “Jere”. 

Hata hivyo tunasimuliwa  kuwa Zwangendaba  alimwoa binti ya binamu ya Zwide aliyeitwa “Loziwawa”. Kwa vile Loziwawa hakubahatika kumzalia Zwangendaba mtoto basi alipewa dada ya Loziwawa aliyeitwa “Sosera” awe mke wake.

Sosera alikuwa ni mama yake Mpenzani na huyo Sosera alitoka kijiji kilichoitwa “Emvuyeyeni”. Zwide na Sikunyene walipopigana na Tshaka, huyo Zwangendaba alikuwa jenerali katika majeshi yao. Baada ya Zwide na Sinyene kupepetwa na Tshaka kwenye vita, Zwangendaba aliwafuata  huko Thongland na kuishi nao.

 Lakini alipendelea kuishi na chifu aliyeitwa Soshangane ili kumsaidia kutoa msaada katika mambo ya kisiasa na kivita. Lakini baadaye ulitokea mgongano kati ya machifu wawili hapo Zwangendaba alimwacha Soshangane na nchi ya Thongaland; akiwa na kundi kubwa la watu aliamua kuelekea Afrika ya Kati.

Tukio la Zwangendaba na watu wake kuelekea Afrika ya Kati lilitokea mwaka 1828. Soshangane alipinga kitendo cha Zwangendaba cha kuihama nchi na baadaye  alichukua hatua ya kukusanya jeshi kubwa na kumfuata ili kumrudisha.
Lakini kitendo cha Soshangane cha kumrudisha Zwangendaba kiligonga mwamba  kwani jeshi la Zwangendaba lilikuwa imara na nguvu kama lake hali ileyopelekea jeshi lake kushindwa na kurudi nyuma.

Maisha ya Zwangendaba Afrika ya Kati

Wangoni wa aina ya Zwangendaba waliishi na kufanya makazi yao ya kwanza  Magharibi mwa Afrika ya Kati na baadaye walilekea Kaskazini. Katika kukaa na kuhamia huko Afrika ya kati Wangoni hao wa aina ya Zwangendaba hawakuwa na makazi ya kudumu huko Kaskazini, baada ya kukaa miaka michache takribani kama miaka 10 hivi  mpaka walipofika mto Zambezi. Watu wa Zwangendaba walitokana na kabila la Wandwandwe, wabathonga na Waswazi. Wangoni halisi katika Afrika ya Kati inasemekana kuwa ni wale waliotokea katika kabila la Waswazi.

Ingawa wengi kati ya watu hao hawakuwa wa kabila la Waswazi, ila kwa asili walitokana na kabila la Wandwandwe. Sababu za kuwa na idadi kubwa ya watu wa Zwangendaba ni kama ifuatavyo:

(a)Wandwandwe walitoroka kutoka kwa Tshaka labda walipita Mashariki ya nchi ya Swaziland kuelekea nchi ya Thongaland na kama ilitokea hivyo basi Waswazi wengi walijiunga na hao watu wa Zwangendaba.

Mwandishi anayeitwa Winterbottom aliandika kwamba Zwide baada ya kushindwa katika vita, Zwangendaba aliivamia Swaziland na hivi kuteka wanawake na mifugo kisha akaondoka navyo pmoja na vitu vingine walivyovikuta huko.

(b)Kusini mwa Swaziland kulitawaliwa na Zwide kabla ya kushindwa katika vita dhidi ya Tshaka na nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wake. 

Watu wa sehemu hiyo ya Swaziland walisababisha kitendo cha kupigana na Wandwandwe na hivi kupigania upande wao kuingia na pia kuhamia pamoja na Wandwandwe huko Thongaland labda hayo ni maelezo yanayoweza kutuhakikishia sababisho la kuwa na idadi kubwa ya watu kwa mtu aitwaye Zwangendaba.

(c)Inawezekana pia kuwa Zwangendaba, alipoiacha Thongaland alipopita Kaskazini ya Swaziland alichukua idadi kubwa ya watu na kuondoka nao.

Kadiri ya Cullen Young na Wenterbottom, watu wa Zwangendaba walipotoka Thongaland kwanza walijiunga na Wamatebele na kuishi nao kwa muda fulani. Baadaye ulitokea uhasama kati ya makabila hayo mawili. 

Mwanzoni Zwangendaba alimshinda Chikuse Maseko  (Jenerali Msilikazi), lakini akitambua kwamba jeshi lake lilikuwa nyonge ukilinganisha na jeshi la Msilikazi, aliona ni afadhali kuiacha nchi ya Wamatebele na kuelekea Kaskazini Mashariki.
 Inasimuliwa kuwa Wangoni hao walipoiacha Thongaland mababu zao kwanza walivamia nchi ya Wanyame na kuiteka na kuwachukua baadhi ya wakazi wa nchi hiyo.

Ukoo wa Nanguru wanaoishi  kwenye Baraza la Mkurumuzi karibu na missioni ya Mpitimbi huku Tanganyika hupata asili yake hutoka kabila la Wanyame. Nduna Zawayayi bin Kapungu bin Chikuse ni wa ukoo huu. Na babu wa huyu Nduna alikuwa na jina aina hiyo hiyo kama ilivyoonyeshwa kwa Msilikazi hapo juu.

Watu wa Zwangendaba walioiacha nchi ya Wamatebele waliiita nchi hiyo “Halale” na inaeleweka kama Nyanda za juu yenye hali ya baridi (Cf Winterbottone) Jina Halale bado linatumika na Wangoni wa Tanganyika kuitambulisha Rhodesia ya Kusini. (Na mji mkuu wa zamani ulioitwa Salisbury kwa sasa ni Harare toka uhuru)



Post a Comment