Utangulizi
Siku hizi watu hukumbana na changamoto nyingi mno katika maisha yao. Kwani nyakati hizi sio jambo la kushangaa kuona uwepo wa dini nyingi na imani nyingi. Bado kuna madhehebu tofauti upande wa ukristo ambayo pengine yanapingana kwa sababu zao za msingi walizozipata wakati wa kupandikizwa imani ya kikristo.
Mambo huwa mabaya sana siku hizi pale inapotokea dhehebu moja lenye msingi ule ule katika imani, waamini wake wanapambana bila sababu za msingi.
Lazima tukubaliane kwamba hizi ni nyakati za siasa hata kwa wanakanisa, ni nyakati zanazotawala hoja za kisayansi, kimila, utamaduni na desturi na hoja za haki, binadamu na jinsia. Ni wakati tunapofadhaishwa na matatizo ya umaskini na elimu duni katika nyanja za elimu ya dini na elimu za kidunia na mengine ya namna hiyo.
Ni nyakati ambazo yanatawala zaidi mawazo ya maendeleo ya kiulimwengu kuliko maendeleo ya kiroho. Hali hiyo hupekekea kumsahau Mungu na kuacha imani zao kwa kutokumpa Mungu nafasi kubwa katika maisha yao. Na kama wanampa Mungu nafsi , basi nafsi zenyewe ni kule kuzidisha ubinafsi wa kibinadamu na hivi kuziba maana ya neno maendeleo ambalo maana yake ni hali ya kutoka kwenye uduni na kwenda kwenye hali njema.
Hali hiyo ni lazima awe nayo mtu upande wa kimwili na kiroho, hutumia elimu yake katika vitendo bila kumsahau Mungu muumbaji. Je maendeleo yalete ulegevu katika imani?
Maelezo ya Baba Mtakatifu Yohane wa 23 kuhusu wazo la Maendeleo
Miaka 59 iliyopita Papa Yohana wa 23 ambaye kwa sasa ametangazwa kuwa mtakatifu aliandika hivi katika moja ya nyaraka zake: “katika siku zetu kumezuka mawazo ya uongo ambayo yameenea sana kati ya watu. watu wanaoeneza mawazo hayo wanasema kwamba dini ambayo inadhaniwa kwamba imepandikizwa katika binadamu na maumbile, sasa lazima itazamwe kama wazo la kipuuzi tena la kufikiriwa tu.
Sasa muda umefika wa kung’oa kabisa mawazo hayo ya dini toka akilini mwa binadamu kwa sababu hayaoani kabisa na hali ya mazingira ya nyakati zetu wala mawazo hayo hayaendani bega kwa bega na maendeleo ya siku zetu (Taz Mwalimu na Mama Nb 214).
Palitokea watu katika miaka hii ya karibuni waliosema wazi wazi kwamba maendeleo kadiri ya hali yake ni maasi na mapinduzi ambapo mtu kadiri ya hali yake anapenda kuwa na furaha au raha ambayo wanasema inapatikana kutokana na maendeleo ya dunia hii kwa sababu watu wakishughulika na maendeleo ya dunia hii kuna hatari ya kusahau au kupoteza imani ya dini.
Watu hao wanaendelea kusema kwamba hata wakuu wa dini mbalimbali wanaendelea kuuza maendeleo ya siku zetu. Kwa sababu watu waliokuwa maskini na wenye njaa wanapoanza kuchukua hatua za kujibidiisha ili kuleta mabadiliko ya hali zao mbaya, wakuu wa dini hawachuchumii.
Kutokana na fikira hizi watu hao wanafikia kwenye mwisho huu: Maendeleo na dini ni mambo mawili ambayo hayaendi pamoja ama mtu anashughulika na maendeleo ya dunia hii na papo hapo anakuwa mlegevu wa dini, au anabaki katika hali ya umaskini na ujinga akiwa mfuasi kamili wa dini fulani.
