Ads (728x90)

Powered by Blogger.



Utangulizi

Tegemeo la Mungu kwa binadamu Mkristo anayeishi katika nchi ya Tanzania ni kuishi kwa amani na utulivu akishirikiana na kila mmoja katika jamii kwenye shughuli zetu za kutafuta ridhiki au masuala ya kumwabudu Mungu n.k.

Binadamu anayatenda hayo si kwa sababu ya mikazo ya viongozi wetu wa nchi wanaodai tuishi hivyo, bali Bwana wetu Yesu Kristo aliye kiongozi wa dini hii ya Kikristo alikazia hivyo (Tazama Yohana).

Isitoshe Mkristo Mtanzania aliyekomaa kiimani analazimika kuwa na matendo ya kweli kuhusiana na amri ya mapendo, kutenda haki na kuishi kamilifu katika mambo yote mazuri na maendeleo bora ya binadamu katika nyanja mbali mbali ikiwemo ile ya elimu, maisha ya jamii, Afya, uchumi, utunzaji wa mazingira, demokrasia n.k.

Mungu wetu anataka tumtumikie na tumtii  hapa duniani bila kusahau kupiga vita umasikini, ujinga na maradhi (wazo ambalo waasisi wetu wa taifa walitukazia katika nyakati tofauti).

Baada ya nchi yetu kupata uhuru Desemba 09, 1961 Baba wa Taifa Jk Nyerere alisisitiza sana suala la kufanya kazi, Mwenyenzi Mungu anafurahishwa sana na Mkristo anayekuwa na dira chanya ya maisha katika hali ya nidhamu huku akiwa na tabia ya ubunifu, ujasiri, juhudi na uthubutu wa kutenda mema na uamuzi wa kupambana katika kuondoa maovu.

Vile vile uaminifu katika kutunza uhai, kutunza mazingira  pamoja kuzingatia malezi bora ya kikiristo katika ngazi zote kuanzia Familia, Jnnk, Mtaani, Kigango, Parokia n.k. 

Waasisi wa nchi ya Tanzania
Miaka 56 iliyopita nchi inayoitwa Tanzania haikuwepo, ni jambo la msingi kuelewa hilo kwa kuwa nchi yetu ilipata uhuru mwaka 1961 awali ilijulikana kwa jina la Tanganyika kabla ya kuungana na Zanzibar mwaka 1964 na kuzaliwa nchi mpya ya Tanzania tunayojivunia hadi kufikia hivi sasa.

Mara nyingi suala la muungano limekuwa likiibua mijadala mingi na kuelezea jinsi ulivyotokea, Je nia na dhamira ya waasisi wa taifa la Tanzania lilikuwa ni nini? Tunapotafakari jambo hili tulejee maneno ya Hayati J.K. Nyerere  kuhusu thamani ya muungano na sababu za kuunda, alisema tunaposema kuna Mtanganyika na Mzanzibar tutaendelea kusema kuna Mchaga na Mkwere, dhambi hii itatutafuna hivyo sio kosa kukubali kama nchi ya  Tanzania kuwa ni Tanganyika ambayo 2017 imefikisha miaka 56.

Taifa lilianza na imani iliyokazia umoja wenye misingi ya haki, ukweli, mshikamano na upendo huku lengo likiwa ni kuleta ustawi wa wote na hivi kudumisha amani. Hii ni imani toka kwa Bwana wetu Yesu Kristo aliyesema “nawaombea mpate kudumu katika umoja” (Taz Yoh. 17:1-26).

Shida zinazomzunguka Mkristo wa Tanzania
Tanzania kuna Amani kwa hoja ya kutokuwa na vita ama vitendo vya kutumia nguvu huku taifa la Tanzania likipata sifa mbele ya mataifa mengine na kusifiwa kwamba ni kisiwa cha amani.

Mpaka sasa watanzania tunajivunia kwamba nchi yetu ni kisiwa cha amani, Je tunu hii tunaidumisha, kuilinda na hata kuiendeleza?
Kutojali maslahi na ustawi wa wote ni moja ya changamoto kuu inayotukabili. Amani yetu imezingirwa na lindi la umaskini, maradhi na ujinga miongoni mwa watanzania walio wengi.

Dira tuliyojiwekea ya kupambana na maadui bado hatujafikia licha ya kwamba kunajitihada nyingi zimefanyika lakini hazijaleta matokeo ya kuridhisha. Sababu ni nyingi lakini mojawapo ni kukosekana kwa uzalendo, uthubutu, ubunifu na kutokujiamini.

Fikra tegemezi zinatutafuna na ubinafsi unatumaliza, kujali utu wa kila mmoja kama walivyofanya waasisi wa taifa letu umeambatana na vikwazo vingi mno jambo ambalo ni ngumu kukataa kuwa kuna vikwazo toka nje ya Tanzania.

