Ads (728x90)

Powered by Blogger.


Kama binadamu angefanya uchunguzi juu ya maisha yake hapa duniani angeweza kugundua kwamba maovu yanaenea kupitia njia zake zote kama vile mateso, vita, mauti, umati mkuu wa watu wenye njaa na watu waliodanganyika katika tumaini.

Wakristo kupitia mafundisho yao ya Imani upande wa Kanisa Katoliki hufundishwa kuwa Mungu ni Mwema kila wakati. Kama Mungu ni mwema anaweza kukubali maovu yawepo? Na kama akiyakubali, je maovu hayatoki kwa Mungu?

Kama wakristu wanamwamini Mungu mwenye upendo na mamlaka aliyeumba na anayetawala ulimwengu, jinsi gani wanaweza kueleza nguvu ya uovu uliopo duniani? Swali hili linawahangaisha watu sana, lakini Biblia na mafundisho ya Kanisa Katoliki hujibu swali hilo na mengine yanayohusu masuala ya uovu wazi wazi kabisa.

Mafundisho ya Kanisa kwa kutumia neno la Mungu  au Biblia Takatifu hutoa majibu ya maswali hayo mintarafu maovu bila kutumia njia ndefu au maelezo marefu ya kushibisha akili au ubishi, lakini katika maana ya kuwasaidia watu ili kujenga tabia yao kuliko kuridhisha akili au ubishi tu. Na kama watu wanakubali msaada huo wa Kanisa, basi wanapokea majibu ya baadhi ya matatizo yao (Yoh 7:17).

Heshima na madaraka ya mwanadamu

Mungu alipomwumba mwanadamu kwa mfano wake, alimpa heshima na hali iliyofanya uhusiano wake na Mungu uwe wa pekee miongoni mwa viumbe wengine (Zab 8:3-8, Mt 10:31, 12:12). Wakati huo huo Mungu aliweka mipaka kwa uhuru wa mwanadamu. Mwanadamu si Mungu, anaishi akiwa mfano wake tu.

Hawezi kuishi kama ametengwa  na Mungu, sawa sawa na mfano wa mwezi katika maji, unaweza kuwepo tu kama mwezi upo. Mwanadamu anaweza kujaribu kuishi mbali na Mungu lakini kwa njia hii anajiletea  uharibufu na shida tu, lakini hawezi kuharibu mfano wa Mungu.  Hata akiwa na dhambi nyingi, bado anaendelea kuwa mfano wa Mungu (Mw 9:6, 1Kor 11:7, Yoh 3:9) ni mfano wa Mungu ndani yake unaomfanya awe mwanadamu. Habari za Adamu na Eva zinaonyesha sehemu ya heshima na madaraka ya mwanadamu akiwa mfano wa Mungu.

Akiwa mjumbe wake ana madaraka juu ya viumbe wengine walio chini yake (Mwa 1:28-30, 2:15, 19-20). Mungu alimweka katika ulimwengu alipoweza kuendelea  na kuzoeza akili zake kwa kufanya kitu cha maana. Mungu alitaka afurahie maisha yake ya pekee  kwa ukamilifu wake, lakini lazima afanye hivyo katika ushirika na utii kwa Mungu. Licha ya kuzoeza akili zake, afanye maamuzi ya kihekima na maana. Hata hivyo hana ruhusa pasipo mipaka kufanya chochote apendacho, wala kuwa mwamuzi mkuu wa mambo yaliyo mema au mabaya (Mwa 2:15-17). Mungu hana mipaka wala kikomo.  Na mwanadamu anaishi akiwa mfano wa Mungu kwa hiyo kuna mvuto ndani yake wa kutaka hali ya kutokuwa na mipaka wala kikomo na huko ndiko kuanguka katika dhambi.

Asili ya maovu

Watu wenye hekima na wenye kufikiri sana wa kale na leo hujaribu kufumbua siri ya uovu kwa kutumia maarifa yao wakitumia elimu ya Filosofia au Falsafa na wengine elimu ya Theologia. Kwa mfano Mwanafalsafa aitwaye Socrates alifundisha kwamba  kwa vile maadili ni matokeo ya elimu basi maovu au dhambi ni matokeo ya ujinga.

Aliendelea kusema kuwa mtu ambaye alikuwa anajihusisha na matendo maovu yaani dhambi huku akijua , huyo ni mjinga na pengine hawezi kufanya hivyo. Hii ina maana kuwa mtu kama kiumbe chenye akili hapa ulimwenguni shughuli yake kubwa ni kuongoza maisha yake  kwani yeye ni kiumbe chenye tabia ya kufikiri.

