Utangulizi
Kutokana na ufunuo wa kimungu twafahamu na kujua kwamba mtu yupo duniani ili amjue Mungu, ampende, amtumike
na halafu afike mbinguni. Haya ndio madhumuni ya kweli na thabiti ya uwepo wa
mtu, binadamu na historia.
Ni jambo la kusikitisha sana kuona
kwamba kuna watu wengi ambao hawajitambui hata kidogo, kwa nini wapo hapa
duniani. Watu hao wapo pia kwenye kundi la Wakatoliki. Sasa hivi sisi binadamu
tunaishi katika utamaduni ambao kwa kiasi kikubwa umeegemea zaidi katika mambo
ya kidunia.
Kuna mamilioni mengi ya watu walio
ndugu zetu na jamaa zetu na wanaomsadiki Mungu na wangependa kuona malimwengu yasiwe na nafasi kumtawala
binadamu, lakini sauti yao haina nguvu wala haisikiki katika utamaduni wa kawaida.
Mkazo mkubwa karibu hata nguvu zote
katika vyombo vya habari…. Radio, Tv (Runinga) n.k…… hivyo vyote vipo katika
dunia hii. Ndio maana mkazo mkubwa unaelekezwa katika masuala ya kifedha,
ngono, heshima, siasa, nguvu na uwezo wa kiserikali.
Watu wengi wanaona kumcha Mungu ni
suala lililopitwa na wakati, linawapotezea muda wao na pengine huwacheleweshea
maendeleo yao. Ebu tujifunze kwa
waisraeli ambao waligundua kwamba uchaji wa Mungu ni mwanzo wa Hekima.
Taifa la
Israeli na utafutaji wa Hekima ya kweli
(a)Waisraeli na vitabu vyao vya
Hekima
Waisraeli ni kati ya mataifa makubwa
katika historia ya ulimwengu, walikuwa na “hekima” yao, kwa mujibu wa maelezo
yaliyopo tukiruhusiwa kutamka vile ambavyo inaelezwa katika vitabu vitano vya
Agano la Kale katika Biblia.
Kwa hiyo vitabu hivi vinaitwa “Vitabu
vya Hekima” navyo ni Ayubu, Mithali, Mhubiri, Yoshua bin sira na Hekima ya
Sulemani.
(b) Waisraeli Waliamini
Waisraeli waliamini kuwa hekima ya
kweli ni ile ambayo mtu anaweza kuitumia hasa katika maisha ya kila siku. Pamoja
na Wamisri wa zama hizo, wao waliona kuwa mtu mwenye hekima ni yule anayeweza
kutekeleza maisha yake, siku kwa siku pamoja na taabu na matatizo yake kwa
ustadi pasipo kumuudhi mwingine. Tena tukikaza waliamini kuwa hekima ni ile
inayoweza kutumika na wala si kuijua tu katika nadhiri mbalimbali.
Basi, tukisoma vitabu hivi, tunaona
maonyo mbalimbali ambayo kwa lugha ya
leo tungeliweza kuyaita kama mwongozo. Mwongozo huo unahusu maisha ya kila
siku, ili mtu akifuata, aweze kutekeleza maisha yake ya kila siku pamoja na
matatizo yake kwa ustadi au ufundi unaotakiwa.
(c)Mambo madogo madogo
Maonyo yaliyoandikwa katika mfumo huo
yanahusu mambo ya kila siku, na mara nyingi mambo madogo madogo. Labda msomaji
unaweza kuuliza: kwa nini kutoa mwongozo au maonyo katika mambo madogo madogo
ya kila siku? Waisraeli walitambua kuwa matendo hayo madogo madogo ya kila siku
ndiyo yanayofanya maisha ya watu wengi.
Wao walijua, ijapo sisi siku hizi
tunasahau kuwa maisha ya binadamu
yanajengwa na kuundwa na matendo ya kila siku kama vile kutembea, kuongea na
watu wa aina mbalimbali, uhusiano na watu wa aina mbalimbali, shughuli za
nyumbani na hata sokoni; kifupi
tungelisema wajibu wa kila siku hata ukiwa mdogo kiasi gani.
Kwani ni dhahiri kwamba matendo
makubwa au ya kishujaa si sehemu ya maisha ya kawaida kwa watu wengi.
