-Marejea yanazalisha
magunia 68 kwa hekta moja
-Baba wa Taifa
alikuwa ni mfuasi mkubwa wa marejea
Na
Albano Midelo
Kilimo ni Mwajiri Mkuu wa watanzania
kutokana na takwimu kuonesha kuwa asilimia zaidi ya 75 ya watanzania
wamejiajiri katika sekta ya kilimo.
Sekta ya kilimo nchini inakabiliwa na
changamoto nyingi zikiwemo ya wakulima wengi kuendelea kutumia jembe la mkono,bei
ya kubwa ya pembejeo na ukosefu wa soko
la uhakika la mazao.
Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwa
tatizo la kutegemea mbolea za viwandani linaweza kumalizika au kupungua iwapo
kitafufuliwa kituo cha mradi wa mbolea ya kilimo mseto (marejea) kilichopo Peramiho
Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoa wa Ruvuma.
Kituo cha MRUMA Peramiho ndiyo Kituo
pekee katika nchi nzima ambacho kilikuwa
kinazalisha mbegu za mbolea ya marejea kilichokuwa chini ya Kanisa Katoliki
Abasia ya Peramiho ambacho kimekufa tangu mwaka 2013.
Hivi sasa majengo Kituo hicho
yanatumiwa kama hosteli ya kulala wanachuo wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Madaktari
cha Bugando tawi la Peramiho.
Historia inaonesha kuwa kilimo mseto
kwa kutumia mradi wa kurutubisha ardhi kwa kutumia mbolea ya marejea kituo cha
MRUMA Peramiho kilianza tangu 1942.
Mwanzilishi wa mbolea ya marejea ni
padre Otmar na Bruda Krisp OSB ambaye aliyaokota marejea kutoka porini na
kuhamasisha watu kutumia kama mbolea mbadala.
Mwaka 1963 bruda Herman OSB wa kituo hicho alianza kutumia mbolea ya marejea na kulishia
mifugo ambapo mwaka 1983 ilianzishwa benki ya mbegu za marejea Peramiho
(sunnhemp seed bank).
Mwaka 1987 baada ya kuona umuhimu wa marejea katika
kurutubisha ardhi kilianzishwa rasmi kituo cha mradi wa kurutubisha udongo kwa kutumia marejea Peramiho (MRUMA) kituo ambacho kilikuwa kinatoa
elimu ya kutumia mbolea ya marejea kwa wakulima katika nchi nzima.
Gabriel Mhagama aliyekuwa Mkuu wa Kituo
cha MRUMA hadi kinakufa mwaka 2013 anasema kuna mimea mingi ambayo ina uwezo wa
kuongeza rutuba katika udongo ikiwemo mimea jamii ya kunde.
Mhagama anasema alikabidhiwa kuwa Mkuu
wa Kituo hicho tangu mwaka 1991 kutoka kwa muasisi wa Kituo hicho hayati Padre
Gerald ambaye alifariki dunia mwaka 2000 ambapo hivi sasa wataalam wengi wa
masomo ya kilimo kutoka ndani na nje ya nchi wamekuwa wakifika katika Kituo
hicho kufanya utafiti na kutunukiwa shahada za kwanza,shahada ya
uzamili(masters) pili na wengine wametunukiwa shahada ya uzamivu (PHD).
Hata Mhagama anasema utafiti
uliofanywa katika Kituo cha MRUMA tangu mwaka 1942 umebaini kuwa mimea ya
porini aina marejea inachukua nafasi ya kwanza kwa kurutubisha ardhi na mkulima
akitumia mbolea hiyo ana uwezo wa kuzalisha mazao mara dufu zaidi ya kutumia
mbolea za viwandani.
Utafiti uliofanywa na kituo cha kilimo
Uyole kuhusu mbolea ya marejea ulibaini kuwa shamba la hekta moja lililolimwa marejea mwaka uliotangulia
linaweza kutoa magunia 68 ya mahindi
yenye uzito wa kilo 100 badala ya magunia 14 tu iwapo haujatumia marejea.
Anasema baada ya kupandwa na kuota ni
lazima kufyeka marejea baada ya wiki mbili hadi
mwezi mmoja na kuyageuza kwa kuchanganywa na udongo ili yaoze iwapo
unataka kulima mazao katika shamba hilo ndani ya mwaka huo.
“Iwapo unataka shamba lililopandwa
marejea, kulima mwaka unaofuata unatakiwa kuyaacha marejea yakue hadi yatoe
mbegu’’,anasisitiza Mhagama.
