Ads (728x90)

Powered by Blogger.


Tafiti kutoka taasisi tatu tofauti zinaonyesha kuwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara zinaelekea kuwa eneo muhimu sana la matumizi ya teknolojia. Mapinduzi hayo yana maana kubwa sana kwetu kiuchumi, kisiasa, kijamii na mengineyo.

Utafiti kutoka taasisi za Next Africa, The Economist na Pew Research Center wa mwaka 2016 zote zinakubaliana kuwa kusini mwa jangwa la  Sahara ni eneo lenye watumiaji wengi wa simu za mikononi. Kwamba kwa sasa Afrika ni sehemu bora ya mapinduzi ya teknolojia. 

Teknolojia inayozungumzwa hapa ni mambo yote yahusuyo utoaji na upokeaji wa huduma zote za kiufundi, elimu au ufahamu na pengine utumizi wa mashine mbalimbali unahusika pia. 

Dunia imerahisishwa mno kuwa na matumizi ya teknolojia. Imesaidia wagonjwa, wahudumu, wafanyakazi, wataalam, waandishi wa habari, mashirika ya habari, watendaji wa kila ngazi ambao wanategemea huduma hiyo kuhakikisha shughuli zinakwenda salama. Bila kuwasahau watumishi wa dini n.k.

Ingawaje dunia hiyo inapanda ngazi kuelekea mafanikio makubwa ya matumizi ya teknolojia, lakini wamiliki wake ni wachache sana. Mathalani, inaelezwa kuwa hadi mwaka 2009 utajiri wa dunia hii ukijumulisha na teknolojia ulimilikiwa na watu wachache sana sawa na asilimia 44 tu. 

Mwaka 2014 ilikuwa asilimia 48. Inakadiriwa mwaka 2020 kuna uwezekano mtu mmoja anaweza akamiliki asilimia 54 ya utajiri wa dunia hii. Lakini inaelezwa pia asilimia 99 ya watu wanauhitaji utajiri huo, kwani sasa teknolojia imebadilisha maisha ya watu kwa namna tofauti.

UKUTA

Teknolojia kama kitu chenye tija kwa jamii kileta mambo mengine ambayo yanajenga ukuta wa mahusiano baina ya watu. Katika zama za teknolojia hizi tumeshuhudia mambo mazuri ambapo dunia imekuwa kama kijiji chenye kila aina ya watu. Lakini vilevile teknolojia hii imechangia kujenga ukuta ambao unatenganisha baadhi ya watu wenye uhusiano au wa kijiji kimoja na pengine zaidi. 

Kwa mfano, teknolojia hii imekuja na  zama mpya za upashanaji wa habari na mawasiliano. Watu wanatumia njia mbalimbali za mawasiliano lakini wanaweza kuwasiliana na watu wasio wajua au kuwatenga wale wanaowajua na kuanzisha mahusiano mapya. 

Jambo la kuzingatia ni kwamba, watu hawa wanatumia mitandao ya kijamii, mfano Blogu, Facebook, Instagram, Twitter, Tagged, Badoo, LinkedIn, Vk, Connect, YouTube, Vimeo, Skype, Tumblr, Flickr, WhatsApp, Messenger, Snapchat, Instagram, Pinterest na kadhalika.

Teknolojia pia imetuletea SimuJanja (Smartphones) ambazo zinaweza kutumia kutwa nzima tukiwa pekee yetu bila kuhusiana na watu wengine. 

Matumizi makubwa ya simu za mikononi ambazo zinakusanya mitandao yote muhimu ya kijamii inawafanya watu wasijenge uhusiano mzuri. Kwamba watu wanaweza kushinda ndani (Indoor) kupiga gumo (chart) na marafiki au kuperuzi mitandao hiyo kwa madhumuni tofauti. Lakini unaweza kukuta ni wachache sana wanatumia kwa manufaa chanya. 

Idadi kubwa ya watu wanaojitenga na jamii na kuona teknolojia ni muhimu zaidi inazidi kuongezeka. Teknolojia inaochukua nafasi ya watu, na watu wenyewe wanakuwa si muhimu. 

Ikumbukwe mtazamo chanya wa mitandao ya jamii inayotokana na teknolojia ni nyenzo ya kuziba nakisi ya uhaba wa wapashaji wa habari na mawasiliano kutoka eneo moja na jingine. Kutoka kwa marafiki hadi marafiki. Kutoka kwa kundi la watu kwenda jingine. 

Kutoka nchi moja      kwenda nyingine.  Kwamba            teknolojia           imevunja                   vunja mipaka                 ya mawasiliano          kutoka jamiimoja kwenda               nyingine, lakini imechota kabisa        moyo wamahusiano                baina ya jamii hizo.  Kama watu wanaweza kutumia saa 24 wakiwa na simu zao za mikononi kupiga gumzo mitandaoni badala ya kutumia saa hizo hizo kujadiliana na watu au kuhusiana na jamii kidogo, ni jambo la hatari. 

Mtu anaweza kuamka asubuhi, akawasha simu yake ya Smartphone, akafungua WhatsApp, atajibu ujumbe kadhaa unaotumwa kwake. Ataingia kwenye makundi ya majadiliano na kuona kama kuna kitu cha kuchangia mawazo, akikiona basi ataandika chochote. 

Akimaliza hiyo atahamia Facebook kuona kuna nini au ujumbe gani wa kujibu kwa marafiki. Atasoma habari (nyingi zisizomjenga na za kusadikika) kwenye “News Feed”, na mwisho atatafakari au kuandika chochote cha kupigia gumzo na watu hao (asiowaona wala kuwajua).

Mwishowe atahamia Twitter kuangalia kuna nini, ataandika au atajibu anachoulizwa. Atabadilisha vilevile kwenda mitandao ya Instagram, Tagged, Badoo, LinkedIn, Vk, Connect, YouTube, Vimeo, Skype, Tumblr, Flickr, Messenger, Snapchat, Pinterest na kadhalika. Akija kushtuka siku nzima inakuwa imekwisha kwa kutumia teknolojia ambayo inamfanya awe “zuzu”. Kwamba hajui kuhusiana na watu angalau kwa dakika kadhaa kunampa nafasi ya kujenga akili pamoja na mahusiano na watu hao. Mtu wa aina hii anajikuta muda wote anatamani kutumia mitandao hiyo.

 Anaiona teknolojia katika jicho la kufungwa ndani au kutumia simu yake pasipo kuweka kando kwa muda fulani ili ashiriki masuala ya kijamii. Ni watu wa aina hii ndio huwa wagonjwa au walevi wakubwa wa teknolojia kwa njia hasi. Ni kundi la aina hii hutumia muda mwingi kusambaza habari za uzushi au mambo yasiyomjenga. 

Kimsingi teknolojia ni jambo muhimu sana katika maisha yetu, lakini uhusiano wetu na watu kiimani, utamaduni, shida, huzuni, michezo na kadhalika ni mambo muhimu zaidi. Hatuwezi kukamilika maishani mwetu eti kwasababu tunatumia kwa kiasi kikubwa teknolojia, bali tunavyoshirikiana na kutambua uwapo wa wenzetu katika maisha duniani. 

Teknolojia ni muhimu, lakini watu ni muhimu zaidi. Matumizi yoyote makubwa kuliko kawaida ya teknolojia huleta madhara makubwa katika afya zetu. Ni lazima kiasi kiwekwe kati ya muda wa kuhisiana na watu na utumiaji wake. Ni muhimu kutumia kwa manufaa. Ni hayo tu kwa leo wasoamaji wa gazeti hili. Ninawatakieni wakati mwema.



Post a Comment