Aidha tusisahau kuwa hata katika
mambo madogo madogo mtu anaweza kukosa raha na amani moyoni iwapo mambo
yanamwendea mrama.
Labda wasomaji wa Biblia wamecheka au
walau kutabasamu mara nyingi waliposoma sentensi nyingi katika vitabu hivi vya
hekima, kwani vyaeleza mambo ambayo mara nyingi watu hawajali katika maisha kwa
mfano twasoma:
“Midomo ya malaya hudondoza asali, na
kinywa chake ni laini kuliko mafuta” Mithali 5:3 au mtu anayezungumza pamoja na
mpumbavu amefanana na yeye anayezungumza
na mwenye kusinzia mwishowe atasema, Nini?”. Yoshua bin Sira 22:10.
Hata tukitabasamu tusomapo sentensi
kama hizo, yatupasa tukumbuke kuwa yote yaliyoandikwa katika Biblia yameandikwa
ili kutufundisha sisi, hata kizazi chetu cha leo. Na mtume Paulo alikazia jambo
hili alipowaandikia wakristo wa Korintho (Taz. 1Kor. 10: 1-11).
(d) Msingi wake
Lakini mtu atapata wapi nguvu ya
kuweza kutekeleza maisha yake kwa ustadi huo unaotakiwa? Tena msomaji utauliza
jambo hili linawezekanaje kwetu ambao tuna matatizo mengi na pengine ni tofauti
kabisa na yao?.
Vitabu vya Hekima vyatutatulia tatizo
hilo. Kwa vile hekima ya kweli ni kuweza kutekeleza maisha ya kila siku pamoja
na matatizo yake, kiini cha kuweza kutekeleza maisha yake ya kila siku huyu ana
hekima.
Yeyote asiyeishi kadiri ya matakwa au
sheria za Mungu, hawezi kuwa na hekima hiyo kwani wao waliamini kwa dhati kuwa
kumcha Mungu ni chanzo na msingi wa kupata hekima.
Kwa sababu hiyo waliandika: “kumcha
Mungu (Bwana) ndio mwanzo wa hekima, wote wafanyao hayo wana akili njema” (Zab
111:100 au wazi zaidi: “Hekima yote ni kumcha Bwana (Yoshua bin Sira 19:20).
(e) Walipitia Taabu
Tuulize walipataje kuamini jambo
hili? Sote twajua kuwa Waisraeli walikuwa taifa teule la Mungu. Hata hivi Mungu
aliwapeleka utumwani Babeli wakatawaliwa na kuwatumikia watu wasiomjua Mungu wa
kweli “washenzi”.
Baada ya kuwa watumwa huko Babeli na
kupata taabu nyingi, waisraeli waliamini jambo hili kikamilifu. Kwani, baadaye
walijua ni kwa nini Mungu aliwapeleka utumwani kuwa chini ya wapagani yaani
“washenzi” ndivyo walivyowaita wote
wasiokuwa wayahudi.
Walipelekwa utumwani kwa sababu za
kumwasi Mungu, na hivi Mungu hakuwahurumia eti kwa kuwa ni taifa lake tukufu kama wenyewe walivyotumaini.
Kutokana na taabu hizo baadaye waliamini sana kuwa kumcha Mungu
ndiyo hatua ya kwanza kabisa ya kujipatia hekima ya kweli.
Huko kumcha Mungu sharti kuwepo
daima, katika kila jambo analolifanya mtu.
Hata katika kujenga nchi, katika
maendeleo sharti kumjali Mungu. Kazi za kila siku na juhudi za mwanadamu sharti
zipate baraka na uongozi wa mwenyezi Mungu, vingine ni bure.
Bwana asipojenga nyumba, waijengao
wafanya kazi bure, Bwana asipoulinda mji, yeye aulindaye akesha bure (Zab
127:1) ndivyo walivyoimba na kusali watu walioitwa Waisraeli.
(e) Kinyume chake Je?
Iwapo kumcha Mungu, kutenda na kuishi
kadiri anavyotaka Mwenyezi Mungu ni kiini cha kupata hekima, kutomcha Mungu ni
nini? Waisraeli walimwona mtu asiyemjali Mungu ni Mpumbavu au mjinga (Taz Zab.
14 na 53).
