Ads (728x90)

Powered by Blogger.


 
Bila shaka sote tunamkumbuka mchezaji kilaka aliyewika na timu ya Lipuli Fc na Majimaji ya Songea, udogo wa umbile lake ulifichwa na ushujaa wake wa kupambana uwanjani kwa kutumia akili alizotunukiwa na mora kisha akapata heshima lukuki mbele ya mashabiki wake.

Alikuwa na uwezo wa kucheza namba zote uwanjani kwa kutumia miguu yake yote miwili, licha ya kucheza namba zote alipendelea zaidi namba nane; sio mwingine ni James Mhagama mwakilishi wa vilabu TFF toka mkoani Ruvuma kuanzia 2010 hadi sasa.

Asili yake ni Lituhi huko Nyasa lakini kutokana na majukumu ya kikazi kwa wazazi wake wakahamia Rudewa (Njombe)  kisha Dar es salam. 

 

Mwaka 1984 alimaliza shule ya msingi Mbuyuni (Dar es salam) kisha akaendelea na masomo ya Sekondari katika shule ya St. peter’s Junior Seminary huko Morogoro. Mhagama anafafanua yafuatayo kuhusu historia yake ya soka:

“Nilianza kucheza mpira nikiwa mdogo katika mtaa wa Twiga na Jangwani pamoja na shuleni kwenye mashindano ya Umitashumta pamoja na Umiseta”.

“Nyota yangu iling’aa zaidi katika timu ya Kanisa Katoliki la St. peter’s Ostabey huko Dar es salam, timu yetu ilisimamiwa na Fr. Kamilius Haule na tulifanya vizuri ingawa tulikuwa vijana wadogo wadogo sana”.

“Licha ya kuchezea timu ya Kanisa, vile vile ni nilikuwa mtumishi wa Kanisa, nilivutiwa kufanya kazi hiyo kwa sababu J.K Nyerere alikuwa muumini wa  Kanisani kwetu, alisali Kanisani kwetu kila siku. Nilifarijika sana kusali Kanisa moja na Mwalimu Nyerere hivyo nikapata hamasa ya kutumikia Kanisani”.

“1985 nilijiunga na Sekondari ya St. Peter’s Junior Seminary Morogoro, tukiwa Dar Fr. Kamilius alitujenga katika misingi ya kusomea upadre hivyo tukafanya mitihani ya kwenda Seminari kisha tukafaulu kwenda Morogoro”.

“Nakumbuka wanafunzi tuliotoka Dar es salam tulikuwa  kama 20 hivi! kati ya hao 12 tulikuwa wachezaji  wa ukweli. Uwezi kuamini katika mashindano ya shule darasa letu la kidato cha kwanza lilichukua ubingwa kwa mara ya kwanza”.

“Watu wengi walishangaa sana kwa kuwa mara nyingi ubingwa ulichukuliwa na madarasa ya juu hasa kidato cha sita, lakini sisi tulichukua mara tatu mfululizo”.
 

“Baadae mimi na wezangu watatu tulihamia Njombe, kule nilicheza vizuri sana ambapo kwenye mashindano wa Umiseta shule yetu ilichukua ubingwa wa mkoa na mimi nilikuwa mchezaji bora wa mashindano kisha tukaenda katika ngazi ya kanda Kantalamba (Rukwa) ambapo baada ya kufanya vizuri nikachaguliwa tena kuendelea na mashindano”.

“1990 Lipuli ya Iringa chini ya Pasco Bella wakanisajili na nakumbuka nilisaidia kuipandisha ligi kuu  na  tulicheza kwa ushindani mkubwa, kisha mwaka 1993 nikatimukia Majimaji ya Songea ”.
“Majimaji waliamua kunipa mkataba  baada ya mimi kuwasumbua katika michezo miwili ya ligi kuu, nakumbuka Songea nikiwa na Lipuli tulitoka sare ya bao 1-1 na mimi nikafunga bao moja, kwenye mechi ya marudiano iliyofanyika  Iringa niliwashusha daraja Majimaji kwa kuwafunga bao 1-0”.
“Sema Majimaji waliponea kwenye tundu la sindano kwa kuwa uongozi wa ligi uliamua kuongeza timu zingine, hivyo timu zilizotakiwa kushuka kama Majimaji zikasalimika”.
“Toka Lipuli kwenda Majimaji nilienda kwa masharti ya kwamba ili kunisajili mimi walilazimika pia kumsajili Steven Makuka pamoja na Amri Said kwa kuwa walikuwa rafiki zangu na uchezaji wao ulikuwa mzuri. Niliitumikia   Majimaji hadi 2000 kisha nikaachana na soka”.

“2000 timu ya Polisi ya Songea waliniomba niwe mwalimu wao, niliwafundisha hadi 2004 kisha nikapata fursa ya kuwa mechi kamishina katika michezo mbali mbali ya ligi kuu ya Vodacom baada ya kupata mafunzo maalum ya kazi hiyo”.

