Na Albano Midelo
Mafunzo
ya Ufundi Stadi VETA Songea yalianza kutolewa mwaka 1984 kwa
kutumia majengo yaliokuwepo katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo Matarawe
Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Katika kipindi hicho chuo kilikuwa na
uwezo wa kutoa mafunzo kwa wanafunzi 60
tu katika fani tatu ambazo ni ufundi magari, ujenzi na useremala.
Mkuu wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi VETA Songea Gideon Ole Lairumbe anasema ujenzi wa majengo ya kudumu
ya chuo hicho katika eneo la Msamala Manispaa ya Songea ulianza mwaka 2003 na
kukamilika mwaka 2005.
Lairumbe anabainisha kuwa ujenzi huo
ulijumuisha karakana tisa za mafunzo, jengo la utawala, maktaba, madarasa,
jengo la maliwato, uzio na chumba cha mitambo ya umeme.
Anabainisha kuwa katika ujenzi huo
zaidi ya sh.bilioni 1.654 zilitumika kati ya fedha hizo, ujenzi wa majengo
zilitumika zaidi ya sh.milioni 975, Mshauri elekezi zaidi ya sh.milioni 86.45
na ununuzi wa mitambo na vifaa vya mafunzo zilitumika zaidi ya sh.milioni 592.
Anasema baada ya ujenzi wa chuo hicho
kukamilika, uwezo wa kudahili wanafunzi katika chuo umeongezeka toka wanafunzi
60 hadi 250 kwa mwaka.
Hata hivyo Mkuu huyo wa chuo
anabainisha kuwa hadi kufikia mwaka 2017
chuo hicho kina wanachuo 646 kati yao wanachuo wanaosomea hatua ya kwanza
(level one) wanaume 253 na wanawake 88, wanaosomea hatua ya pili wanaume ni 176
na wanawake 67 na wanaosomea hatua ya tatu wanaume ni 55 na wanawake saba.
“Chuo kinatoa mafunzo ya muda mrefu
na muda mfupi, kwa kozi za muda mrefu mafunzo yanayotolewa ni katika fani za
ufundi magari, uungaji vyuma, umeme wa magari, umeme wa majumba, useremala,
uashi, ufundi bomba, ushonaji na uhazili na kompyta’’, anasema Lairumbe.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo hadi sasa wanafunzi
ambao wanaendelea na mafunzo ya muda mrefu ni 591 na kwamba chuo hicho bado
kinaendelea kupokea wanafunzi wa mwaka wa kwanza na kwamba mafunzo yanatolewa
katika awamu mbili tofauti asubuhi na mchana.
Mkuu huyo wa Chuo anayataja mafunzo
ya muda mfupi yanayotolewa na VETA
Songea kuwa ni fani za udereva wa magari daraja D, udereva wa magari ya abiria
na uhazili.
Fani nyingine ni ukarabati wa
kompyuta, utumiaji wa kompyuta, umeme wa majumba, umeme wa jua,
ulimbwende(cosmetology), utengenezaji wa dawa za usafi, sabuni za maji, upishi
na utengenezaji wa batiki na ujasirimali.
Takwimu zinaonesha kuwa tangu
kuanzishwa kwa chuo hicho hadi kufikia mwaka 2016 wahitimu wa mafunzo ya muda
mfupi ni 3013 kati yao wasichana 523 na wavulana 2490.
Miongoni mwa walionufaika na VETA
Songea ni wahitimu wa kwanza 20 wa fani ya ushonaji ambao walikabidhiwa vifaa
vya ushonaji vyenye thamani ya
sh.milioni 10 kwa ajili ya kuwajengea
uwezo wahitimu wa fani ya ushonaji kabla ya
hawajaingia rasmi kwenye soko la ajira.
“Chuo kiliamua kuanza na fani ya
ushonaji kuwapa motisha ya vifaa kutokana na uzoefu kuonesha kuwa wanaojiunga
na fani hii wengi ni wanafunzi wa kike ambao pi waathirika zaidi wa ukosefu wa
ajira nchini’’, anasema Mkuu wa Chuo.
Anasema kuwa chuo hicho kimefanikiwa
kupata jengo jipya ambalo linajumuisha maabara za Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano(TEHAMA), madarasa na ofisi za walimu.
Sanjari na ufundishaji wa kozi fupi,
Mkuu huyo wa chuo anasema chuo kinafundisha kozi fupi za udereva wa pikipiki,
udereva wa magari, utengenezaji wa
sabuni na batiki na kwamba lengo ni kuwafikia wahitaji wote mahali
walipo ili kupunguza changamoto ya ajira.
Licha ya kutoa kozi hizo katika
Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Mkuu wa Chuo hicho anasema, VETA Songea pia
imefanikiwa kufundisha kozi hizo katika wilaya za Njombe, Ludewa na Makete
mkoani Njombe.
“Chuo pia kinatoa mafunzo kwa
kushirikiana na viwanda na maeneo mbalimbali ya kazi, lengo likiwa ni
kuwajengea uwezo zaidi wafanyakazi viwandani ili kuongeza tija’’, anasema
Lairumbe.
Anasema VETA Songea inashirikiana na
viwanda na kampuni mbalimbali zikiwemo UNILEVER ambayo ni kampuni ya kiwanda
cha chai, Kampuni ya MANTRA ya mgodi wa uranium na kampuni ya Food Security
ambayo wafanyakazi wake 31 wamepata mafunzo ya muda mfupi kupitia VETA.
Anayataja matarajio ya chuo hicho
kuwa ni kuanzisha fani ya uandaaji wa vyakula (Food Production), utengenezaji
wa vifaa vya kilimo(Agro Mechanics) na kozi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano(TEHAMA).
Anatoa rai kwa serikali na wadau
wengine kuiangalia VETA kama mkombozi wa ajira kwa vijana hasa katika kipindi
hiki ambacho Tanzania na Dunia nzima inakabiliwa na janga la ukosefu wa ajira
ambapo vijana ndiyo waathirika wakuu.
Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda
wakati anafungua chuo cha VETA Songea mwaka 2013, pamoja na mambo mengine
aliagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kusaidia kuongeza nafasi za
mafunzo katika vyuo vya VETA ili vijana wengi wanaomaliza shule za msingi na
sekondari waweze kupata nafasi ya kujifunza kozi mbalimbali ambazo zitawawezesha
kuajiriwa na kujiajiri.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya anasema kwa kutambua umuhimu wa elimu ya
mafunzo ya ufundi stadi, serikali inaendelea kujenga vyuo vipya vya VETA katika
mikoa na wilaya mbalimbali nchini.
Mhandisi Manyanya anasisitiza kuwa
serikali itaendelea kusimamia mafunzo ya ufundi stadi nchini kama
yalivyoelekezwa katika sera ili kusaidia kukuza uchumi kupitia mafunzo ya VETA
huku uhamasishaji zaidi ukiwekwa katika ubunifu na ujasiriamali.
Post a Comment