Ads (728x90)

Powered by Blogger.


Na Mwandishi Wetu

Licha ya hatua  mbalimbali  zinazochukuliwa na serikali na wadau mbalimbali nchini, bado UKIMWI na Virusi Vya Ukimwi ni tishio hapa nchini. Takwimu kutoka mikoa mbalimbali nchini zinaonesha kuwa UKIMWI ni janga kwa kuwa kuna idadi kubwa ya watanzania wanaendelea kuathirika, wengine wanaugua na kufa hivyo kuathiri ustawi wa jamii kwa kuwa nguvukazi inapotea.

Mratibu wa UKIMWI na tiba katika Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma Felista Kibena amenema ya kwamba, zaidi ya watu 21,000 katika manispaa hiyo wanaishi na virusi vya UKIMWI. Kwa mujibu wa Kibena kati ya watu wenye virusi, watu zaidi ya 10,000 ndiyo wanaugua ugonjwa wa UKIMWI na kutumia dawa za kurefusha maisha za ARV na kwamba maambukizi ya virusi vya UKIMWI katika Manispaa ya hiyo ni asilimia nne.

Hata hivyo Takwimu zinaonesha kuwa Mkoa wa Ruvuma unashika nafasi ya tano kitaifa ukiwa na maambukizi ya asilimia saba ambapo Mkoa wa Njombe ndiyo unaongoza kitaifa ukiwa na asilimia  14.5, nafasi ya pili inashikwa na Mkoa wa Iringa, ikifuatiwa na Mkoa wa Mbeya katika nafasi ya tatu na Mkoa wa Rukwa ukiwa nafasi ya tano.

“Kiwango cha maambukizi katika Mkoa wa Ruvuma kinapanda kwa kasi awali kiwango cha maambukizi kilikuwa ni asilimia tano lakini sasa ni asilimia saba, tumevuka kiwango cha kitaifa ambacho ni asilimia tano’’, alisisitiza Kibena.

Alisema maambukizi makubwa ya virusi vya UKIMWI katika Manispaa hiyo, hivi sasa yanachangiwa na makundi maalum ambayo aliyataja kuwa ni watu wanaofanya ngono kinyume cha maumbile, watu wanaofanya biashara ya ngono, wafungwa na watumiaji wa dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano au kubwia.

Kibena alisema maambukizo ya virusi katika makundi maalum yamefikia asilimia 36 ambapo kila watu 100 watu 36 wana virusi vya UKIMWI ukilinganisha na kiwango cha kitaifa cha asilimia tano ambayo ni sawa na kila watu 100 watano wana virusi. Alizitaja kata ambazo zinaongoza kwa maambukizo ya virusi vya UKIMWI katika Manispaa ya Songea kuwa ni Bombambili, Mateka, Ruvuma na Lilambo.

Takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa hadi kufikia mwaka 2013 hapa nchini watu milioni moja na nusu walikuwa wanaishi na virusi ambapo kwa mwaka 2014 pekee hapa nchini watu 74,000 wameambukizwa virusi na zaidi ya watu laki tano walikuwa wanatumia dawa za ARV na kwamba  watu zaidi ya laki sita wanatumia ARV.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO)  watu milioni 35 wanaishi na virusi vya UKIMWI hadi kufikia mwaka 2013 kati yao  watu milioni 24 sawa na asilimia 71 walitoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara ambapo watu milioni moja na nusu wamekufa hadi kufikia mwaka 2013 na watu milioni 12 wanatumia dawa za ARV.

Utafiti umebaini kuwa matumizi ya dawa za kulevya hasa kwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 45 bado ni tatizo kubwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea. 

Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2015 Manispaa hiyo ilikuwa na Waathirika wa dawa za kulevya 145 kati ya hao Wanaume ni 138 na Wanawake ni saba hali ambayo inaongeza maambukizo mapya ya Virusi vya UKIMWI.

Katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Mei, 2016 Manispaa ya Songea ilikuwa na  jumla ya waathirika wa dawa za kulevya 97  kati yao Wanawake wawili na Wanaume  95 ambapo waathirika wote wakiwa na umri kati ya miaka 15 hadi 45. Kutokana na hali hiyo Mratibu wa UKIMWI na Tiba wa Manispaa hiyo alisisitiza kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya ili kujenga  jamii na maisha na utu wa mtu bila matumizi ya dawa za Kulevya.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2013 ya Shirika la Taarifa na Ushauri kuhusu ugonjwa wa Ukimwi duniani (Avert), Tanzania ilifanikiwa kupunguza maambukizi mapya ya ugonjwa huo kutoka asilimia 7.1 mpaka asilimia 5.1 huku Mkoa wa Njombe ukiwa  kinara  kwa kuwa na asilimia 14.8 ya maambukizi nchini.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa mwaka huo watu waliokuwa wanaishi na virusi vya Ukimwi nchini walikuwa Milioni 1.4 ambayo ni sawa na asilimia 6 ya watu wote wanaoishi na virusi vya Ukimwi kusini mwa Jangwa la Sahara.

Nchi zilizokuwa vinara kwa maambukizi kulingana na utafiti huo ni Botswana, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Swaziland, Zambia na Zimbabwe ambapo asilimia 10 ya wananchi  wa  nchi hizo walikuwa wameshaathirika.

Utafiti wa viashiria vya Virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI kwa mwaka 2011/2012 unaonesha maambukizi ya VVU kwa upande wa Tanzania Bara yapo kwa asilimia 5.3. takwimu hizo zimetolewa na Wiziri ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu.

Kwa mujibu wa takwimu hizo,wanawake ndiyo wameathirika zaidi na janga hili ikilinganishwa na wanaume ambapo asilimia 6.2 ni wanawake na asilimia 3.8 ni wanaume. 

Inakadiriwa kuwa kuna watu 1,538,382 wanaishi na VVU nchini Tanzania ambapo vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 ni asilimia 10.6 na watoto walio chini ya miaka 15 ni asilimia 11.8 ya watu wanaoishi na VVU nchini.

Hata hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamefanikiwa,Kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa watoto kutoka asilimia 26 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 4, 2015 ambapo juhudi zaidi zitawekezwa katika kuhamasisha ufuasi wa matumizi ya ARV kwa kina mama wajawazito na wanaonyonyesha.

Lengo la serikali kupitia Wizara ya Afya ni Kupanua wigo wa upatikanaji wa mashine za kupima wingi wa VVU mwilini (HIV Viral Load) sanjari na kupima chembe hai za damu aina ya CD4, hali ambayo itasababisha kufikia lengo la kupima asilimia 50 ya watu wote walio kwenye tiba kabla ya mwisho wa  mwaka  huu.


Post a Comment