Ads (728x90)

Powered by Blogger.




“Kabla ya kwenda  kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa  ya Afrika  mwaka 1980  (Nigeria) tulienda kuweka kambi ya mwezi mmoja nchini Mexico  na tulicheza mechi kadha wa kadha za kirafiki ili kujiweka fiti tayari kabisa kwa vita. 

Siku moja nakumbuka tulienda kucheza mechi ya kirafiki  katika mji maarufu wa starehe Uliopo nje kidogo ya makao makuu ya nchi ya  Mexico (jina sikumbuki)”.

“Katika mchezo huo  mwamuzi  alitufanyia fitina kwa kuwatoa wachezaji wetu watatu kwa kadi nyekundu  na wakati huo tulikuwa nyuma kwa bao 2-1, kwa bahati nzuri Peter  Tino alifanya kazi ya ziada akafanikiwa kuisawazishia  Taifa Stars lile bao na ubao ukasomeka 2-2”,Basi tulianza kucheza rafu mbaya sana kwa wapinzani wetu tuliwapiga buti hadi mwisho wa mchezo  wachezaji wa Mexico walishukuru Mungu, kwa mchezo kuisha salama”. 

“Sheria za soka zinasema mwamuzi haruhusiwi kutoa kadi nyekundu zaidi ya tatu kwa timu moja, baada ya kadi tatu nyekundu kinachofuata ni kuvunja pambano endapo timu hiyo itaendelea kufanya makosa. Sisi tulilijua hilo ndio maana tuliamua kuwachezea rafu wapinzani wetu”.

Anasimulia  Rashidi Idd Chama wengi tunamkumbuka na tutaendelea kumkumbuka kukutokana na uwezo wake  mkubwa wa kusakata kandanda aliokuwa nao  hasa miaka ya 1976 hadi miaka ya 1990 akiwa na wazee wa Jangwani Yanga, Maji Maji, Pan Afrika  pamoja na Taifa Stars.

Chama mzaliwa wa Tabora eneo la Ng’ambo, alianza kusakata kandanda akiwa katika shule ya msingi Miembeni kisha Sekondari  ya kinondoni zote za Jijini Dar es salam,  nyota yake ilianza kung’ara toka  mwaka 1971 akiwa na  kikosi cha watoto cha Yanga kwa kipindi cha miaka 5 kabla ya 1976 kusajiliwa rasmi na Yanga lakini katika kikosi cha wakubwa, umahiri wa wake wa kucheza namba zote katika safu ya ulinzi ulionekana toka alipokuwa darasa la sita (06)

Mwaka 1978  akiwa na Kili Stars alipata bahati ya kwenda kushiriki mashindano yanayoshirikisha nchi za Afrika Mashariki na kati (Challenge)  yaliyofanyika huko Nairobi (Kenya), lakini walitolewa na  Malawi katika mchezo wa nusu fainali kwa stahili ya kushangaza kwa kuwa mchezo wao ulichezwa  mara tatu ndani ya siku tatu; siku ya kwanza  timu zote zilitoka sare ya bila kufungana  zikapigwa penalti 5 kwa kila upande  na zote zilipata, mchezo ukaahilishwa hadi siku ya pili kwa kuwa sheria za kipindi kile penalti zilikuwa ni tano tu!  

Mchezo ukarudiwa  siku ya pili  lakini kwa mara nyingine mchezo ulimalizika kwa sare ya penalti 5-5,  lakini siku ya tatu jahazi la Tanzania lilienda mrama kufuatia  mchezaji wa Tanzania Kasimu Manara kukosa penalti baada ya Tanzania na Malawi kutoshana nguvu kwa mara nyingine ndani ya dakika 90 ambapo Malawi walipata nafasi ya kuingia fainali huku  Kili Stars wakikumbana na ndugu zao toka visiwani Zanzibar  katika kinyang’anjiro cha kumtafuta mshindi wa tatu na Zanzibar ililala kwa bao  2- 0 zilizofungwa na  Peter  Tino.

Mwaka 1979 alitimkia Pan  Afrika alicheza hadi mwaka 1982 na kurudi tena Jangwani ambako alikaa kwa muda mrefu hadi mwaka 1988 alipoamua kujiunga na  Maji Maji ya Songea kisha mwaka 1990 akajiunga na Pamba ya Mwanza.

