Ads (728x90)

Powered by Blogger.


Ni majira ya saa kumi na mbili jioni, Bwana Victor Ndomba anafunga duka lake la nguo lililopo mkabala na Soko Kuu la Songea, baada ya kumaliza kufunga anatoka nje ya duka lake na anawaaga mafundi kushona ambao wanafanyia shughuli zao nje ya duka lake, wao wanaendelea na kazi zao katika jitihada za kukamilisha kazi za wateja wao hususani sare za shule katika kipindi hiki cha kuanza kwa mwaka mpya wa masomo kwa wanafunzi wa msingi na sekondari.


Baada ya kuagana na majirani zake wengine anaingia kwenye gari yake Toyota Harrier aliyoinunua miezi michache iliyopita, anaiwasha na kisha safari ya kuelekea nyumbani kwake maeneo ya Msamala jirani na Shule ya Sekondari ya Kutwa Msamala inaanza kwa mwendo wa wastani.

Dakika kumi baadaye, Bwana Victor anawasili nyumbani, anapiga honi na haraka haraka kijana Rashidi ambaye ni msaidizi wa shughuli za nyumbani zikiwemo utunzaji wa mifugo na bustani ya maua anaelekea getini na kulifungua, Bwana Victor anaingia na kuegesha gari katika eneo lililotengwa maalum kwa ajili ya kuegesha magari.

Na taratibu anapiga hatua kuelekea ndani, ile anaingia tu sebuleni analakiwa na watoto wake wapenzi Valeria na Ivan ambao kutokana na umri wao kuwa mdogo wao hawako shuleni kama walivyo kaka zao James na Humphrey, “Wooow, woow baba” wanamrukia baba yao naye anawapokea kwa kuwabusu na kuwakumbatia wote kwa pamoja....Mara baada ya kuketi sebuleni, mkewe Jennifer, anafika sebuleni akitokea chumbani alikokua amejipumzisha, wanasalimiana na kisha Victor anaingia chumbani kubadilisha nguo huku akiwaacha mkewe na wanawe wakiangalia maraudio ya Tamthiliya iliyowahi kurushwa kitambo kidogo ikifahamika kama “Secreto de Amore”

Akiwa chumbani, Bwana Victor anajilaza kitandani huku akijaribu kuyatafakari maisha yake aliyoyapitia, hatimaye anaishia tu kusema “Mwache Mungu aitwe Mungu.

.....Ni hivi, Bwana Victor, yeye ni mtoto wa kwanza kati ya watoto wa nne katika familia ya Mzee Ndomba aliyehamia kijijini Mlete baada ya kupata uhamisho wa kikazi akiwa kama Mwalimu wa Shule ya Msingi, Kwa mantiki hiyo Bwana Victor anao wadogo zake watatu wote wa kiume.
Bahati mbaya ni kwamba Victor hakuwa mwanafunzi hodari darasani na hivyo hakuweza kuendelea sana katika elimu, aliishia kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Namabengo, hii ni baada ya kufeli mara mbili mtihani wa mchujo wa kuendelea kidato cha tatu. Kutokana na hali hiyo, Victor alilazimika kurejea nyumbani ambako baba yake Mzee Ndomba alikataa katakata kumwendeleza katika fani nyingine yeyote, hivyo akabaki nyumbani akifanya shughuli mbalimabali hususani kutunza ng’ombe wa baba yake na kuuza maziwa mjini Songea.

Hao wadogo zake wengine watatu walifika mbali sana kitaaluma kwani wote walihitimu Chuo Kikuu katika fani mbalimbali, hivyo wakaja kuwa ni watu wenye ajira nzuri na maisha mazuri pia.
Bahati mbaya ni kwamba hao wadogo zake walichukulia kushindwa kuendelea kimasomo kwa kaka yao kama ni uzembe hivyo wala hawakumjali kwa lolote na zaidi ya yote waliishia tu kumdharau hata pale alipokuwa akikwama kiuchumi na kuwaomba msaada walipiga chenga kumsaidia.
Hali hii ilimuuma sana kwa Victor, maumivu hayo yalimfanya aweke dhamira ya kujituma sana katika shughuli zake hizohizo ndogo ndogo ili na yeye aweze kufanikiwa tena hata kuwazidi wadogo zake ambao tayari walijiona wamekwisha yapatia maisha.
*********
Miaka ilienda kasi sana huku Bwana Victor akizidi kujikita katika shughuli za kilimo na ufugaji, sasa hakuwa akihudumia mifugo ya baba yake tena bali alikuwa amepatiwa mgao wake wa majike wawili wa maziwa hii ni baada ya Mzee Ndomba kufurahishwa na kazi nzuri ambayo Victor alikuwa amemfanyia lakini pia Mzee Ndomba alilazimika kumgawia ng’ombe mwanaye kwa kuwa Victor tayari alikuwa amekwisha oa na hivyo alihitaji kuwa huru katika kufanya mambo yake.
Hivyo Victor aliendelea na shughuli za uuzaji wa maziwa ya ng’ombe wake huku baba yake akiwa amemtafuta kijana mwingine wa kusimamia mashamba na mifugo. Mmoja kati ya wateja wakubwa wa Bwana Victor, alikuwa ni mfanyabiashara mmoja wa kihindi Bwana Rakesh Patel aliyekuwa akimiliki maduka kadhaa ya nguo katikati ya Mji wa Songea.

