Kwa asili Wangoni ni kabila linalotokana na ukoo wa akina Zulu na wale wa aina ya
Wathonga ambao ni kundi shiriki la kabila la Wangoni ndio walioruhusiwa
kushika madaraka ya uongozi katika serikali ya kikabila.
Lakini hali
hiyo ilibadilika baada ya Wangoni kupata makazi ya kudumu. Wangoni kutoka kundi
la Wakatanga, Wasenga, Wasukuma n.k. waliruhusiwa kutawala kama Manduna
(subchiefs) katika maeneo yao, vyeo ambavyo walikabidhiwa watu wenye akili ya
kuongoza jeshi kwenye vita. Lakini amkio kuu la “Bayete” lilitumika kwa chifu
Mkuu yaani Nkosi tu!
Walichofanywa Wangoni na
Waingereza
Kutoka
mahali ambapo Wangoni waliweka masikani yao ya kudumu, walikuwa na tabia ya
kuwashambulia majirani zao. Kadiri
walivyoendelea kuviteka vijiji, makabila mengi yalijisalimisha kwa
Wangoni hali iliyopelekea kabila hilo kupanuka kwa kuwa mateka wengi waliingizwa
moja kwa moja kwenye kabila lao.
Lakini
vijiji vingi vya wenyeji vilijisalimisha
chini ya himaya ya Wazungu (Waingereza) hivyo iliwawia vigumu sana
Wangoni kuviteka na kupata matatizo walipojaribu kuviteka. Kwani waingereza
ukianzia huko Zomba Nyasaland (Malawi)
chini ya Afisa wa Kiingereza aliyejulikana kwa jina la Sharpe aliliongoza jeshi la kiingereza
ambalo lilijitoa mhanga dhidi ya Wangoni kisha akafanya nao vita kwa lengo la kuwazuia Wangoni wasiwashambulie
watu (wenyeji) waliokuwa chini yao. Wangoni aina ya Ngomani
walishambuliwa na kikosi hicho cha jeshi la Waingereza na hivi
kulazimika kusalimu amri na kukubali kuwa chini ya uingereza. Waliojisalimisha
kwa waingereza bila kumwaga damu, walikuwa ni Wangoni wa aina ya Mbelwa.
Mwaka 1889
Afisa wa Kiingereza ililichukua jeshi la Wangoni wa aina ya Mpezeni na kuliweka
chini ya utawala wa Waingereza. Lakini Afisa huyo alipokwenda likizo (Ulaya).
Jeshi la Mpezeni liliamua kuasi chini ya Mpezeni mwenyewe na mwanae
aliyefahamika kwa jina la Nsingu kisha
wakakataa kabisa kutawaliwa na Waingereza ambapo waliamua kuanzisha vita dhidi
ya wazungu kwa kuwafuata hadi Forte Jameson sehemu iliyokaliwa na waingereza
wengi sana.
Mkuu wa
kikosi cha Waingereza Bw. Brake, aliyewalisi kutoka “Bua ili kuliimalisha jeshi la waingereza na
kulipiga jeki, alifaulu kulishinda jeshi la Wangoni wa Mpezeni. Mzungu huyo kwa
ushenzi alimwua Nsingu mwana wa Mpezeni.
Mpezeni mwenyewe walimfanyia unyama wa kumchomea mashamba yake ya chakula katika vijiji vyake
na baadaye Wazungu wakateka mifugo yake
yote. Mpezeni baada ya kukiona kisanga hicho
yeye na raia wake waliamua kujisalimisha kwa waiingereza.
Mambo hayo
yote yalitendeka mwaka 1897. Mpenzeni alikufa mwaka 1900 na kiti chake
kikatwaliwa na Mpezeni Cholowa, Mtwalo alikufa mwaka 1890, Mbelwa alikufa mwaka
1891 mrithi wake alikuwa Chimtungu aliyekufa mwaka 1924. Mrithi wa Chimtungu
alikuwa Mkuzo aliyekufa mwaka 1927, na
kurithiwa na Lazaro Chikupizga.
Wangoni wa Afrika ya Kati
Hadi leo bado kuna
makundi matatu ya Wangoni waishio Afrika ya Kati ambayo ni Wangoni wa aina ya
Mpezeni, Mbelwa na Mseko. Kwa kuingiliana katika suala la kuoana na makabila ya
wenyeji, Wangoni hao walipanua kabila lao na kuongeza nguvu huku makabila
yaliyotawaliwa yakiingizwa kwenye kabila la Wangoni.
