Utangulizi
Waliosoma somo la Sayansi ya Jamii (Sociology) watakubaliana nami kwamba katika dunia hii kuna baadhi ya makundi ya watu ambayo hutegemea makundi mengine ya watu ili kusonga mbele kwa upande wa maendeleo ya dunia vile vile kiroho.
Makundi hayo ya watu yanayotegemewa katika kuiongoza jamii huwa kama dira au mwanga ili wengine wanufaike na hekima, busara, ushauri au fadhila zao.
Kwa mfano watoto hutegemea wazazi wao katika malezi, kufundishwa maadili n.k. wanafunzi hutegemea walimu ili wafikie lengo lao.
Wagonjwa huwategemea waganga, upande wa serikali kwa viongozi raia hutegemea busara, hekima, akili ili waongozwe vema kuelekea kwenye kilele cha mafanikio.
Viongozi wa dini nao hutegemewa na wakristo ili wapate kuongozwa vizuri upande wa kiroho ili kujengwa maadili ya kiroho na baadaye kufika mbinguni.
Viongozi hao au makundi hayo ya watu huwa na kazi ya kuongoza, kufundisha, kulea na kutoa mwongozo. Huwa kama “Mwanga” katika jamii, huwa pia kama chumvi ili kuendeleza mema na kukemea mabaya au maovu ili watu wawe wema huku wakiendeleza maendeleo ya kimwili na kiroho.
Ndio maana Wahenga wetu walipoona hilo walitunga methali ya “Asiye sikia la mkuu huvunjika guu” achilia mbali maana inayotolewa kila mara; kama usipowasikiliza wakuu katika maonyo na maadili utapata hasara bali pia usipowasikiliza wakubwa katika ushauri wa mema; maonyo yao, busara, hekima ni sawa na mtu anayetembea gizani na kuuacha mwanga.
Tabia ya baadhi ya viumbe kuchukia mwanga na kupenda giza
Katika dunia hii kuna baadhi ya viumbe ambavyo vina tabia ya kuchukia mwanga na kuipenda giza. Baadhi ya viumbe vinavyoshabikia giza na kupiga teke kabisa mwanga ni pamoja na mdudu aitwaye mbu, kipepeo na nzige wa usiku pindi afanyapo tendo la kuruka vile vile kunguni na wadudu wengine wenye tabia kama hiyo. Aidha wanyama wengine wenye tabia hiyo ni kama vile popo, simba, chui, panya n.k.
Wataalam wa saikolojia ya wadudu na wanyama hutuambia kuwa wanyama, ndege pia wadudu hufanya hivyo kwa sababu ya tabia walizonazo hasa pale wanaposalimisha maisha yao au kwa sababu ya kujipatia mawindo yao kirahisi, mfano mdudu aina ya mbu hupenda kuwinda usiku ili kupata damu ya mnyama au mwanadamu pindi alalapo usiku.
Lakini pia panya, simba, paka, popo na wengineo hupendelea giza ili kupata mawindo yao kirahisi. Upo uthibitisho wa kutosha juu ya baadhi ya wadudu kama vipepeo, nzige na kumbikumbi huogopa kuonekana kwenye mwanga kwa sababu ya kuwaogopa maadui zao wanaoweza kuwapata kirahisi zaidi wakati wa mwanga kuliko wakati wa giza.
Ndio maana wadudu hao huwa na tabia ya kuzima mishumaa, vibatali au taa. Vile vile giza utumiwa na wanadamu katika kufanya mambo mema kama vile kujenga madaraja wakati wa usiku, mikutano na starehe lakini pia watu hutumia giza ili kubomoa nyumba za watu na kuwaibia mali zao, hutumia giza kwa ajili ya uzinzi, kufanya mauaji n.k.
Giza ni kielelezo cha maovu na mwanga ni kielelezo cha mema.
Mwanga na giza katika Biblia humaanisha nini?
Katika gano Jipya maneno “Mwanga na giza” yana maana tatu:
(a) Kama vile jua liangazavyo njia kwa mwangaza wake vivyo hivyo kila chochote kiangazacho njia ya kwenda kwa Mungu ni Mwanga.
Zamani sheria, hekima pia neno la Mungu (Mhu 2:13, Mit 4:18-19, 6:22, Zab 119:103, Rum 2:19) vilikuwa mwanga. Sasa Yesu Kristo ni Mwanga (Yoh 1:9, 9:1-39, 1Yoh 2:8-11), anayejifananisha na wingu la moto katika kutoka Misri (Yoh 8: 12, kut 13:21-22, Hekima 18:3-4) Mwishowe kila mkristo auonyeshaye ulimwengu fadhila za Mungu ni mwanga (Mt 5:14-16, Lk 8:16, ufu 21:24).
(b) Mwanga ni kielelzo cha uzima, heri na furaha. Giza ni kielelezo cha kifo, maafa, machozi (Ayu 30:26, Isa 45 :7, Zab 17:15). Giza ya utumwa inapingana na mwanga wa wokovu wa masiha (Isa 8:22-9:1, Mt 4:16, Lk 1:79, Rum 13:11-12).
Mwanga wa Kristo utawaangiza pia hata wapagani (Lk 2:32, Mdo 13:47, Efe 5:14).
(c) Mwanga na giza ni kielelezo cha falme mbili zinazohitalafiana na kupingana yaani ufalme wa mema utawaliwao na Kristo na ufalme wa maovu unaotawaliwa na shetani (2 Kor 6:14-15, Kol 1:12-13, Mdol 26:18, 1Pet2:9).
