Na
Alex Mapunda
Wamatengo
ni kabila dogo linalopatikana mkoani
Ruvuma katika wilaya ya Mbinga upande wa Mashariki, Wamatengo wanaishi sehemu
za milimani eneo ambalo lina hali zuri ya hewa pamoja na ardhi yenye rutuba
inayowawezesha kulima mazao kama kahawa, mahindi, ngano n.k. kama ilivyo kwa
makabila mengine Wamatengo nao wanasifa ya ukarimu, kuchapaka kazi na hata
katika upande wa mahusiano wana vitu vingi vinavyowatofautisha na makabila
mengine.
Katika
suala la mahusiano Kijana wa kiume
anapobalehe wazazi humshawishi atafute mwenza kwa kumwambia; “sasa tafuta jiko
lako, wewe sasa ni mkubwa kwa kuoa”. Miaka ya nyuma ilikuwa sio rahisi kumpata
mchumba kwa sababu wasichana hawakuruhusiwa kwenda shule wala kukusanyika
katika matamasha kama ilivyo sasa. Vijana wa kiume walilazimika kwenda kuwinda
wasichana kwenye shughuli za matanga, michezo ya ngoma maarufu kwa jina la
Mhambo, Chihoda au kwenda nyumbani kwa wazazi wake.
Kwa
kawaida Ndoa ni muungano wa hiari kati ya mume na mke wenye nia ya kuishi
pamoja mpaka mwisho wa maisha yao au mmoja wao, ili ndoa iweze kufungwa sheria
inafafanua kuwa umri wa wanandoa uanzie miaka 18 na kuendelea, licha ya kwamba
vijana wanaweza wakaoana chini ya umri huo kwa sababu maalamu (chini ya
uangalizi wa wazazi) kwa kibari cha mahakama. Kuna ndoa ya Kidini, Serikali
pamoja na Kimila.
Asilimia
kubwa, Wamatengo wanafunga ndoa za kimila kuliko ndoa za kidini au za serikali
na wanaishi uchumba bila kufunga ndoa ya Kanisani kwa muda mrefu wakati wao ni
wakristo, sheria za Kanisa haziruhusu wakristo wa jinsia tofauti kuishi pamoja
kama bibi na bwana bila kufunga ndoa. Amri ya 06 kati ya Amri 10 za Mungu inafafanua
suala la unzizi; kufanya mapenzi bila kufunga ndoa ni dhambi kwa mujibu wa
Kanisa. Baadhi ya sababu zinazowafanya wamatendo waishi uchumba muda mrefu bila
kufunga ndoa:
Utandawazi; Hadi
kufikia miaka ya 1990 taratibu za Kanisa kuhusu ndoa pamoja na taratibu za
kimala zilifanana kwa kiasi kikubwa; moja wapo ni kuto waruhusu wachumba kuishi
pamoja bila kufunga ndoa au bila kutoa mahari na kipindi kile wamisionari
walifanikiwa kulifikisha neno la Mungu kwa usahihi mikononi mwa wazee wa kimatengo hivyo iilikuwa rahisi
kuwashawishi vijana wao kufunga ndoa kabla ya kuishi pamoja. Kwa sasa utandawazi umeingilia kati
vijana wanakutana tu njiani na kwenda kuishi pamoja bila wazazi kupewa taarifa
wala hawajali amri 10 za mwenyenzi Mungu. Hivyo ni mara chache mno kushuhudia
vijana wakifunga ndoa kabla ya kuanza kuishi pamoja.
Tamaa; Wanaume
wengi wa Kimatengo wana tamaa ya kuoa mwanamke zaidi ya mmoja au baada ya
kuoana anaishi nae kwa muda fulani tu! na kuoa mwingine, hivyo wanaogopa
wakifunga ndoa watabanwa na sheria pindi watakapoamua kumwacha wa kwanza na kuoa
mwingine: “wengi ni wajanja wanaishi na mwanamke kijanja wakimchoka wanatafuta
mwingine au anaweza akaoa mke wa pili na kumwambia yule wa kwanza kwamba naenda
kufunga ndoa na huyu wa pili” anasimulia Mzee Union Komba Mkazi wa kijiji cha
Manzeye Wilayani Mbinga. Wanaume wa kimatengo hawajazoea kuishi na mwamke mmoja
toka ujana hadi uzee hali ambayo inawafanya waoe mke zaidi ya Mmoja maarufu kwa
jina la “Mitara”
Mahari; Baadhi
ya wazazi wanaweka kipingamizi cha kufunga ndoa kwa kigezo cha mahari, kabla ya
harusi wanataka upande wa mwanaume watoe kwanza mahari yote waliyokubaliana
tofauti huweka zuio na wakilazimisha kufunga hutoa laana kwa binti yao kwa
kusema “kama tulikuzaa sisi basi kuanzia leo sisi sio wazazi wako tena, na
tusikuone kwetu”. Licha ya kwamba siku hizi wazazi wengi wameelimika na suala
la kuwazuia vijana wasifunge ndoa kwa sababu ya mahari limepungua kwa kiasi kikubwa mno.