Inaonyesha sisi bado ni watumwa kupitia ukoloni mamboleo, wakoloni waliwatumia watu wetu wa ndani kututawala kama vile machifu, wakati leo wanatutawala kisiasa, kiuchumi na kijiamii; kwa kuwatumia wanasiasa, wataalamu, wanavyuoni na dini mbali mbali.

Inatupasa kujitambua na kubadili ukweli huu ni wajibu wetu sote “watanzania” na sio kazi ya mwingine toka Magharibi wala Mashariki. Kusimamia ukweli au kutetea haki sio jambo rahisi ni kazi ngumu mno, kwani Injili inatuambia kwamba: ukweli utawaweka huru (Taz. Yoh 8:32).

Nyerere na vita dhidi ya Rushwa
Mwasisi wa Taifa la Tanzania J.K. Nyerere ambaye yupo kwenye mchakato wa kutangazwa kuwa mwenye Heri na hatimaye Mtakatifu. Kwa hakika Kanisa limefanya vema kuanza mchakato huo mapema lakini muhimu zaidi ni kupokea majibu na kuendeleza maadili mema aliyotuachia.

Wosia wake kwetu hakuutoa siku moja bali maisha yake yote alitoa maneno ya kinabii, huku hakifanya bidii kuishi kile alichokiamini na kujenga umoja wenye  kudhihirisha ujenzi wa ustawi wa jamii.

Nyerere alikuwa kiongozi mwenye msimamo wa kimaadili , mtu wa kila mmoja, ikiwa ndio lengo na sababu ya jitihada zake na taifa aliloliongoza la Tanzania. Aliweka dira ya taifa na kuiongoza dira hiyo kwa vitendo.

Kanisa Katoliki Tanzania
Kanisa Katoliki limeshiriki katika kupigania uhuru na kujenga Tanzania ya miaka 56 iliyopita. Kanisa lenyewe limekuwa kimuundo na katika idadi ya waumini na wazalendo wanaoshika nafasi za uongozi na uchungaji.

Kwa kuzingatia wito wake wa kutoa huduma za kiroho na kimwili, Kanisa limeweza kufahamika popote Tanzania (mjini na vijini). Huduma zake zinaendana na maana ya Kanisa Katoliki yaani jumuiya ya wote katika mambo yote bila ubaguzi wa aina yeyote ile. 

Huduma za Kanisa zimekuwa katika afya na elimu: kuwawezesha watu kuwa na maarifa na ujuzi  bila kusahau afya njema ili waweze kumtumikia Mungu na majirani.

Hivi ndivyo Kanisa linavyotimiza amri kuu na mpya ya mapendo kwa mujibu wa Injili “Amri mpya nawapeni pendaneni” (Tazama Yoh. 13:34) vile vile Kanisa limesaidia kupatikana kwa mahitaji ya lazima ikiwemo maji safi na salama.

Kwa kiasi kikubwa katika maeneo ambayo Kanisa limejengwa kuna huduma ya zahanati, shule na maji. Hivyo Kanisa linamiliki taasisi mbali mbali katika elimu na Afya lina shule toka za msingi hadi vyuo vikuu pia lina Hospitali toka ngazi ya zahanati hadi rufaa.

Kanisa pia linashiriki katika kuhamasisha watu kwenye shughuli za kimaendeleo kama vile ujezi wa barabara, kilimo,ufugaji, uvuvi n.k.

Vile vile kwenye vyama vya ushirika Kanisa Katoliki ndio mwanzilishi katika nchi ya Tanzania. Mazao ambayo ushirika ulianzia, kisha kuenea na kupanuka ni Kahawa, Pamba na Chai.
Mafaniko hayo yamekuwa ya pekee kwa Takribani Miongo miwili iliyopita kutokana na sera ya kushirikisha taasisi za dini katika huduma za afya, elimu na miradi ya maendeleo.

Mafanikio haya ya ukuaji wa Kanisa lenyewe pamoja na  huduma zake zilifanya Kanisa kugusa maisha ya watu na kutambua umaana wake katika maisha yao.

Hukimbilia “Miungu wengine” na “wakatoliki wa Mguu Mmoja”
Kanisa lina changamoto ambazo ni mwaliko wa kujitazama, kujitathimini na kufanya bidii zaidi kutimiza wito wake, ni changamoto zilizogusa Kanisa lenyewe na mazingira linamofanyia kazi.  (Inaendelea Uk.07)

Japo sio rahisi kupima maendeleo na mafanikio upande wa kiroho lakini tunaweza kutumia kigezo cha maadili na imani miongoni mwa waamini wa Kanisa hilo.