Ujinga au upumbavu huo unafikia
kilele chake pale mtu huyu anapotenda uovu fulani au dhambi. Mtu asiyemjali
Mwenyezi Mungu akatekeleza maisha yake kama anavyotaka mwenyewe tu huyu hana
hekima, hata kama angelionekana machoni pa wengine kuwa ana akili nzuri. Maana
kumcha Mungu ni Mwanzo wa Hekima.
Tena kazi ya mtu wa namna hii, hata
kama zingalionekana kuwa vema, mwishoni zitaangamia tu, kwani kazi hizi
zitapata wapi baraka ya Mungu iwapo huyu mtu hamjali Mwenyezi Mungu?.
(g) Leo Je?
Tungeliweza kuendelea kuitazama
hekima hii ya kweli ambayo Waisraeli waliiamini. Hekima hiyo ndiyo inayotakiwa
wakristo tuizingatie na kutoa mwanga kwa
wengine wasioijua bado.
Kwani mtu akiwa na fikira au mawazo
kuwa dini ni kasumba na kusema eti dini inazuia maendeleo ni vigumu kuamini
kuwa anajua maana halisi ya dini.
Tena, wakristo tunaamini kuwa
Biblia ni neno la Mungu na ndivyo
ilivyo. Kumbe, Biblia hutufundisha hekima ya kweli ni nini kwa hiyo si waisraeli wanaotufundisha wao
waamini, bali ni Mungu mwenyewe atufundishaye jambo hili.
Tukitaka kufanikiwa katika shughuli
zetu sharti la kwanza si juhudi zetu, bali kutenda kama anavyotaka Mungu na
kumwomba baraka kwa kazi.
Maana utaalam pasipo baraka za Mungu
hautoshi. Hata siku hizi, twaweza kufundishwa mengi, mradi tu tukifungua Biblia
na kusoma walau kidogokidogo.
Binadamu na utafutaji wa hekima ya
Mungu
(a)Mtu wa leo huitwa “Mtu Mwenye
Hekima”
Wataalamu wa Sayansi ya Anthropolojia
ya kimwili (Physical Anthropology) Sayansi ambayo huchunguza habari za uhai wa
mtu, historia yake katika mageuzi yenye kuendelea (evalution) uhusiano wake na
viumbe wengine walio karibu naye n.k.
Hutuambia kwamba mtu, jinsi alivyo
sasa, hakutokea duniani ghafla bali ana historia ndefu. Amebadilika polepole
kwa njia ya mageuzi yenye kuendelea na kupata hali yake na umbo lake la leo
(Theory of Evolution).
Mtu wa sasa huitwa kwa kilatini “Homo
Sapiens” yaani “Mtu Mwenye hekima”. babu yake wa kwanza ajulikanaye kwa sasa
“Homo Habilis” maana yake “Mtu mwenye kuweza” mabaki yake yamepatikana huko
Olduvai Gorge Tanzania ambapo aliishi kama miaka 1, 250, 000 – 1, 750, 000 hata
pengine na zaidi iliyopita.
Mtu huyo aliye babu alijua kutumia
vifaa, fulani kama kisu kilichotengenezwa kwa jiwe hivyo wataalam wakampa jina
hilo la mtu “Mwenye kuweza”.
“Mtu wa sasa kama tulivyosikia huitwa
Mtu mwenye hekima yaani wewe na mimi basi mtu aliye mkristo awe makini
zaidi kwa vile anatazamwa kuwa ni mwenye hekima ili amche Mungu vizuri.
(b)Maana ya neno Hekima
Kama tumefuatilia maelezo ya neno
“hekima” kama Waisraeli walivyoelewa hapo juu na pia wataalam wa elimu ya
Anthropology wanavyodiriki kumwita mtu
wa leo kwa jina la “Homo sapiens yaani” mtu mwenye Hekima.
Basi kadiri ya matumizi ya neno
hekima katika Biblia hali kadhalika katika matumizi yake nje ya Biblia hali
“Hekima” ni elimu au mbinu zinazomwezesha mtu kuyamudu maisha yake ya kila
siku.
Hata
ufundi wa msanii huitwa “Hekima” pia (Kutoka 31:1-5) hali kadhalika uwezo wa
kutawala vizuri ni hekima, kama hekima aliyojaliwa Solomoni (1 Wafalme 3:1-15).