Safari yake ya Mwanza iliambatana na mikosi kwa kuwa  kabla ya kucheza mechi yeyote ya ligi Pamba ilienda nchini Burundi kucheza michezo ya mjaribio kabla ya ligi kuanza,  kilichotokea aliumia mguu pasipo kucheza mchezo wowote  na akafungwa bandeji ngumu (P.o.p) na ndoto za kuchezea Pamba zikaota mbawa akarudi Dar es salaam.

Mwaka 1991 alizungumza na katibu wa Kampuni ya Ndovu  Bw. Twaa Funguo ili kuchezea timu ya yao ambapo aliichezea hadi mwaka 1996 kisha akaachana na soka.

MWAKA 1980 NCHINI NIGERIA

“Mimi ni miongoni mwa wachezaji wachache tuliopata bahati ya kwenda kuwakilisha taifa letu  nchini Nigeria, ingawa kipindi hicho nilikuwa na  umri mdogo mno,  na nilifanikiwa kuwanyang’anya namba watu ambao nilikuwa nikiwaheshimu sana katika soka la hapa Tanzania (nilifarijika sana)”.

“wachezaji ambao tuliitwa kwenda Nigeria tulikuwa na viwango vya hali ya juu kiasi kwamba hadi dakika za mwisho wachezaji ambao walikuwa na uhakika wa kwenda Afcon walikuwa wawili tu! Juma Ponda mali na Athumani Mambosasa kwa kipindi chetu wao ndio walikuwa tishio mno katika nafasi ya unyanda (golikipa)”.

“Baadhi ya wachezaji ambao  tulipata nafasi adhimu ya kupeperusha bendera ya nchi yetu (Nigeria) ni pamoja na Juma Pondamali, Athumani Mambosasa, Leopard Mukebezi, pamoja na Mohamed Kajore (marehemu). wengine ni Leodgar Tenga, Jela Mkagwa, Juma Mkambi (marehemu), Omari Husein, bila kumsahau Hussein Ngurungu, Mimi mwenyewe, Mohamed Salumu, vile vile Peter Tino”. 

“Tukiwa kule presha ya mashindano kwetu ilikuwa kubwa mno kwa kuwa ilikuwa ni mara yetu ya kwanza kushiriki michuano ya Mataifa huru ya Afrika; mchezo wa kwanza tulipepetana na wenyeji Nigeria tulichezea kichapo cha bao 2-1, mchezo wa pili tukaburuzwa na Misri tena bao 2-1, kabla ya kujikongoja katika mchezo wa mwisho dhidi ya Tembo wa Afrika Ivory Coast kwa matokeo ya sare ya bila kufungana”.

“Sisi tulitolewa  mapema kwa sababu ya woga wa Mashindano, lakini tulisakata kandanda safi, kinachoniumiza mara baada ya kutolewa katika michuano ile hadi leo hii hatujapata tena nafasi ya kushiriki mashindano makubwa kama yale kila nikikumbuka roho inauma sana”. 

“Vijana wetu wa sasa hawajitambui starehe  zimezidi tofauti na enzi zetu tulikuwa  na nidhamu ya hali ya juu ndio maana tulikuwa na miili ya kucheza mpira, mpira na starehe ni vitu viwili tofauti, tunatakiwa kubadilika la sivyo AFCON tutaisikilizia kwenye bomba”.

 Ushauri kwa soka la Tanzania.

“Ili kukuza soka letu Rais wa shirikisho la mpira wa miguu hapa Tanzania  lazima atutambue  na kuheshimu  michango yetu sisi wachezaji wa zamani ambao tulitumikia taifa hili kwa mafanikio makubwa, kama atatupuuza basi vijana wetu watakosa madini toka kwetu”.
“Sisi wachezaji wa zamani hapa nchini kusema kweli hatutambuliki kama wachezaji wenzetu katika nchi zingine, tatizo tunachagua viongozi wa soka kisiasa, tuangalie watu wenye sifa ambao wanaujua mpira na wapo tayari kujitoa kwa ajili ya soka letu”.
Maisha baada ya Soka

 “Umri wangu ni miaka 60, nafanya biashara ndogo ndogo, nina duka la vifaa vya michezo hapa mjini Arusha, vile vile nina mke na watoto  watatu mmoja wa kiume ambaye  naamini atarithi mikoba yangu  kwa sasa yupo kwenye kituo cha michezo ambacho nafundisha hapa Arusha, alikuwepo kwenye michuano ya Kopa Cocacola anaitwa Ibrahim Chama anacheza nafasi ya ushambuliaji.


Post a Comment