Naye Mwanafalsafa aitwaye Plato akiongelea juu ya asilia ya maovu hapa duniani alisema kuwa ndani ya roho ya mtu kuna maumbile yenye uwezekano wa kuwepo kwa mvurugano (disorder) unaopelekea kuwepo kwa maovu au dhambi. Kwa sababu mvurugano hutokea kwenye roho ya binadamu basi chanzo cha uovu lazima kitafutwe kwenye roho au undani wa roho ya mwanadamu au mtu, kwani maovu au dhambi ni usahaulifu na ujinga ambao hutokea ndani ya roho yenyewe juu ya dira ya ukweli.

Mtakatifu Augustino ambaye ni mwanafalsafa pia Mtheologia na mwenzake mtakatifu Thomas wa Aquino, ambaye naye ni mwanafalsafa na Mtheologia mzuri walikaza kuwa dhambi ni matokeo ya mapungufu yaliyomo ndani ya roho ya binadamu. Ukifuatilia maelezo ya wataalam hao utaona kwamba  asili ya uovu hautoki kwa Mungu bali chanzo chake ni mwanadamu kutokana na maumbile yake ya kiroho au kimwili na hasa kutotii anachotaka Mungu, imemsababishia aingie kwenye hali hiyo ya uovu. Sasa tuchungulie mafundisho ya Kanisa Katoliki kupitia Neno la Mungu yanafundishi nini juu ya maovu:

Maovu hayatoki kwa Mungu

Mafundisho ya Kanisa Katoliki hutuambia kuwa Mungu ni Mwema kama tulivyokwisha kusikia katika utangulizi wetu. Yoyote yaliyoumbwa na Mungu ni mema: Nuru, mimea, wanyama, wanadamu na kazi yake ya kutawala juu ya viumbe, licha ya hayo mwanadamu hatakiwi kuishi peke yake. 

Juu ya mwanadamu aweza kuishi katika mahusiano na amani na Mungu, na duniani na nafasi yake mwenyewe. Kwa neno moja: Mungu ndiye anayetoa maisha kwa mwanadamu na hayo huonekana kwa kielelezo cha Paradisi. Kama ndivyo uovu unatoka wapi?

Maovu yanatoka kwa mwanadamu

Yampasa mwanadamu kupokea heri yake kwa hiari na kuijali hali yake akiwa kiumbe cha Mungu. Kwa sababu hiyo Mungu anampa mwongozo lakini mwanadamu hufuata ushauri wa shetani na kukataa na kuhukumu mwenyewe ni nini kinachofaa na nini kinachomdhuru.
Hapo hutokea dhambi na mapato ya dhambi hutokea uharibifu wa kila namna yaani aibu, hofu,  kuvunja mapatano na kukosa madaraka, ugomvi kati ya mume na mke, katika maisha ya ndoa na mwisho kufa kwa uchungu.

Maovu baada ya kuingia ulimwenguni kupitia dhambi ya mwanadamu, yalizidi zaidi na zaidi ya mwanadamu alipofukuzwa paradizini alipata kuwa mwuaji wa ndugu yake. Badala ya kumtunza ndugu yake anamwua. Mwishoni mwa kuumba: “Mungu akaona kila kitu alichofanya na tazama ni chema sana” (Mwa 1:31).

Lakini sababu ya dhambi au maovu yamezidi sana hata imeandikwa: “Mungu akaiona dunia na tazama imeharibika (Mwa 6:12). Ingawa waliadhibiwa vikali kwa ghar ika kuu, wanadamu walizidi kupotea tena wakijenga mnara wa Babeli na kuabudu miungu ya uwongo.

Tabia ya mwanadamu

Kama tulivyosikia huko nyuma kuwa Mungu aliumba dunia vizuri naye alitaka wanadamu waifurahie pamoja naye (Mwa 1:31, 1Tim 4:4, Ebr 4:4,10). Lakini kwa kuwa alimwumba mwanadamu awe kiumbe chenye wajibu na uhuru wa uamuzi wake mwenyewe, iliwezekana kwamba aliweza kuutumia uhuru wake vibaya.

Aliweza kuamua kufanya aliyoyajua kuwa hakutakiwa kuyafanya (Mwa 15-17). Ukamilifu wake ungetokana na kufanya uamuzi ambao ungekuwa sawa kufuatana na wajibu wake. Kujikana kungeonekana katika kukataa majaribu mabaya na hivyo kungeimarisha tabia ya nia yake (Ebr 5:8, 14). Mungu alitaka mwanadamu aishi katika uhusiano wa upendo pamoja naye na wanadamu wenzake.

