Ads (728x90)

Powered by Blogger.


Kijana Mfaume ambaye sasa ni marehemu enzi za uhai wake alibahatika kuwa na kazi nzuri kabla ya kuoa. Baada ya kuoa miaka mitano ya kwanza akabahatika kuwa na watoto mapacha wa kike na wa kiume na mke wake aliishi kwa furaha akifurahia baraka ambazo Mungu aliwapa katika familia yao.

Mke hakuwa na kazi na mume akaona ni vyema amsaidie kwa kumsajilia kampuni na mama yule akawa na kampuni ya usafirishaji na ikafana sana na kupata umaarufu katika eneo lile.

Miaka michache baadae mume akapatwa na matatizo kazini na kusimamishwa kazi na kwa kuwa alikuwa Wakili basi na leseni yake ya uwakili ikafungiwa na hakutakiwa kufanya kazi yoyote.
Mpango huo ulisukwa na wenzake pale kazini kwa kuwa alisifiwa sana kwa utendaji wa kazi zake na kupinga vitendo vya rushwa.

Maisha yakazidi kuwa mabaya pale nyumbani kwani miaka ilivyosogea hakupata tena wala kuliona lile penzi la mkewe, kwani mke akawa ni mtu wa kumchukia mumewe mara mume akihitaji fedha apewe kwa masimango na mbaya zaidi hata watoto wakaanza kufundishwa na mama yao kumchukia baba yao.

Hali ile ilimpa mzee yule wakati mgumu na ikafikia kipindi akaanza kudhohofika mwili kwa mawazo ingawa akajitahidi sana kutoyaonyesha hayo machoni pa watu na majirani.

Baada ya muda akapatwa na homa na akawa akijiuguza lakini baada ya muda akashauriwa aende akapimwe na kugundulika kuwa alikuwa na tatizo katika moyo wake lililosababishwa na msongamano wa mawazo.

Akamfuata mkewe ofisini kwake na kumwambia ana tatizo la moyo na ilihitajika apate msaada wa fedha kiasi cha laki tano (500,000) kwa thamani ya fedha za kitanzania ili afanyiwe upasuaji wa haraka na kujiokoa katika hali hiyo hatarishi kwa maisha yake.
Mke alimjibu, " Sidhani kama nina hela ya kuchezea kwa kukupa mwanaume usiye na faida kwa familia yako, Wanaume wenzako wanafanya kazi na sio kama wewe ulivyo sasa"

Baba alinyanyuka na kuufuata mlango bila ya kusema neno machozi yakimtoka na akikumbuka jinsi alivyoijenga familia yake kwa upendo na amani akiwapa mahitaji yote na jinsi alivyotumia mpaka tone lake la mwisho la fedha, muda na hata jasho kuinyanyua biashara ya mkewe ambayo ni kwa ajili ya familia.
Akawasha gari na kuondoka kuelekea nyumbani akiwa na mawazo huku akiona jinsi mtu umpendaye anavyoweza kubadilika kiasi cha kukuombea ufe kwa kuwa ni kero kisa huna kazi..

Huku nyuma mke akaingiwa na roho ya ubinadamu na kujilaumu kwa kauli ile na kuanza kuumia kisha akajaribu kumpigia simu Mzee yule (Mumewe) ikawa haipokelewi na kumua kuliwasha gari lake na kuanza kumfuata mumewe.

Kilomita chache mbele akaona kuna mkusanyiko mkubwa wa watu akapaki gari na kuuliza kuna nini? wakamwambia kuna ajali ya gari kuna mzee alikuwa anataka kuingia upande wa kushoto bila kuona kama kuna gari.

Kusogea pale hakuamini kuona mwili wa mume wake ukiwa umefunikwa alianza kutokwa na machozi kabla ya kuingia kwenye gari na kuona kuna kadi nzuri ikiwa kwenye bahasha akaifungua na kuisoma.

Kilio kikubwa kilimtoka baada ya kugundua kuwa siku hiyo ilikuwa ni siku za kuzaliwa ya baba huyo na hakuna aliyekumbuka zaidi ya yeye mzee kununua kadi iliyoandkiwa " NAKUSHUKURU MUNGU KWA KUNIFIKISHA MWAKA HUU MPYA PAMOJA NA CHANGAMOTO NINAZOZIPITIA NAAMINI KUNA SOMO WATAKA KUIPA JAMII KUPITIA MIMI. JAZKAALLAH HERI….. "HAPPY BIRTH DAY TO ME"
Mama yule aliomboleza na mpaka sasa anazidi kuomboleza na hana amani tena hata faida ya ile biashara haioni tena na hajui nani atamsamehe.

TUTAFAKARI
1. Je unapitia mapito gani sasa katika mahusiano yako?
2. Je unayamudu vipi matatizo ya mahusiano yako?
3. Je unafikiria nini kama siku ukiamka na kuona wewe ndio chanzo cha kifo, kilema au chanzo cha msongamano wa mawazo kwa mwenza wako kutokana na tabia zako za ubinafsi?

MUHIMU

Ndugu una kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kukupa mwenza wako wa maisha, ni jambo jema kuamini kuwa katika kila mnalolipitia ni jaribu la kuwafanya muwe na sababu ya kuonyeshana upendo mwema zaidi ya ule wa mwanzo.
Yatafakari mahusiano yako kwa sasa. Jiulize, una nafasi gani kwa mwenza wako? Ujumbe huu uwape matumani wote walio katika migogoro ya mapenzi na wapendane kwani hakuna hali mbaya inayodumu zaidi ya kuwa mapito tu ya Dunia.
Kuweni na Siku njema.......


Post a Comment