Hali hiyo
ilipelekea idadi ya Wangoni kuongezeka toka 25% hadi 75% katika kabila la
Wangoni hasa vijijini ambako kwa kiasi kukubwa kunakaliwa na Wangoni halisi. Baadhi ya Wangoni
kiidadi ni watu wenye kuongea lugha
zaidi ya moja. Mara nyingi Wangoni hao huacha kuongea lugha yao na kuongea
lugha za wenyeji.
Mwaka 1936
Wangoni wa Rhodesia ya Kaskazini (Wangoni wa Mpezeni) walikuwa 80, 000 kiidadi, wakati wale
walioishi huko Nyasaland (Malawi)
walikuwa 250,000. Kama unafuatilia kwa ukaribu idadi ya kundi hilo la
Wangoni huko Afrika ya Kati, ni kitambulisho na ushaidi tosha kwamba, Wangoni
waliofika huku Tanganyika na kuweka makazi yao ya kudumu hususani Songea ni sehemu ya ndogo tu ya kabila lote.
Katika
Afrika ya Kati kabila la Wangoni lilijulikana kwa jina la Angoni badala ya Wangoni
kwani jina Angoni ni neno la uwingi kutoka lugha ya kichewa na kinyanja. Mfano
wa maneno hayo ni:
Neno (Kinyanja
au Kichewa)
Mtu (Umoja) Mundu (Uwingi) Andu, Mtoto (Umoja) Mwana (Uwingi)
And, Msafiri (Umoja) Mlendo (Uwingi) Alendo
Mjumbe (Umoja) Mtenga (Uwingi) Atenga Mzungu (Umoja) Mzungu (Uwingi) Azungu, (Umoja) Mngoni (Uwingi) Angoni
Makabila
yaliyounda kabila la Wangoni Afrika ya Kati
Wangoni halisi huko Afrika ya Kati wametokana na makabila mengi
yaliyojichanganya na Wangoni wenye asili
ya Kizulu na Kithonga. Kama ilivyo Tanganyika kwamba Wangoni walipowasili
(Tanganyika) waliyakuta makabila mengine yakiishi, lakini Wangoni waliyateka na
kuyaingiza katika kabila lao. Makabila
hayo ya Afika yaliyoshiriki kuunda kabila la Kingoni ni pamoja na Waswazi,
Wathonga, Wakalanga, Wasenga pamoja na Wasukuma kwa mujibu wa mwandishi aitwaye Cullen Young. Ukoo wa Angoni huko
Afrika ya Kati una makundi yafuatayo:
(a) Wenye Asili ya
Kiswazi: akina Chiziwa, Chongwe, Daba, Gama, Gausi, Jere, Kambuli, Mabaso,
Mdhlopa, Madisi, Mafuleka, Mbuyisela, Ndhluli, Mgawezulu, Mhlanga, Mkala,
Mkaripi, Mlota, Mvalo, Molabandaba, Nhlane, Nkosi, Nyumayo, Nyambosi, Pakati,
Quangwane, Sibande, Sichi, Tawi na Tole.
(b) Majina ya ukoo yenye
asili ya Wakalanga ni akina Chibambo,
Gumbo, Hara, Mapara, Mbizi, Mloyo, Nali, Ndoro, Neba, Nungu, Nyanguru, shaba,
shumba, Soko na Ziba.
(c) Majina ya ukoo yenye asili ya Wasenga ni akina
Lungu, Miti, Mumba, Mvula, Mwanza, Ng’oma, Nguruwe na Tembo.
(d) Majina ya ukoo yenye
asili ya Wasukuma ni akina Chipeta, Chisi, Chuku, Mchizi, Mkawe, Mlenje, Mpepo,
Msmziya, Nkana, Ntara, Nyika, Nyoni na Tindi.
Majina ya ukoo kama akina Chongwe, Gama, Nkosi, Nyumayo, Tole, Nkuna,
Hara, Mapara, Moyo, Soko, n.k ni majina ya ukoo ya Wangoni kwa hapa Tanganyika.
Kadiri ya orodha hii ya majina ya ukoo wa kabila la Wangoni yamo majina hayo
hata kwa Wangoni wanaoishi huko Afrika ya Kati. Hata hivyo ifahamike kwamba si
watu wote wa aina hiyo wenye majina hayo ya ukoo wana uhusiano na kabila la
Kizulu, na pengine waliingia humo bila kuwa Wangoni wa Kizulu.
Post a Comment