Katika hali isiyo ya kawaida kwa wafanyabiashara wa jamii ya Kihindi, Bwana Patel alitokea kumpenda sana Victor kutokana na unadhifu wake wa mavazi na vifaa vyake vya kubebea maziwa lakini pia kutokana na tabia yake ya ucheshi, kujituma na kuzingatia muda. Moyoni mwake Bwana Patel alipanga kumfanyia jambo moja kubwa Bwana Victor lakini kabla ya kumfanyia jambo hilo ilikuwa lazima ampe kwanza mtihani.

Siku moja asubuhi wakati Victor alipomaliza kumpimia maziwa mfanyakazi wa ndani wa Bwana Patel na kutaka kupanda baiskeli yake na kuondoka alishtushwa alipoambiwa kuwa anaitwa na Mzee Patel ndani sebuleni.....! Victor alipigwa na butwaa kubwa....! lakini kwa woga akaingi sebuleni.
Baada ya mazungumzo ya dakika kadhaa...! bila kusita Victor anaridhia ombi la Bwana Patel la kumsaidia kuuza moja ya maduka yake yaliyoko pale mjini. Ili kutimiza kazi yake vizuri Victor akamtafuta kijana wa kumkabidhi kazi zake za maziwa na kisha yeye, mkewe Jennifer na mtoto wao wa Kwanza James, wanahamia mjini katika nyumba waliyotafutiwa na Bwana Patel tayari kwa kuanza maisha mapya.

Siku zilizidi kusonga kwa kasi, hatimaye miaka minne ilipita tangu Bwana Victor awe mfanyakazi wa Bwana Patel, Victor aliifanya kazi yake kwa moyo na kujituma na kwa kuzingatia uaminifu uliotukuka, kitu ambacho kilizidi kumfurahisha sana Bwana Patel kwani tangu aanze kufanya kazi na vijana wa kitanzania, Victor alikuwa ni kijana wa pekee mno ambaye aliifanya kazi yake kwa uaminifu pasipo kudokoadokoa mali wala fedha, hii ilimfanya sasa Bwana Patel amuongezee majukumu mengine Bwana Victor, sasa akawa ni msimamizi wa maduka matatu ya Bwana Patel ambayo yapo jirani, maisha ya bwana Victor yalianza kubadilika na sasa hata wale wadogo zake wakaanza kumtafuta kwenye simu tofauti na pale mwanzo kwani walipata taarifa kuwa ndugu yao sasa amekuwa Meneja wa maduka kadhaa akiwa amepatiwa nyumba na usafiri wake binafsi.

......Licha ya kuwa na maduka mjini Songea, Bwana Patel kumbe alikuwa akimiliki maduka mengine ya jumla jijini Dar-es-salam na bahati nzuri ni kwamba biashara ilikuwa imekuwa kwa kasi kubwa sana hivyo akahitaji kuwepo na kuishi jijini Dar-es-salaam ili aweze kufanya usimamizi wa karibu kwa kushirikiana na watoto wake watatu ambao walikuwa wakiishi huko, Hivyo basi Bwana Patel akalazimika kuuza mali za maduka yake manne yaliyopo Mjini Songea na kulibakisha moja tu ambalo alilikabidhi kwa Bwana Victor, ambaye alitakiwa kuendesha bisahara kwa muda wa mwaka mmoja na kuhakikisha anazalisha duka jingine lenye thamani ya lile aliloachiwa na akifanikiwa kufanya hivyo basi angeachiwa jumla lile duka la awali.

Hiyo ilikuwa ni fursa adhimu na adimu kwa Bwana Victor wala hakufanya makosa na ndani ya mwaka mmoja na miezi miwili alikuwa ameshazalisha duka jingine na hivyo rasmi akakabidhiwa duka lake, Sasa Victor hakuwa tena mwajiriwa bali mmiliki halali wa duka lile baada ya makabidhiano ya kisheria kufanyika. Hivyo ndivyo maisha ya Bwana Victor Ndomba yaivyobadilika.
........Mwisho.......


Post a Comment