Je, huu ni ukweli?
Huenda mawazo haya yametokana na kutofahamika kwa mafundisho ya dini mbalimbali yaliyotolewa Karne zilizopita. Kwa mfano: pametokea watu waliofahamu vingine kuhusu Semi fulani fulani za Biblia kama “Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mvae nini (Mt 6:25) au Bali tafuteni kwanza ufalme wa Mungu na hayo yote mtazidishiwa (Mt 6:33) au hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili….”
Hamwezi kumtumikia Mungu na mali (Mt 6:24), au ninyi si watu wa dunia hii (Yn 16:15). Kulikuwepo watu waliofahamu kuwa dini na shughuli za dunia hii ni mambo mawili yanayokwenda tofauti wala hayawezi kuoana kamwe. Kumbe ukweli wa mambo upo tofauti.
Hakuna mpingano kati ya dini na maendeleo
Mzee wa mapinduzi katika Kanisa Katoliki, Papa Yohane wa 23 alisema hivi: pasiwe hata mtu mmoja anayefikiri kwamba pana upinzani kati ya mambo haya mawili, kwamba hayawezi kwenda pamoja. Nayo ni ukamilifu wa roho ya mtu na shughuli za maisha ya dunia hii.
Haiko hivi kwamba mmoja au anaacha maisha na shughuli za dunia hii na kushughulika na roho yake tu ili ajipatie ukamilifu wa roho au mmoja anashiriki maisha ya dunia hii papo hapo akihatarisha usalama wa roho yake (Mwalimu na Mama NB 255).
Papa aliona kwamba dini na maendeleo ya dunia hayapingani bali yanakwenda kadiri ya mpango wa Mungu. Na mpango wa Mungu ni huu: mtu ajiendeshe mwenyewe kwa sababu mambo haya yanasaidia katika kupata uzima wa milele.
Iko hatari ya kupoteza Imani
Ingawa maendeleo ya dunia hii hayapingani na dini, lakini kuna hatari fulani katika maendeleo haya. Hatari yake ni kwamba watu wanajishughurisha zaidi na maendeleo ya dunia hii ambayo mapato yake yanaonekana kwa macho, huku wengi wao wakielekea kuyasahau mahitaji ya roho zao kama tulivyokwisha sema katika utangulizi.
Ni dhahiri kwamba mahitaji ya mwili yanajionyesha wazi wazi lakini yale ya kiroho hayaonekani sana, hivyo ni rahisi kusahau mahitaji haya.
Katika waraka ule maarufu ujulikanao kwa jina la Mwalimu na Mama umebainisha kwamba shughuli za dunia hii pamoja na mambo yake ingawa ni za lazima sana na zinafaa licha kuleta hatari kwa binadamu.
Hatari ni ile ya kusahau kipeo cha binadamu alichopangiwa na muumba wa vyote (Mwalimu na Mama Nb242).
Mungu alikusudia nini alipoumba Dunia?
Tunaposoma katika kitabu cha Mwanzo: “Mungu aliona kuwa kila kitu alichofanya na tazama ni chema sana” (Mw 1:30) na pia tunasoma Mungu aliwaambia watu wa kwanza: “ zaeni mkaongezeke na kuitisha dunia” (Mw 1:28).
Hapo tunaona Mungu aliwakabidhi wanadamu dunia na vyote vilivyomo ili wavitumie kwa manufaa yao. Huu ulikuwa mpango wa maongezi ya Mungu.
Kwa kweli binadamu si tu inafaa avumbue mambo katika ulimwengu au ajipatie maendeleo yake kutoka ulimwengu huu bali ni wajibu wake kufanya bidii na juhudi yake yote ili aweze kujiendeleza mwenyewe na kuwasaidia wale wasioweza kujiendesha.
Hii ndiyo amri aliyopata mwanadamu toka kwa muumba wake.