Inavyoonekana waamini wengi hawana imani thabiti na maisha yao kiujumla hayaongozwi na mafundisho ya Mungu (ujumbe wa Yesu Kristo).

Ukweli huu tunauona pale linapotokea tatizo au mgogoro katika maisha, watu hukimbilia miungu. 

Kwa hiyo ushirikina unaendelea, zaidi ya hayo watu hutafuta mafanikio katika biashara, kazi, kupambana au kubaki katika cheo, pia ushindani katika medani za kisiasa.

Vile vile mila na desturi zilizo kinyume na ujumbe wa Injili bado zinaongoza maisha ya baadhi ya waumini yakiwemo matambiko. Kutokana na imani hafifu watu wanaamini kwamba wanaweza wakatatua matatizo yao kwa njia ya miugiza.

Baadhi ya wakatoliki wamelihama Kanisa lao la kweli na kuingia madhehebu ya Pentekoste. Baadhi bado wamo lakini wanafuata ukatoliki kwa mguu mmoja.

Labda Kanisa linakosa kukidhi mahitaji na matarajio ya wafuasi wake na hivyo wanatafua msaada kwingine. Hili nalo si jambo la kudharau. 

Jitihada za kukuza imani na kipaumbele kwa Kanisa tuangalie juu ya elimu ya dini na tunawafikia kwa asilimia ngapi. 

Lakini vile vile wanaowafundisha Makatekista wana ujuzi, moyo wa kazi na wanatosheleza? Tunawasaidiaje wanandoa na familia kukuza imani na uimara. Ndoa ni Sakramenti au ni ushindi wa sherehe? Hapa mnaweza kusema mengi lakini ukweli ni kwamba tumepotoka.

Malezi ya Makatekista na Wanasiasa miaka 50 ijayo
Katika Kanisa Katoliki, hapa katika misingi ya imani yetu  tunayo mapungufu kadhaa katika utendaji wetu kwa kipindi cha miaka 56 toka uhuru, inatupasa kuomba toba kisha kujipanga upya na kushiriki kujenga maisha ya watu kiroho na kuwaletea maendeleo katika miaka 50 ijayo.

Kwa mwelekeo wa sasa kutokana na kupungua ufadhili toka nje kipaumbele cha kwanza cha Kanisa ni kutafuta fedha, kujenga Makanisa na tasisi za elimu.

Si mbaya, lakini tuone zaidi umuhimu wa
malezi ya kiroho kwa watu wote, mkazo ukiwa kwa watoto na vijana, lengo ni kumjenga kila mmoja toka katika ngazi
ya familia na popote anapotoa huduma au kufanya kazi basi aweze kuongozwa na neno la Mungu na aweze kuchochea tunu za Injili na kuishi ushuhuda wa Kristo.

Kanisa linaelekea kusahau mafundisho ya dini mashuleni kulingana na changamoto za sasa, kazi za Makatekista ni muhimu sana kwa maisha ya Kanisa. 

Mahitaji ni makubwa sana kutokana na ongezeko la shule za msingi na Sekondari, umakini unaitajika ili kuwanusuru vijana na watoto wetu miaka 50 ijayo.

Wanasiasa na watendaji wengine serikalini wakiwemo wanataaluma wakatoliki lazima watambumbue umuhimu wa kufanya kazi kwa kufuata misingi ya uadilifu, uajibikaji na uwazi wenye kuendana na maadili ya Kanisa Katoliki.

Yafaa Kanisa kuwa na utaratibu wa kutatua matatizo madogo madogo na kutatua migogoro kabla haijafika katika hatua ya kusambalatisha familia. 

Tukumbuke familia ni msingi na chimbuko la jamii, Kanisa na taifa; kwa hiyo matatizo mengi yaliyopo kwenye kizazi hiki cha leo yanatokana na udhaifu wa chimbuko katika “familia”.

Ni dhahiri familia za miaka hamsini iliyopita ni tofauti na zile za leo na udhaifu na changamoto ni nyingi zaidi kwa wakati huu. Miongoni mwa sababu kuu ni mabadiliko ya kiuchumi na kiutamaduni, ambayo yameathiri kwa kiwango kikubwa mfumo wa maisha ya familia na jamii nzima.

Je, Sherehe ni Muhimu kuliko Malezi? au Tumepotoka?

Zaidi tumeshindwa kutafakari kwa makini mabadiliko hayo na kutafuata namna nzuri ya kuyapokea bila kuathiri tunu msingi za jamii, Maadili ndani ya Kanisa ni Changamoto nyingi na nzito; Walei na Makleri wote tunahusika.