Kila ufalme unajaribu kuushinda mwingine (Lk 22:53, Yoh 13:29-30) watu wanagawanyika baina ya wana wa mwanga na wana wa giza (Lk 16:8, 1Thes 5:5, Efe 5:5, Efe 5:5, Efe 5:7-8, Yoh 12:36) kadiri waishivyo kwa mvuto wa Mwanga Kristo au giza shetani 1The 5:4 n.k. 1yoh 1:6-7, 2:9-10).
Wana hao wote watatambulikana katika vitendo vyao (Rum 13:12-14, Efe 5:8-11).
Nuru mfano wa mema na giza mfano wa mabaya
Kwa matumizi ya kawaida kama ilivyokuwa wakati wa Biblia na hata siku hizi nuru huhusishwa na mfano wa mambo yaliyo mema. Wakati giza huhusishwa na mambo mabaya (Ayu 30:26, Zab 112:4, Yoh 3:19-20).
Zaidi sana, nuru huhusishwa na Mungu, Mungu amevaa nuru, hukaa katika nuru, naye mwenyewe ni nuru.
Kwa kuwa Mungu huwa tofauti na viumbe nyote na hasa huwa mbali na mambo yote yaliyo ya dhambi, nuru ni mfano wa utofauti wake (Zab 104:2, Dam 2:22, 1Tim 6:16, 1Yoh 1:5).
Mwanga ni ishara ya Mungu mwenyewe
Katika Biblia umuhimu wa mwanga unaonyeshwa wazi. Mara nyingi umuhimu wake unalinganishwa na giza inayotokana na kukosekana kwa mwanga.
Katika Agano la Kale ukweli huu unadhihiriswa kwenye kitabu cha Mwanzo kuwa Mungu ndiye aliyeumba mwanga (Mwa 1:3-5) imethibitishwa na nabii Isaya kuwa Mwanga ni ishara ya Mungu mwenyewe (Isa 45:7).
Ni pale yanaposimuliwa matendo ya kihistoria yanayoelezea jinsi Mungu kwa upendo wake alivyowakomboa watu wake na kuwaongoza usiku na mchana kwenye maisha ya heri.
Jua litakuwa nuru yako tena wakati wa mchana. Wala mwezi hautakupa nuru ya milele kwako na Mungu atakuwa utukufu wako. Jua lako halitashuka tena. Wala mwezi wako hautajitenga.
Kwa kuwa Bwana mwenyewe atakuwa nuru yako milele na siku za kuomboleza kwako zitakoma. Watu wako nao watakuwa wenye haki wote. Nao watairithi milele……(Isa 60:19-22).
Licha ya Mungu mwenyewe kuwa “Mwanga” anayewakomboa watu wake kutoka giza na kujaliwa maisha ya heri, mtumishi aliyeteuliwa na Mungu mwenyewe kwa mjumbe wake, atapewa wadhifa wa kuwa mwanga au nuru ya mataifa, chombo cha Yahwe cha wokovu wa mataifa yote.
Mimi bwana nimekushika katika haki, nami nitakushika mkono na kukulinda na kukutoa uwe Agano la watu na nuru ya mataifa (Isa 42:6), hii ni sehemu mojawapo katika Biblia inayoonyesha kuwa wale wote walioitwa na Mungu kwa wito maalum kama ule wa ukasisi, utawa, ukatekista na watumishi wa Mungu ambao pia ni Nuru ya mataifa wanaotekeleza utume wao kwa nguvu na uwezo wa Mungu.
Hitimisho
Mkristo katika ulimwengu huwa si mwanga tu bali pia chumvi. Bwana wetu Yesu Kristo alitumia ishara ya chumvi iliyojulikana sana kwa wafuasi wake ili wazingatie uzito na umuhimu wa utume aliowakabidhi katika ulimwengu wenye utandawazi wa aina mbalimbali, maovu mengi, ukosefu wa haki, dhuluma, kuchakachulijiwa dini na upotofu wa imani.
Mkristo daima awe mtume mwaminifu wa Mungu, akitii Amri za Mungu na kukemea maovu, kuungama imani yake kwa watu pia kushindania haki ya wanyonge bila kuogopa watu.
Kama vile chumvi hufanya kazi ya kutakasa katika maisha yetu, kuhifadhi vitu visioze, inasaidia kukoleza. Vile vile mkristo afanye kazi ya chumvi ya kukoleza imani Katoliki kwa watu waweze kuonja ukweli wa Imani.
Leo hii watu wengi huitekeleza imani na kuwa kinyume na imani Katoliki hawawi mwanga wala chumvi.
Vijana wengi walio wakristo badala ya kujisomea vitabu vya dini ili kuongeza imani, hukusoma magazeti ya udaku, husoma habari chafu za mapenzi na mengine ya namna hiyo.
Kazi mojawapo ya mkristo ni kuleta mwanga kwa kutumia Injili kwa kuziponya familia zile zinazokaa uchumba ili zifunge ndoa , huhimiza watu waende kusali siku za Dominina na katika JNNK, kuwatembelea wagonjwa na kuwafariji, kukemea imani za kishirikina, kuhimiza watoto katika familia ili wazingatie ibada.
Tunapofanya hivyo tutaitwa Mwanga na chumvi katika dunia hii iliyo na maovu ya aina mbali mbali.
Post a Comment