Lakini mwanadamu asingeweza kupenda  kama asingekuwa huru. Kama angefanana mashine (kama vile roboti) angeweza kufanya yale tu ambayo mumbaji wake alimpangia kuyafanya lakini asingeliweza kupenda au kufurahia chochote.  Lakini kama vile uhuru unavyoweka uwezekano wa kujitoa kwa Mungu na kwa wema, vivyo  hivyo upo uwezekano wa kuasi na kufanya maovu. Maovu hayakuwa matokeo ya kazi ya uumbaji wa Mungu bali yalikuwa matokeo ya kut
umia uhuru vibaya kwa viumbe vyenye akili timamu na wajibu wao (Mwa 3:1-7, Yah 1:12-13).

Maisha katika ulimwengu ulioharibika

Mafundisho ya Kanisa Katoliki kwa kutumia Neno la Mungu yaani Biblia yanasema wazi yanapoongelea habari za Maovu. Mafundisho hayo hufafanuliwa kwa kutumia njia mbili zinazohusiana dhidi ya maovu. Kwanza mafundisho hayo ya Kanisa hutoa maelezo kwa maana ya maadili sawasawa na maelezo ambayo yameelezwa hapo juu ambapo uovu ni kinyume cha wema wa tabia (Mit 8:13, Yer 7:24, Mika 2:1, Mt 5:45, 15:13, 5:19).

Pili mafundisho hayo ya Kanisa kwa kutumia Biblia huongelea habari za maovu katika maana ya kawaida zaidi ambapo maovu huhusika na misiba, matatizo, maafa, bahati mbaya na hata mambo kama vile shida za mwili au matunda yaliyooza. Maana ya neno pia ni kinyume cha wema, lakini pasipo maana ya maadili (Kumb 7:15, 2Sam 15:14, Mt 7;17, LK 16:25). Lakini kuna uhusiano kati ya aina mbili za matumizi ya neno la maovu kwa kuwa maovu ya dhambi yaliingia ulimwenguni, maafa na misiba vimekuwa ni sehemu ya maisha ya ulimwenguni.

Agano la kale linaposema kwamba Mungu anatuma yote, yaani wema na uovu halina maana ya wema na uovu kwa maadili bali linasema habari za baraka na shida, Waisraeli wa wakati wa Agano la Kale walitambua utawala wa Mungu juu ya mambo yote ya maisha, yaani mambo mazuri na mabaya pia (Ayi 2:10, Isa 45:7). 

Waliona kwamba uovu na matatizo, maafa na uharibifu mara nyingi ulikuwa chombo cha Mungu cha kuadhibu watu waovu (Isam 16:15, Yer 35:17, Amos 3:6).

Hitimisho
Ingawa  kuingia kwa dhambi katika ulimwengu wa mwanadamu kulichafua makusudi ya Mungu kwa mwanadamu, uovu haukuweza kupindua au kuharibu makusudi yake. 

Mungu anaweza kukusudia wema kutokana na uovu (Mwa 50:20, Rum 8:28). Matatizo ya maisha si kila mara adhabu ya Mungu juu ya kosa fulani kwa kawaida Mungu haelezi kwa nini maovu yanatokea au kwa nini watu wanapatwa na maafa.
Lakini siku zote hutumia maovu yake  ili kuleta matokeo mema (Hab 1:13, 3:17, Lk 13:1-5, Yoh 9:2-3, 2Kor 12:7-9).

Lakini hili halitokei udhuru kwa watu wanaosababisha uovu (Isa 10:5-11, Yer 51:5-10,34-36, Mt 26:24, Mdo 2:23, Rum 3:8) labda Mungu hutumia hata mauti ili kutimiza makusudi yake kwa wema.
Kwa njia ya mauti ameshinda mauti na kuwaweka watu huru mbali na uovu (Ebr 2:14).
Kwa sababu ya kifo cha Kristo waumini wanaweza kufurahia ushindi juu ya uovu (Rum 6:7-11, 14, Gal 1:4). 

Watafurahia ushindi wa mwisho wakati  Kristo atakaporudi ili kuondoa uovu wote, na kuleta mbingu mpya na dunia mpya ya Mungu (1Kor 15:25-28, Ufu 21:4, 27, 22:1-2).


Post a Comment