Ads (728x90)

Powered by Blogger.


Na Albano Midelo
Pori la Akiba la  wanyamapori la Liparamba linapita katika  wilaya za Songea, Mbinga na Nyasa mkoani Ruvuma; limejaaliwa kuwa na vivutio ambavyo havipatikani katika hifadhi nyingine nchini.

Liparamba ni hifadhi iliyopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ambapo wanyama wake pia huwa wanavuka hadi hifadhi ya Niassa nchini jirani ya Msumbiji kisha kurudi Tanzania kupitia pori la Liparamba hadi Pori la Akiba la Selous.

Meneja wa Pori hilo Richard Bwire anasema pori la Akiba la Liparamba lipo katika ukanda wa misitu maarufu duniani ya miombo (woodland) inayokadiriwa kuwa na tembo zaidi ya 60,000 kulingana na utafiti ambao ulifanywa mwaka 2011 na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii za mwaka 2003 zinaonesha kuwa idadi ya tembo nchini iliongezeka na kufikia 120,000 ambapo nusu ya tembo hao walitoka katika pori la Akiba la Selous ambapo Liparamba ni ushoroba wa tembo toka Selous ambao wanavuka hadi nchini Msumbiji.

Hata hivyo sensa ya Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) ya mwaka 2009 ilionesha idadi ya tembo nchini ilikuwa 109,051 ambapo kutokana na kukithiri kwa ujangili mwaka 2014 idadi ya tembo ilishuka hadi kufikia 43,330 sawa na asilimia 60 ya tembo wote.

Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Africanus Challe anasema pembe za tembo wa Liparamba zimebainika kuwa na uzito wa kilo karibu 140 kwa pembe moja ,wakati katika hali ya kawaida pembe za tembo zina uzito wa kilo 100 kwa kila moja. Tembo anakadiriwa kuwa na kilo 7000 sawa na tani saba.

Kwa mujibu wa Mhifadhi huyo, tembo anaweza kuishi kati ya miaka 60 hadi 70, tembo jike hubeba mimba kwa miaka miwili, tembo mtoto huzaliwa na kilo kati ya 80 hadi 120, chakula cha tembo kwa siku ni kilo 300 na maji kwa siku tembo anakunywa lita 40.

“Ni mara chache sana hapa duniani kuwepo kwa hifadhi moja ya wanyamapori ambayo inatumika na nchi mbili tofauti. Tanzania tuna bahati kwa kuwa kuna na hifadhi ya wanyamapori ya Liparamba  inayotumiwa na wanyama upande wa Tanzania na nchi jirani ya Msumbiji’’, anasema.

Meneja wa Pori hilo Richard Bwire anabainisha kuwa pori hilo lilikabidhiwa rasmi Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya usimamizi wa Idara ya Wanyamapori serikani Juni 5 mwaka 2006 ambapo pori hilo lina ukubwa wa kilometa za mraba 571 likiwa na eneo la kilometa za mraba 11,396.

Anasema ukubwa wa misitu mizito minene iliyopo katika pori hilo inachangia kupunguza hewa ukaa(CO2) na kwamba pori hilo ni eneo muhimu katika mchakato wa (Carbon sink) ambao hupokea mvua za kutosha kwa msimu mmoja tu kwa mwaka.

Bwire anabainisha zaidi kuwa pori hilo lina mito mikubwa miwili ambayo ni mto Lunyere na mto Lumeme ambayo inamwaga maji yake katika mto Ruvuma unaomwaga maji yake Bahari ya Hindi na kwamba pori lipo katika ukanda wa madini  hivyo pori linaangaliwa dhidi ya uvamizi wa uchimbaji madini. 

“Miongoni mwa vivutio adimu ni uoto wa asili ya jamii ya miombo zikiwemo aina 60 za miombo, nyasi adimu aina 35, aina 80 za ndege na wanyama wa aina mbalimbali wakiwemo tembo, simba,  chui, parahali, tandala, pundamilia, nyati, kuro, pofu, kima, mamba, kiboko, ngiri na wanyama wengine’’, alisema Bwire.

Kwa mujibu wa Mhifadhi huyo, pori hilo lina uoto wa asili ambao haujaharibiwa katika ukanda wa wilaya za Mbinga na Nyasa na kwamba pori hilo linatoa matunzo ya tembo wanaohamia kutoka Msumbiji na kuja Tanzania na kurudi Msumbiji na kwamba utafiti umebaini wanyama wengine wakifika Tanzania hawarudi Msumbiji.

