Ads (728x90)

Powered by Blogger.




Hii hapa Historia ya Mpendwa wetu Bambu Gama.

Alizaliwa tarehe 27/01/1934 huko Fürth, Nurnberg, nchini Ujerumani. Alibatizwa kwa jina la Werner. Alikuwa mtoto pekee kwa wazazi wake Ludwig na Frederica.
Baba yake alifariki katika vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1943 na kusababisha Br. Polycarp kukosa malezi ya Baba katika utoto wake.

Baada ya kumaliza shule ya msingi, Br. Polycarp alisomea ufundi wa kunyoa na kutengeneza nywele mwaka 1947-1953.

Alifaulu sana katika fani hii na aliitumia vizuri katika maisha yake yote kutengeneza na kukata nywele za watawa wenzake huko Ulaya na hapa Peramiho.

Mara baada ya kumaliza mafunzo ya Fani ya kutengeneza nywele, alijisikia wito wa kumtumikia Mungu katika maisha ya Kitawa. Hivyo aliingia tarehe 30/08/1953 ambapo alipewa jina la Polycarp na kufunga nadhiri za muda za kitawa tarehe 27/09/1955.

Mwaka 1955-1957, Br. Polycarp alipelekwa katika shule ya uhunzi wa kufua vyuma (Usonara). Alifuzu mafunzo hayo vizuri. Kwa kutumia dhahabu aliweza kutengeneza au kukarabati vitu kama Kalisi, Pete, Chetezo nk.

Mwaka 1959 alifunga nadhiri za daima. Baada ya hapo kwa muda wa miaka 3, alifanya kazi mbalimbali katika Jumuiya yake ya münsterschwarzach. Pia alihudhuria mafunzo mafupi kuhusu Uongozi na mambo yahusuyo jamii (Sociology), hadi mwaka 1964.

Awamu ya pili ya maisha ya Br. Polycarp Utawani ilianza alipotumwa Misioni hapa Peramiho. Alipokea msalaba wa Kimisionari tarehe 08/03/1964.

Akiwa hapa Peramiho Br. Polycarp aliweza kutumia vipaji vyake vya Ufundi au Fani alizojifunza.
Hivyo bila bila kuchelewa baada ya kujifunza na kuzoea Lugha ya Kiswahili mwaka 1965 alianzisha karakana ya Usonara hapa Peramiho.

Alitengeneza na kukarabati vyombo vya Kanisani kama vile Kalisi, Siborio, Monstrance, Chetezo, Tabernakulo, Pete na vitu vingine vingi.

Punde Karakana hii ilipata umaarufu mkubwa kwa kupata wateja hapa nchini na hata katika nchi za Afrika Mashariki kwa ujumla.

Br. Polycarp hakuwa mchoyo katika ufundi wake. Hivyo mara aliwapata watu aliowashirikisha ufundi huu kwa kuwafundisha yeye mwenyewe, kiasi kwamba wanaweza kuendeleza kazi hiyo licha ya yeye mwenyewe kutokuwepo.

Licha ya ufundi huu Br. Polycarp alikuwa na vipaji vingi. Alikuwa mwimbaji wa mashairi. Vipaji hivyo alitumia kuleta uhai na uchangamfu katika Jumuiya yetu hasa tulipokuwa na sherehe zetu za ndani.

Kutokana na uchangamfu na vipaji vyake watawaVijana walimpenda sana. Alikuwa mwimbishaji wa Tenzi na Zaburi kwa Vijana walelewa.

Kwa Kipindi cha miaka kadhaa alisimamia na kuendesha kwa uweledi mkubwa Kiwanda chetu cha Uchapaji (Peramiho Printing Press)
Br. Polycarp hakuwa na mahusiano ya karibu na watawa tu, bali hata nje ya Uatwa alipendwa na wengi. Alijifunza na kuelewa Lugha ya Kiswahili kwa ufasaha.

Pia alijifunza Mila na Desturi za Kabila la Kingoni kwa kina. Aliweza kuzungumza Kingoni kwa ufasaha pengine kuwazidi hata Wangoni wenyewe.
Yeye mwenyewe alijiita Mngoni wa ukoo wa Gama. Alicheza ngoma za jadi na alianzisha Kikundi cha ngoma ya utamaduni iliyoitwa Likwamba.