Mtaguso wa pili wa Vatikano unakaza neno hili unaposema Mungu alikusudia; dunia na vyote vilivyomo viwe kwa matumizi ya kila kiumbe (Kanisa katika ulimwengu NB69). Kwa hiyo tunaona kwamba ni wajibu wa binadamu kupata maendeleo na kuondoa chochote kinachomfanya binadamu asiweze kuendelea. Lakini maendeleo haya lazima yaelezwe kwenye kipeo cha binadamu yaani Mungu.
Hakuna ustawi kamili bila dini
Ustawi kamili wa binadamu hauwezi ukazuilika katika maendeleo ya kimwili tu. Kama ustawi utakuwa halisi lazima uweze kushika mambo haya mawili; ambayo ni dini na maendeleo ya mwili. Binadamu lazima aendelee katika mwili na roho- mtu mzima kama moja kati ya mambo haya litakazwa zaidi na jingine kupuuzwa. Hapo yanaanza matatizo. Mambo haya mawili yanatakiwa ili binadamu aweze kufikia ustawi kamili.
Papa Paulo wa VI, alipowakaribisha wajumbe walei wa Afrika huko Roma alisema: “hakuna ustawi kamili wa binadamu bila kuwako na dini” yeye anaona kwamba maendeleo ya nyakati zetu ni lazima kwa binadamu hapa duniani, lakini anaona pia kwamba maendeleo ya wanadamu hayawezi kufaulu katika mahitaji ya kiulimwengu tu. Binadamu ni muungano wa mwili na roho kama binadamu anataka ustawi kamili anahitaji pia maendeleo katika roho yake.
Utakuwa ni kivuli tu
Papa Paulo wa VI anakaza ukweli huu mara kwa mara katika hotuba zake. Kwa mfano anasema: “ toka sasa maendeleo ni neno jipya litakalosimama badala ya amani”.
Ni wazi kwamba amani kamili haiwezi kupatikana kama binadamu hatamtambua mtoaji wa amani hii, kuwa ni Mungu.
Na pengine anasema: “Kutambua kwamba yuko Mungu aliyeumba vitu vyote ni hatua ya maana sana katika maendeleo ya binadamu”. Katika waraka wake kuhusu maendeleo ya mataifa alisema: “ustawi wa watu bila kuthamini maisha ya kiroho na fikra za Mungu aliye chanzo cha maisha yote ungekuwa na maana fulani ya kivuli cha ustawi tu. (Maendeleo ya mataifa NB26).
Daraja la umaarufu wa vitu
Ni wazi kwamba Kanisa muda wote limefundisha kwa moto na kuonyesha kwa vitendo kwamba maendeleo ya ulimwengu huu na mapato yake lazima yatazamwe kama kitu cha maana katika ustawi wa binadamu.
Lakini Kanisa linafundisha pia kwamba mapato ya maendeleo au uvumbuzi huu unaofanyika sharti yapimwe sawa sawa kufuatana na hali yao.
Maana maendeleo hayo lazima yatazamwe kama vyombo kutumiwa na watu ili viwasaidie kufikia kipeo chao.
Kwa maana kama alivyosema Bwana wetu Yesu Kristo miaka elfu mbili na zaidi iliyopita na anaendelea kusema siku zote: “kwani atafaidiwa nini mtu akipita ulimwengu wote na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake (Mt 16:26).
Hitimisho
Maendeleo ya nyakati zetu kwa yenyewe hayamfanyi mtu aache dini yake au imani yake.
Ninakubali kwamba iko hatari ya mtu kusahau kipeo chake katika shughuli za dunia hii.
Lakini hapa inafika kazi ya wakuu mbalimbali wa dunia ya kuwa hodari wa kusoma alama za nyakati na kuwaelekeza na kuwaongoza watu namna ya kuyaendesha yote mawili, ambayo yanatakiwa kabisa katika maisha ya hapa duniani.
Post a Comment