Anazitaja shughuli za uhifadhi ambazo zimefanywa katika kipindi cha Julai 2016 hadi Agosti 2017 kuwa ni doria za kawaida ndani ya pori, kazi za intellijensia, usuluhisho wa migogoro ya mipaka, kutoa elimu ya uhifadhi kwa umma na kupandisha hadhi mapori tarajiwa ya Gesimasowa na Litumbandyosi.

Shughuli nyingine ni zoezi la uwekaji wa alama za kudumu kwenye mipaka ya hifadhi, doria maalum ya kupambana na kilimo cha bangi hifadhini, kuhamisha wavamizi kwenye ushoroba wa pori la Selous na Gesimasowa, doria ya kudhibiti wanyama waharibifu na kikao cha ujirani mwema kati ya mikoa ya Ruvuma na Mtwara upande wa Tanzania na mikoa ya Niassa na Cabodelfado nchini Msumbiji.

Hata hivyo Bwire alitaja pendekezo la kuhifadhi pori la Akiba Liparamba lilitokana na utafiti uliofanywa na Idara ya Maliasili wilayani Mbinga katika miaka ya 1980 hadi 1982 ambapo mambo kadhaa yaligundulika. 

Mambo hayo ni upungufu mkubwa wa eneo la misitu kutokana na kilimo cha kuhamahama na kilimo cha mazao ya msimu kilichoendeshwa na wakulima toka eneo la milimani kwenda katika ukanda wa chini kulima mahindi kwa ajili ya chakula. 

Mambo mengine ni upungufu wa maeneo yaliohifadhiwa kwa ajili ya kulinda miti muhimu na yenye thamani kubwa kama mininga, mahogani na kupotea kwa mimea ya asili ambayo ilihitajika na kuendelea kuhitajika kwa ajili ya chakula, dawa na ulinzi wa viumbe asilia. 

Hata hivyo Meneja Mwanzilishi wa mradi wa pori la Akiba la  wanyama Liparamba, Hashim Sariko anasema kutoweka na kupotea kabisa kwa wanyamapori na wadudu asilia ambao miaka ya nyuma waliishi katika misitu  ndiko kuliisukuma  Halmashauri ya wilaya hiyo kuamua kuwa na maeneo ya misitu ya kutosha kama misitu ya akiba. 

Sariko anabainisha zaidi kuwa maeneo hayo yalizuiliwa kwa kulinda misitu, miti, wanyama, wadudu na viumbe wasiharibiwe kwa kuwa na maeneo ya vivutio vya asili kwa lengo la kuwawezesha wananchi kutembelea, kuona na kujifunza historia na sayansi ya viumbehai katika vivutio vya utalii,  makazi ya wanyamapori na hifadhi ya maji na mazingira. 

Afisa Maliasili wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe alisema kuwa pori hilo lina kiwango cha juu cha hifadhi ambacho kinatiliwa mkazo kisheria katika ulinzi, usimamizi, uendelezaji na matumizi ya malihai ikiwemo misitu, samaki na wanyamapori hivyo kuhifadhiwa  kumejumuisha sekta nzima ya maendeleo ya mazingira,m aliasili na utalii kwa gharama nafuu. 

“Hili eneo ni la kipekee katika ukanda wa juu wa misitu ya miombo, lipo karibu na ziwa Nyasa, wengi watavutiwa na eneo hili kuona msitu mzuri wa asili usioharibiwa sanjari na wanyama adimu wakiwemo chui, simba, palahala na tandala wakubwa”, anasema. 

Anasema pori la Liparamba ni kielelezo cha ukanda wa viumbehai katika mazingira yao ya asili ambapo anayataja malengo mengine ambayo yamesababisha serikali kuweka pori la akiba la Liparamba kuwa ni kulinda vyanzo vya maji na milima ya kuvutia. 

Pori la Liparamba linapakana na vijiji saba ambavyo ni Liparamba, Ndondo, Mipotopoto, Mitomoni, Mseto, Mtua na Mpepai na kwamba wakazi wa vijiji hivyo baadhi yao wanafanya ujangili kwa ajili ya kupata kitoweo hali inayosababisha askari wa wanyamapori kufanya doria siku 20 kila mwezi.
 Albano.midelo@gmail.com, simu 0784765917


Post a Comment