Na
Alex Mapunda, Ruvuma
TIMU
ya Parangu Fc imeendelea kugawa pointi kwa wapinzani wake katika mashindano ya
Ansgar Cup ngazi ya Tarafa, mara baada ya kukumbana na kipigo cha bao 4-1 dhidi
ya Kilagano Fc kwenye dimba la Ansigar Peramiho.
Katika
mchezo huo ambao Parangu ilielemewa kila idara, mabao ya Kilagano Fc yalifungwa
na Liambi Kipanga dakika ya 26, Fred Membe dakika ya 31, Frey Ngonyani dakika
ya 34 kabla Jofrey Soka kushindilia
msumari wa nne kwenye geneza la Parangu mnamo dakika 78. Bao la kufutia machozi
kwa upande wa Parangu Fc liliwekwa kimiani na Erick Nyoni dakika ya 62 katika
ungwe ya lala salama (Kipindi ya pili).
Kivutio
kikubwa katika mchezo huo ni kwamba wachezaji wote ambao walivaa jezi namba 11,
yaani Frey Ngonyani toka Kilagano Fc pamoja na Godfrey Hala toka Parangu Fc
walitolewa nje kwa kadi nyekungu baada ya kukiuka sheria na taratibu za mpira
wa miguu.
Timu
zote mbili zilikumbana na kichapo katika michezo yake ya awali ambapo timu ya
Parangu ilitandikwa bao 2-1 dhidi ya timu ya Litisha wakati Kilagano Fc
ilikung’utwa na Peramiho (Afya Fc) kwa jumla ya bao 3-0.
Katika
michezo mingine timu toka kata ya Litisha iliifunga Peramiho (Afya Fc) bao 1-0,
Liganga Fc iliichabanga Mpandangindo bao 3-2 kisha Maposeni Fc ikaishindilia
Lilambo bao 2-1 katika mchezo ambao Lilambo waliianzisha vurugu.
Mwaka
huu zawadi zimeboreshwa toka shilingi 300,000/= kwa washindi wa kwanza hadi
shilingi 400,000/=, 250,000/= washindi wa pili hadi shilingi 300,000 pamoja na
150,000/= washindi wa tatu hadi 200,000/= huku mchezaji bora akiambulia kifuta
jasho cha shilingi 50,000/= hali ambayo
imesababisha ongezeko la ushindani na kila timu shiriki inatamani kunyakua
ubingwa wa mshindano hayo.
Ansgar
cup ni moja ya ligi kongwe mkoani Ruvuma na imedumu kwa zaidi ya miaka 20,
lengo kubwa la mashindano ya Ansgar yanayoandaliwa na mkurugenzi wa Hospitali
ya Peramiho Dkt Ansigar Stuffe OSB ni kuibua vipaji kwa wachezaji, burudani
baada ya kazi, kuongeza soko la biashara kwa wafanyabiashara wa tarafa ya
Peramiho n.k.
Baadhi
ya wachezaji waliotokea Ansgar Cup ni pamoja Pato Ngonyani (Maji Maji, na
Yanga), Anold Nguruchi na wengine wengi.
Post a Comment