Hakika Br. Polycarp OSB alikuwa kiunganishi kikubwa kati ya Abasia yetu na watu wa nje ya Abasia. Aliweza kuwazoea watu na hata kuwaelewa kwa muda mfupi. Mwenyewe alipenda kujiita "MLUGALUGA"
Kwa muda wa miaka mitatu, Br. Polycarp alielemewa sana na magonjwa kadhaa. Alishambuliwa hasa ana Saratani iliyoharibu sehemu ya uti wa mgongo.

Ugonjwa huu ulisababisha kupindika na kutoweza kusimama wima wala kutembea. Hivyo alishindwa kuyafanya yale aliyozoea kuyafanya wakati wa enzi wa afya yake nzuri. Muda mwingi alikaa akijisomea na hata kufanya kazi ndogo ndogo.

Br. Polycarp alishsiriki shughuli zote za Jumuiya bila kujali afya yake. Daima alikuwa wa kwanza kushika ratiba za Kitawa. Alikuwa wa kwanza kufika Kanisani katika vipindi vya Sala, Mezani, kwenye Mikutano, kwenye Mazoezi ya Kuimba nk.

Kuanzia Mwezi Novemba 2017, Br. Polycarp alishambuliwa pia na ugonjwa wa moyo, kisukari na kuenea sana kwa saratani na figo hivyo kutoweza kufanya kazi vizuri.

Licha ya maumivu makali aliyoyapata, aliweza kuyavumilia kwa Saburi bila malalamiko makubwa. Kila alipoulizwa kuhusu afya yake, alisema ni nzuri.

Naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru wale wote waliomsaidia Br. Polycarp katika ugonjwa na mateso yake kwa muda mrefu.

Najua ni wengi na itaniwia vigumu kuwataja kwa majina. Uliyeshiriki katika kumhudumia, kumfariji, kumwombea na kumsaidia Br. Polycarp naomba ujisikie kuwa nakushukuru kwa niaba ya Wanajumuiya wote wa Abasia ya Peramiho.

Nawashukuru Madaktari wa Hospitali ya Mtakatifu Joseph-Peramiho kwa kumhudumia kwa njia nyingi hasa kwa lengo la kuokoa maisha yeke.

Wauguzi wote wa Infirmary huko St. Scholastica pamoja na Masista wote. Watawa wote wa Abasia ya Peramiho ambao kwa muda mrefu walikuwa wanakesha naye usiku kumhudumia.

Kwa namna ya pekee naomba kumtaja kwa jina Bw. Kevin Gama (Matata) alikuwa kama Yaya kwake. Mungu amrudishie mara mia huduma aliyoitoa kwa Mzee wetu Br. Polycarp.

Br. Polycarp amefariki akiwa na miaka 84 ya kuzaliwa. Miaka 63 ya Utawa na miaka 54 ya Umisionari hapa Peramiho. Nguvu zake nyingi katika uhai wake alihudumia katika Kanisa la Songea na Tanzania akwa ujumla na hasa Abasia hii ya Peramiho. Tuna kila sababu ya kumshukuru.

Tunamshukuru sana Mungu kwa zawadi ya Br. Polycarp kuwa kati yetu kwa kipindi chote cha uhai wake. Tunaishukuru familia yake na marafiki zake waliomsaidia kwa hali na mali katika shughuli zake za misioni.

Pia tunaishukuru Abasia ya Münsterschwarzach kwa kumtuma hapa kwetu Peramiho.
Mwisho tukumbuke kwamba maisha yetu yapo mikononi mwa Mungu daima. Yeye ndiye Mwamuzi wa mwisho. Anajua mwisho wa maisha ya kila mmoja wetu na hata yataishia namna gani.
Kinachotakiwa kwetu ni kukesha kwani Bwana wetu Yesu Kristo anatuambia "Kesheni basi kwani hamjui siku wala Saa" Mt. 25:13.

Tumkumbuke ndugu yetu Br. Polycarp Stich OSB katika Sala zetu naye pia atatuombea.
Roho ya ndugu yetu Br. Polycarp (Bambu Gama) ipate rehema kwa Mungu na ipumzike kwa amani. Amina.

Imeandaliwa na Priori Msimamizi na Watawa wa Abasia ya Peramiho.


Post a Comment