Elimu; “Baadhi
ya vijana wanapoenda masomoni wana kawaida ya kuoa na kumwacha mwanamke kwa
wazazi wao bila kufunga ndoa, suala ambalo ni kinyume na sheria za Kanisa
ambapo hadi kumaliza masomo inachukua muda mrefu, hali hii inapelekea wao
kuishi katika uchumba kwa muda mrefu bila kufunga ndoa kwa miaka 10 hadi 35”
alisema Mzee Komba.
Viongozi
wa dini wana kazi kubwa sana ya kuwaelimisha Wamatengo ili waweze kufunga ndoa
kabla ya kuishi pamoja kwa kuwa hadi sasa wamejitahidi kutoa elimu lakini
hakuna mafanikio. Utandawazi umeingilia kati na vijana hawashikiki wala
hawaambiliki, wengi wao utasikia wakisema “suala la kufunga ndoa kabla ya tendo
ni sawa na kuuziana mbuzi kwenye gunia” na sheria za Kanisa haziruhusu kufanya
mapenzi bila kufunga ndoa kwa (Wakristo).
Wazazi;
Wazazi ni kikwazo kikubwa mno kwa vijana wa kimatengo katika suala la kufunga
ndoa, wao ndio washauri wakuu na wanauwezo wa kusema ndoa ifungwe au isifungwe.
Wazazi wanaamini kwamba kipimo kimojawapo cha vijana wao kuishi pamoja bila kuachana
(milele) ni lazima waishi kwanza bila ndoa angalau miaka mitano (05), hata kwa
vijana waliosoma nao wameshindwa kutumia taalama zao ili kuwashawishi
wanaoshikilia mfumo huo waachane nao; cha kushangaza na wao wametumbukia shimoni na kusahau taratibu
na maadili ya Kanisa Katoliki.
Sifa; Kwenye
suala la Ndoa Wamatengo wengi wanapenda kuonekana, kijana anatumia miaka 15 ili
kujiandaa na harusi kwa kuamini kwamba ndoa bila sherehe inapoteza thamani,
hata kama kipato cha wanandoa ni kidogo wanajitahidi kwa namana yeyote ile ili
kufanikisha sherehe. Ndoa zinazofungwa bila sherehe zinaitwa ndio za “Mafungu”
au “Ndio za mikeka” au “Ndoa za walalahoi” na mara nyingi wanandoa wanaofunga
ndoa ya mkeka wanakosa furaha au amani kwa kuwa wanachekwa na wenzao katika matukio
mbali mbali kama vile sherehe, misiba n.k.
Kuiga; “Kwa
kuwa Baba alifunga ndoa baada ya kuishi uchumba kwa kipindi cha miaka 20 basi
na mimi nitakaa kama Baba au rafiki yangu alifanya sherehe kubwa siku ya arusi
yake basi na mimi nitafanya sherehe kubwa kama yeye, pasipo kuangalia hali ya
uchumi wangu ipoje zoezi ambalo linapelekea wanandoa kujiingiza kwenye madeni
yasiyo ya lazima” anaeleza Damas Januari kijana wa kimatengo ambaye toka ameoa
ana miaka minne na bado hayafunga ndoa.
Miaka
25 ambayo Katekista Jonas Komba amefanya kazi ya uchungaji katika Kanisa la
Manzeye huko Mbinga, ndoa alizoandikisha kwa kutumia mkono wake wa kulia, zote
wahusika waliishi pamoja (uchumba) kwa kipindi kisichopungua miaka mitano na
zaidi; “wengi wanaoana bila kufuata taratibu za Kanisa, kwa madai kwamba
wanaenda kuchunguzana tabia, mara nyingi wanahukumiwa na mafundisho ya Komunio
ya kwanza au kipaimara kwa watoto wao, wasiofunga ndoa tunawasitishia huduma za
Kanisa. Kufunga ndoa ni tendo la kheri, anayejua kuhusu hatima ya maisha yetu
ya hapa duniani ni Mungu peke yake” alilisitiza Kat. Komba.
Padre
Christian Mhagama amefanya wa Jimbo Katoliki la Mbinga, hivi karibuni
aliliambia Gazeti la Mwenge kwamba ndoa ambazo amefungisha zinazowahusu Wamatengo
hadi kufikia leo ni zile tu! ambazo wanandoa waliishi katika hali ya uchumba
kuanzia miaka Saba (07) na kuendelea; “ Wamatengo wanafunga ndoa baada ya
kuishi pamoja kwa muda mrefu, kitu ambacho kinatushangaza wengi. Wanafunga ndoa
baada ya kuishi miaka 10 hadi 20. Kila
nikipata fursa ya kufungisha ndoa, kwanza nataja Kanisani idadi ya miaka ambayo
Bibi na Bwana harusi wameishi katika hali ya uchumba, ikiwa chini ya miaka 10
basi tunawapongeza kwa kufunga ndoa mapema” alisema Padre Mhagama (yupo mbinga
kwa takribani miaka 11 sasa).
Yatupasa
kutafakari kwa kina kuhusu namna ambavyo tutaenda mbinguni bila kuchoka, suala
la Wakristo kuishi uchumba bila kufunga ndoa lipo katika makabila mengi na sio
kwa Wamatengo tu! Sote inatupasa kutubu zambi zetu, kumrudia Mwenyenzi Mungu na
kushika amri zake, Amina.
Post a Comment