Hekima ni Elimu inayomsaidia mtu
kutafuta majibu kwa matatizo ya kila siku kwa mfano Mbinu za kuhusiana vizuri
na watu wa matabaka mbalimbali hizo zinapatikanaje? Mang’amuzi ya maisha humpa
mtu mbinu hizo.
Wale waliopata mang’amuzi ya maisha
hurithisha elimu kama hiyo inapatikana katika jamii zetu za wanadamu ispokuwa
siyo jamii zote za wanadamu zimewahi kuaandika elimu hiyo. Katika jamii
zisizokuwa na maandishi hekima hizo zimo katika methali na vitendawili.
(c)Hata maana ya neno Falsafa
limetokana na neno hekima
Falsafa (Philosophy) ni neno
litokanalo na maneno mawili ya Kigiriki yenye maana ya Upendo na Hekima kwa
hilo neno falsafa linamaanisha upendaji
wa hekima katika mambo yote na kushirikiana na ukweli huo. Falsafa huanza kwa njia ya mshangao yaani Falsafa
hukiona kile kitu kionekanacho cha kawaida
kama ni cha kushangaza na kitu cha kushangaza, kwetu sisi falsafa
hukiona ni cha kawaida tu.
Falsafa inakufanya uwe huru kifikra
na kujitegemea kimawazo na kimaoni.
Binadamu asiyekuwa na falsafa yoyote
humfanya aonekane hana faida katika jamii. Falsafa humsaidia mtu kushinda ndoto
zake za mambo fulani. Ni kweli kuwa jinsi kila mmoja anavyofikiria hutegemea
jamii, elimu, mazingira utamaduni, dini, uchumi, tabia na siasa inayomzunguka,
lakini falsafa inamsaidia mtu kwenda juu
zaidi ya haya yote.
Falsafa inashughulika na mambo makuu
matatu yaani Mungu, binadamu na dunia. Falsafa humsaidia mtu kuwasilisha mawazo
yake katika mtiririko wa mawazo mantiki unaoeleweka kwa wenzake.
Falsafa ni Elimu inayojihusisha na
ukweli kama ulivyo. Na kwa sababu hii elimu inajihusisha zaidi na masuala ya
msingi ya kila kitu na kanuni ya uwepo.
(d)Hekima inayofaa ni ile
inayomheshimu Mungu
Ni mapenzi ya Mungu kwamba wanadamu
wajifunze na kukuza hekima ya maisha, ili waweze kuishi kwa maarifa ya kweli.
Kwa njia hii maisha yao yanafaa, yakimfurahisha Mungu na kunufaisha maisha yao
na yale ya watu wengine (Mit 1:2-7,
2:7-11, Efe 5:15-16). Hekima inayofaa ni ile inayomheshimu Mungu.
Hekima inayopendekezwa katika Biblia
inahusika zaidi na mambo yanayosaidia maisha ya kila siku kuliko mawazo ya
Falsafa (Philosophy) tu watu wanaishi katika ulimwengu wenye matatizo,
wanapaswa kuishi na watu wenye matatizo (Kumb 1:13-15, 34:9, 1Fal 3:9, Mdo
6:3,7:10) lakini msingi wa hekima ile si ujanja wa binadamu, bali ni utii na
heshima kwa Mungu.
Mungu ni asili ya hekima ya kweli,
naye anawapa watu wale wanaoitafuta (Mit
1:7, 2:6, 9:10, Dan 2:20 Rum 16:27, 1Kor 1:30, Yak 1:5-8).
Bila heshima ile, hekima inaweza kuwa
ya ubinafsi au ya kidunia, inayoonekana katika udanganyifu. Hekima isiyomjali
Mungu ni kama vile tabia ya wivu na udanganyifu. Kinyume chake hekima itokayo kwa Mungu alama
yake ni unyenyekevu, unyofu na hamu ya kusaidia watu (Mit 8:12-16, 10:8, 11:2,
Isa 5:21, Yakobo 3:13-18).
Hekima hii itokayo kwa Mungu
inapatikana kama watu wako tayari kuacha ujinga wa njia zao za ubinafsi na
kuipokea kutoka kwa Mungu (Mit 1:20-23, 8:1-6, 9:1-6) inawataka watu washinde
majaribu ya maisha (Mit 6:23-27) lakini wakiikataa watajipatia aibu na hali ya
kukatisha tamaa (Mit 1:20, 24-26, 5:11-13, 7:1-23, Mhu 10:1-3).
Post a Comment