Sababu kuu ni imani hafifu, kujenga imani ni kazi endelevu inayowalazimu wadau wote kutimiza wajibu wao. Kudhihirisha kuwa kazi hii endelevu ni kama imetelekezwa, ufisadi umetapakaa toka ngazi ya familia na ngazi zote za Kanisa.

Vile vile katika vyama vya kitume, watendaji na wanasiasa wakristo wakatoliki, badala ya kuwa mashahidi wa Injili, baadhi wamekuwa ni mabingwa wa kukiuka maadili ya kikiristo katika utumishi wao; amri ya kumpenda Mungu na jirani inayotakiwa kudhihirishwa katika kutenda haki, kuushinda ubinafsi na kushughulikia maslahi ya wote hasa wanyonge  limekuwa tatizo.

Matabaka yanaendelea kuimarika, walio nacho wakijiwekea mazingira na hata sheria zinazowawezesha kuendelea kujineemesha huku wasiokuwa nacho wakiendelea kuwa hohehahe wangine wakiishi maisha yaliyo kinyume na utu wa binadamu.

Moyo wa kazi na uwajibikaji ni janga lingine ambalo taifa limeingia. Kanisa limeshiriki kwa jitihada kubwa na kwa njia za madharia na vitendo kujenga moyo wa kazi na tabia za kuheshimu kazi.

Karibu kila mmoja ana uwezo wa kufanya kazi, aliye na uwezo wa kufanya kazi anatumia vipawa vyake kujitafutia mahitaji na kushiriki kujenga jamii.

Moyo wa kujitolea na kujali maslahi kwa wote ilikuwa ndio mtindo wa maisha kwa sehemu kubwa katika maisha ya watanzania lakini thamani na maana ya kazi katika maisha ya mwanadamu  imetoweka toka ngazi ya familia na athari zake zinaonekana wazi Kanisani na kwenye huduma mbali mbali za kijamii.

Bila kazi hakuna maendeleo mfano hai ni miaka 56 ya uhuru na hali ya Tanzania kisiasa, kiuchumi na kajamii sio ya uhakika inazidi kuelekea kila kukicha. 

Vipaumbele vyetu ni sahihi katika matumizi ya mali na muda? Hili ni tatizo kubwa kwa jamii nzima ya Tanzania tangu familia hadi taifa.

Tujiulize kipi ni muhimu programu ya malezi ya kiroho na maadili au kujenga Makanisa makubwa na kuchangia sherehe? Je, maandalizi ya kiroho ya vijana wanaojiandaa kufunga ndoa au kupokea Sakramenti nyingine ama ni maandalizi ya sherehe kubwa?
Liwafikie na kuwapatia malezi  kimaadili. Ni lazima tuelewe kuwa tukiwaacha peke yao watashindwa kwa kuwa nafasi hizo zinaambatana na majiribu na udhaifu ambao unahitaji neema ya Mungu kuweza kuushinda.

Nafasi yao katika kuleta mabadiliko na kujenga Tanzania ya miaka 50 ijayo ambayo ni maisha bora kwa kila mtanzania ni kubwa na ni muhimu mno ili kuwasindikiza katika kuwa mashahidi wa Injili katika utumishi wao.

Katika Sinodi ya pili ya Afrika (1994), Kanisa la Afrika limehimiza kujibidisha kutenda haki ili liweze kuthubutu kuzungumzia wengine juu ya haki. Ujumbe huo bado ni hai kwa Kanisa la leo.

Kanisa ni mwalimu mzuri, lakini kuwa mfano kwa vitendo hapo tuna udhaifu mkubwa. Tunayo mafundisho na pia maazimio na maamuzi ambayo  kama yanatekelezwa sura ya jamii isingalikuwa hivi ilivyo.

Kutotekeleza tunayoyaazimia ni kosa, ni dhambi. Tukiri na kuomba radhi au toba na tujibidishe kufikisha mafundisho kwa watu na kutekeleza maamuzi yetu huku tukifanya bidii kuishi yale tufundishayo.

Upande wa walengwa katika mafundisho ambayo zaidi ni walei na pengine huwa na Wakleri kwa pamoja ama Wakleri peke yao tuone kasoro yetu kubwa katika kuitikia na kushiriki kujifunza.

Mara nyingi maandalizi mazuri hufanyika lakini walengwa wachache sana ndio huitikia. Hii inakatisha tamaa. Lazima tuelewe kwamba tunawajibika kujifunza kila wakati ili kupata kuelewa na maamuzi mapya kadiri ya mahitaji na mazingira tuliyomo.

Vizingizio vya kukosa muda tusiviendekeze, kwani cha muhimu ni kuwa makini na kuchagua vipaumbele vyetu kwenye matumizi sahihi ya muda ambao Mungu anatujalia.
Na George Milinga
Parokia Peramiho


Post a Comment