Ads (728x90)

Powered by Blogger.






Chuo cha Ufundi Peramiho ni miongoni mwa vyuo vikongwe hapa nchini na kinasifika kwa kuzalisha wafanyakazi bora, wanaofanya kazi za ufundi katika maeneo mengi hapa Tanzania.

Chuo hicho kinachomilikiwa  na Watawa wa Mtakatifu Otilia waitwao Benedictine Fathers Peramiho  ambao walifika Tanzania Karne ya 19 ambapo Septemba 25, 1928 walifanikiwa kuanzisha chuo hicho katika Ardhi ya Peramiho, Songea. Novemba 17, 2017. Chuo cha ufundi Peramiho kiliazimisha mahafali ya 86 huku mahafali ya kwanza ikifanyika mwaka 1931.

Jumla ya wanafunzi 46 wameshiriki mahafali ya mwaka huu wakiwemo wanafunzi 10 kutoka Chipole, yaliyofanyika katika ukumbi wa Posta ingawa kwa bahati mbaya wanafunzi  wapatao 08, wameshindwa kuhitimu kwa matatizo mbali mbali ikiwemo utovu wa nidhamu, ada pia kutofikia wastani wa Chuo katika mitihani yao.

Wanafunzi hao ambao walianza masomo yao mwaka 2014 huku wawili wakianza mwaka 2015, wamesomea fani za Umeme, Ushonaji, Mabomba, Ufundi Magari na Useremala. Chuo cha Ufundi Peramiho, kimebakiwa na miaka 11 ili kusherekea mahafali ya 100 na kutimiza karne, suala ambalo litakuwa ni historia ya pekee kuandikwa katika ardhi ya Tanzania na mkoa wa Ruvuma, lakini kwa kipindi cha miaka Nane toka yalipofanyika Mahafali ya 79 mwaka 2010, Chuo kimepiga hatua kwa kiasi kikubwa katika vitu mbali mbali.

Mikakati iliyowekwa mwaka 2010 ni pamoja na kuanzisha fani mpya, kozi fupi fupi kwa (Driving school), kuwaendeleza wakufunzi pamoja  na kukarabati majengo ya Mruma Center kama Bweni kwa wasichana,  mikakati ambayo imefanyiwa kazi kwa zaidi ya 79% ambapo mkakati ambao haujaboreka kwa asilimia zote ni upande wa Magari (Driving School) bado unafanya upembuzi yakinifu ili kupata mkufunzi mwenye ujuzi stahiki ambaye atasimamia zoezi hilo.

Changamoto za sasa kwa Chuo ni uhaba wa vitabu ya kiada na ziada, kukosekana kwa maktaba, upungufu wa walimu wenye sifa, kukosekana kwa vifaa vya kisasa pamoja na Safari mbali mbali za kimasomo (Stadi Tour).

Wahitimu wa mwaka huu (2017), katika risala yao wamependekeza kwamba uongozi wa juu wa Chuo ujitahidi kufanyia kazi Changamoto zinazokikabiri Chuo hicho ikiwemo ukosefu wa Safari za Mafunzo ya Vitendo ili kupata uzoefu na ujuzi wa kutosha toka katika maeneo mengine.

Mkuu wa chuo, Bro.Augustine Mbilinyi OSB alikiri kuwa wahitimu wa mwaka huu wamefaulu mitihani yao ya ngazi ya pili (level 2) kwa kiwango cha juu katika mfumo mpya ambao walianza nao wa CBA (Competence based on assessment) kabla ya hapo ulikuwa ukitumika mfumo wa CBET (Competence based on education and training).

“Mfumo wa sasa una masomo mengi na unahitaji walimu wa Diploma lakini licha ya uhaba wa walimu tumeukabiri na tupo kwenye mikakati ya kuajiri walimu wengine wenye Diploma”.
“Ubora wa chakula unategemea sana mpishi, aina ya chakula na kufaa kwake kwa afya ya walaji. Nawaomba wahitimu wakawe mafundi bora na sio bora mafundi, tumewafundisha tabia nzuri na ufundi, vyote hivyo ni silaha katika maisha yenu”.

“Pia chuo chetu kinategemea zaidi wafadhili toka nje, suala ambalo ni hatari kwa siku za usoni kwa kuwa haitolewi kama mwanzo, tumeanzisha miradi kama kufuga Nguruwe, kupanda maparachichi (miti 150) na vingine vingi ili kujijengea uwezo wa kujitegemea. Kwa sasa bado tunahitaji msaada wa hali na mali ili tuweze kusonga mbele” alisisitiza Mbilinyi.

Naye Priori Msimamizi Sylvanus Kessy wa Abasia ya Peramiho, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo ya 86, alisema dunia ya sasa imegubikwa na maovu, kwa kuwa watu wengi wamekosa hofu ya Mungu; hivyo wahitimu hao wanatakiwa  kumtii Mungu ili kuendeleza ujuzi walioupata kwa hoja ya kupita njia ya wema.

“Maadili mema ni kitu kizuri, tuache kuiga tamaduni za ajabu zisizokuwa za kwetu; watu wasivae heleni, kujichora michoro ya ajabu n.k. pasipo kujua maana zake” alisema Priori Kessy. 

Kuhusu mapendekezo ambayo wahitimu hao waliyaainisha kwenye risala, alisema yote atayafanyia kazi kwa kiasi kikubwa kwa kushirikiana na  Mkuu wa Chuo hicho. 

Katika ujenzi wa jamii mpya ya kizazi cha Peramiho hasa katika Chuo cha ufundi, kwa lengo la kulinda heshima iliyojengwa na Mababu wa chuo hicho toka mwaka 1928 na Watawa wa Mtakatifu Otilia wanaoitwa Benedictine Fathers Peramiho ambao walifika karne ya 19 (1898) inahitajika elimu, mshikamano na hofu ya Mungu kwa watendaji.

Mungu ibariki Peramiho, Mungu kibariki Chuo cha ufundi Stadi Peramiho, ili kizidi kusonga mbele na kuendelea kusaidia taifa hili katika kitengo nyeti cha ufundi, Amina!


Post a Comment