Utafiti umebaini kuwa mbolea ya
marejea ndiyo majibu ya mkulima ambaye hawezi kumudu kununua mbolea ya
viwandani kwa kuwa mbolea hiyo
hurutubisha na kudumisha rutuba ardhini.
“Siku zote tunawambia watu kwanini
wanang’ang’ania kulima mazao kwa kutumia mbolea za chumvi chumvi wakati
zinawaumiza na kuua ardhi,badala ya kuchukua mbolea ya marejea ambayo hayana
gharama”, anasisitiza Mhagama.
Kulingana na mtaalam huyo mbolea ya marejea husaidia wiki mbili hadi
mwezi mmoja baada ya kufyeka shamba
ambapo mkulima anatakiwa kupanda marejea kilo 20 kwa ekari na kutumia
mfumo wa kubadilisha mazao yaani crop rotation ili kupata mafanikio wakati wa
kutumia mbolea ya marejea.
Uchunguzi umebaini kuwa miaka ya 1983
mbolea ya marejea ilianza kutumiwa na wakulima wengi katika sehemu mbalimbali
nchini ambapo wakulima na vikundi vya wakulima walifika katika Kituo cha MRUMA
Peramiho kujifunza kuhusu uzalishaji wa mbolea hiyo hali ambayo ilisababisha maelfu ya tani za
mbegu za marejea kununuliwa na kwenda kuzalishwa.
Aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha MRUMA
Gabriel Mhagama anasema miaka ya 1980,Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius
Nyerere alitembelea kituo hicho na kufurahishwa na uzalishaji wa mbolea hiyo
hali iliyosababisha baba wa Taifa kununua tani za mbegu za marejea na kununua
vitabu mbalimbali vinavyotoa elimu ya mbolea ya marejea.
“Padre Gerodi masisi wa marejea na
hayati Baba wa Taifa walikuwa ni wafuasi wakubwa wa mbolea ya marejea ambapo
mama Maria Nyerere bado anaendelea kutumia mbolea ya marejea, mwaka 2012 alinunua
tani mbili za marejea ambazo tulimpelekea
nyumbani kwake Butihama”, anasisitiza Mhagama.
Mhagama anasema kuwa marejea kutoka Peramiho
yameenea karibu nusu ya Bara la Afrika na mengine yamepelekwa hadi katika Bara
la Ulaya ikiwemo nchi ya Uswis ambapo nchi hizo zinatumia vitabu vya mafunzo ya
mbolea hiyo na kufanya kilimo hicho kuwa endelevu.
“jambo la kusikitisha ukiachia
aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Mstaafu wa Ruvuma hayati Dk.Lawrence Gama, baba wa Taifa
na Mke wake mama Maria Nyerere ambao wametembelea kituo chetu,hadi kituo kinakufa
mwaka 2013 hakuna watalaam wa ugani wa serikali Mbunge,Mkuu wa Mkoa,Mkuu wa
Wilaya,Waziri wa Kilimo wala Rais aliyetembelea hapa “,anasema Mhagama.
Mhagama anasema hayati Dk.Gama akiwa Mbunge
wa Songea Mjini alipeleka teknolojia ya mbolea ya marejea bungeni ili Waziri wa
Kilimo aweze kufuatilia zaidi kuhusu matumizi ya mbolea hiyo na kwamba jambo la
kusikitisha tangu wakati huo hadi sasa hakuna ufuatiliaji wowote wala hatua za
kuhakikisha wakulima nchini wanahamasishwa kutumia mbolea ya marejea.
Mtaalam huyo anasema dhana ya kilimo
kwanza ambayo ilipigiwa chapuo na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu
Mstaafu Mizengo Pinda ingeweza kupata mafanikio makubwa endapo watanzania wote
wangetumia mbolea ya marejea ambayo ni endelevu kwenye udongo.
“Serikali ingenipa nafasi hata ya saa
moja katika Bunge la Muungano ningeweze kutoa elimu hii kwa wabunge wote
naamini wabunge wangehamasisha wapiga kura wao kuachana na mbolea za viwandani
na kuanza kutumia mbolea ya marejea”,anasisitiza Mhagama.
Naye Mwakilishi kutoka Shirika la
Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM) Noel Kwai anasema kilimo hai sio kitu kigumu kwa sababu Mkulima
wa kawaida anaweza kutumia mbolea za asili ambazo ni endelevu na hazina madhara
kwenye udongo.
“Historia inaonesha kuwa Kilimo Hai
kimeanzia Peramiho ambako waligundua mbolea ya marejea ”,anasema Kwai.
Albano
Midelo ni Mchangiaji wa gazeti hili unaweza kuwasiliana kwa simu 0784765917,baruapepe
albano.midelo@gmail.com
Post a Comment