Familia nyingi duniani husubiri kwa
hamu kubwa usiku wa kuamkia Mwaka Mpya. Usiku huo watu hujikusanya katika
maeneo tofauti huku wakiimba nyimbo mbali mbali za kufurahia kuona mwaka
mwingine, hata wale ambao kwa kipindi cha mwaka mzima walikuwa mbali na Mungu
husikika wakilitaja jina lake kwa heshima kubwa.
Katika orodha ya sherehe maarufu dunia, moja wapo ni
sherehe ya mwaka mpya. Gazeti pendwa la Mwenge linakuletea asili ya mwaka mpya
na mkanganyiko wa kimahesabu uliopelekea miaka sita kupungua.
Maadhimisho ya kwanza ya sherehe za Mwaka Mpya
yalishuhudiwa huko Mesopotamia miaka 2018 iliyopita. Ilisherehekewa na Wamisri,
Waajemi na Wafoeniki katika zama za Equinox katikati ya mwezi Machi, Wayunani
walisherehekea katika kipindi cha majira ya baridi. Kwa mujibu wa kalenda ya
kale ya Kirumi Mwaka Mpya uliangukia Machi 1, Kalenda hiyo ilikuwa na miezi
kumi tu na Machi ilikuwa mwezi wa kwanza wa mwaka. Kalenda hii asili yake ni
mzunguko wa mwezi, ikianzia majira ya kuchipua na kumalizia na majira ya vuli.
Numa Pompilius, mfalme wa pili wa Roma ndiye aliyeugawa
mwaka katika miezi kumi na mbili ya mzunguko wa jua na kuongeza miezi ya
Januari na Februari. Mwaka Mpya ukabadilishwa na kuwa Januari kutokana na mwezi
huo kusadifu mwanzo wa miaka ya kiraia huko Roma.
Kaizari wa Roma Julius Caesar alitangaza rasmi kuwa
Januari mosi ndio mwaka mpya ilikuwa mwaka 46 B.C. Warumi walikuwa wakimwabudu
Mungu Janus ambaye alikuwa na nyuso mbili, moja ikiangalia mbele na nyingine
ikiangalia nyuma. Mwezi wa Januari ulipewa jina la Mungu huyo wa Kirumi na
kumpa Kaisari wazo la kuanzisha Januari kama mlango na Mwaka Mpya.
Inasemekana kuwa Kaisari aliisherehekea Januari mosi, kama
mwaka mpya kwa kuamuru majeshi ya mapinduzi ya Wayahudi kurudi nyuma.
Waliadhimisha mwanzo wa mwaka kwa kurejesha sheria za zamani kabla ya amani
kuenea. Watu wakajua kuwa Januari ndiyo mwezi wa kwanza wa mwaka.
Katika kipindi cha
zama za kati, sikukuu za Kipagani zilipewa umuhimu mkubwa na Machi 25
ilitangazwa kama mwanzo wa Mwaka Mpya. Machi 25 iliitwa kuwa ni Siku ya Kupashwa habari Bikira Maria na
Gabrieli kwamba atamzaa Yesu Kristo (Annunciation Day). Baadaye, Malkia wa
Uingereza alitangaza kuwa tarehe 25 Disemba, yaani siku aliyozaliwa Yesu lazima
iadhimishwe kama Mwaka Mpya.
Takriban miaka 500 baadaye, Papa Gregory XIII aliipiga
marufuku kalenda ya zamani ya Julian na kuanzisha kalenda ya Gregori ambayo
ilijumuisha mwaka mrefu wenye siku 366 ambao mwezi wa Februari unakuwa na siku
29 na 28 ili kuleta uwiano kati ya
misimu na kalenda. Hatimaye, mnamo mwaka 1582, kalenda ya Gregori ilianzishwa
na kusherehekea Mwaka Mpya, siku ya kwanza ya Januari.
Yesu alizaliwa katika Betrehemu mwaka 6 au 7 kabla ya
Kristo (BC), tunaweza kueleza kwa urahisi kwamba wakati alipozaliwa watu
walihesabu miaka yao kutoka mwanzo wa mji wa Roma. Lakini Mtawa Dionyius Exiquus, alianza kuhesabu miaka toka
alipozaliwa Yesu na ukaitwa Mwaka wa Kwanza, kadiri ya hesabu za kuzaliwa kwake
toka Roma ni miaka 754.
Kadiri ya Mt.2 tunaona ya kwamba Yesu alikuwa na miaka 2-3
wakati alipokufa. Mfalme Herode naye alikufa mwaka wa nne kabla ya Kristo (BC)
Hata hivyo maelezo ya Biblia yanaonesha kwamba Mtawa
Dionysius Exiquus ambaye alipewa jukumu la kufanya mahesabu ya miaka, kuna makosa aliyafanya katika
mahesabu ambapo alisahau kuhesabia kati ya miaka 6 au 7 ( The Results of false
Calculations), makosa ambayo inaelezwa yalifanyika kwenye karne ya sita, kwa kuwa inakadiliwa Yesu alizaliwa
kati kati ya 7BC na 2BC.
Mtawa Dionysius
Exiquus alizaliwa 470 C.AD huko Scythia Mashariki mwa milki ya Roman na
alifariki dunia 544 AD Roma, Italy. Kutoka na mkanganyiko huu, kwa kuzingatia
maelezo ya kitabu kitakatifu cha Mwenyenzi Mungu yaani Biblia, ni wazi kwamba
Miaka 6 ilisahaulika, hivyo 2018 tukiongeza miaka 6 jumla yake tunapata miaka
2024.
Basi kila mmoja wetu anaweza akaongezea lakini ni ngumu
kubadiri hesabu ya sasa ya 2018 kwa kuwa imeshakubarika na inatumiwa na
wanadamu wote licha ya kwamba katika uislamu wanamfumo wao tofauti wa jinsi ya
kuhesabu miaka yao.
Mwaka mpya wa kiislamu ambao unafupishwa kama H au
Hijriyyah, tarehe 01 Muharram H ilikuwa ni sawa na tarehe 16 Julai 622 M. Na
inatamburika hivyo mpaka leo. Historia inasema miaka ya kiislamu imeanza
kuhesabika baada ya Maswahaba kuhama kutoka Makkah kwenda Madiynah, lakini
mfumo uliokubarika kimataifa wa kuhesabu miaka ni huu wa baada ya Yesu Kristo
kuzaliwa.
Mwaka 2018 umeanza na sisi sote bado tuna kamba mguuni,
nikiwa na maana ya ugeni wetu katika mwaka huu, inatupasa kutafakari kwa kina
kihusu wajibu wetu wa hapa duniani jinsi tutakavyoingia mbinguni kwa lengo la
kuurithi ufalme wa Mungu.
Hakuna marefu yasiyokuwa na ncha, ndio maana kila baada ya
mienzi 12 tunasherekea mwaka mpya. Hata maisha yetu yanaukomo vile vile, lazima tusali na kumwomba Mwenyezi Mungu
daima, kwa kuwa hatujui muda wala saa pale mwana wa Adam atakapokuja
kutuchukua, Amina!
Post a Comment