“Mwaka 2006 nilichukua fomu ya kugombea nafasi ya ujumbe kwenye chama cha Soka mkoani Ruvuma (FARU) lakini kuna watu walinishauri nichukue fomu ya makamu mwenyekiti ili kunikomoa, kweli nikachukua na nikapata ushindi wa kishindo kisha nikawakwaza kwa kiasi kikubwa wale wote waliozani kuwa ningedondokea pua na badala yake nikaibuka shujaa”.

“Mwaka 2010 nikagombea nafasi ya uwakilishi wa vilabu nafasi ninayoitumikia hadi sasa, vile vile 2013 nikagombea nafasi ya kamati ya utendaji TFF kanda ya nane nako nikachaguliwa kwa kishindo tena kwa kura nyingi kuliko wajumbe wote”. Anafafanua James Mhagama kisha anaendelea.

Timu ya taifa

“Sikupata  nafasi ya kucheza mechi hata moja kwenye timu ya taifa kwa kuwa mwaka 1998, mwaka ambao nilipata bahati ya  kuitwa kwenye Timu ya Taifa ya Vijana na kocha Tauzan Zoisaba timu za taifa zilikumbwa na ukata hivyo kambi yetu ikavunjwa, basi sikupata tena nafasi ya kuitwa kwenye timu za taifa”.

Ajali ya Misungwi

“Ajali ile ilisababishwa na mwendokasi uliosababisha gari kumshinda dereva kwenye kona; kwa bahati mbaya alikufa abiria mmoja tu lakini wachezaji wote tulitoka salama ingawa tulikuwa na majeraha”.

“Baada ya ile ajali TFF walitung’ang’ania tukacheze mchezo wetu uliofuata na Polisi ya Morogoro, baadhi yetu tuliingia uwanjani tukiwa na mishono, lakini tulifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0".
Tukio la Kagera

“Watu wa Kagera wakiniona mara nyingi wanalikumbuka tukio la Majimaji kupewa kadi tatu nyekundu kwenye uwanja wa Kaitaba dhidi ya RTC Kagera zote zilitolewa kipindi cha kwanza. Wachezaji waliopewa kadi hizo ni Dello Ntumba, David Mjanja pamoja na Marehemu Twaa Omari”.
 

“Lakini licha ya kuwa pungufu tuliwakimbiza sana RTC na hadi mwisho wa mchezo tulitoka sare  ya bila kufungana. Kabla  ya kucheza na sisi walitoka kuzikung’uta  Simba na Yanga katika uwanja wa Kaitaba”.

Hawezi kusahu

Kabla ya kusimulia alitikisa kichwa mara nne huku akionesha masikitiko makubwa, akapiga moyo konde huku akiamini kwamba matokeo ni matokeo tu!

“Niliangaika sana kufuatia tukio la kuvunjika mguu mara tatu baada kukanyagwa kwa bahati mbaya na golikipa katika uwanja wa Majimaji kwenye  lango la kusini, ilikuwa ni kwenye mazoezi tu ya kawaida  baada ya kustaafu kucheza mpira”.

“Nilifanyiwa upasuaji mara saba; mara tatu kwenye Hospitali ya Peramiho na mara nne kwenye Hospitali ya taifa Mhimbili Dar es salam. Nashukuru Mungu nimepona kwa kiwango cha kutembea lakini kucheza mpira japo mazoezi tu haiwezekani tena”.

Azam Fc sio washirikina

“Timu zetu zinaamini sana katika imani za kishirikina lakini cha kushangaza Azam Fc mara nyingi sana wananichukua kama kiongozi kwenye msafara wa timu yao sijawahi kuona matukio ya imani za kishirikina, wao wanamtegemea Mungu, wataalamu na mazoezi tu”.

“Mimi siamini katika imani za kishirikina, msimu wa mwaka 1997/98 sisi tulimtoroka mganga hapa Songea bila viongozi wetu kujua na tulienda kanda ya ziwa tukarudi na pointi nane bila kutumia matunguli”.

Majimaji vs Simba na Yanga

“Mara ya mwisho Majimaji kupata ushindi kwa timu hizo mbili katika uwanja wa Majimaji ilikuwa ni mwaka 1999, tuliwafunga Simba bao 2-1 mimi ndio nilifunga bao la ushindi hadi leo haijatokea tena”.

“Sasa nimetoa ahadi kwa wachezaji wa Majimaji atakayezifunga hizo timu kwenye uwanja wa Majimaji nitampa zawadi hata kama sio bao la ushidi kwa timu yake ila kitendo cha kufunga tu! mfungaji wa bao husika nitamzawadia”.

Majimaji

“Timu ili ifanye vizuri inahitaji usajili mzuri, timu ikisajili vizuri mtu yeyote anaweza kuisimamia lakini ikisajili vibaya hata aje Alex Ferguson, bado itafanya vibaya”.
“Majimaji inahitaji malezi bora kwa wachezaji, viongozi bora pia fedha; hayo yote yanawezekana endapo sote tutakuwa kitu kimoja”.

Timu ya taifa

“Kushiriki Afcon inawezekana kama tutakuwa na msingi imara mfano baada ya kuipeleka Serengeti Boys kwenye fainali tulianza kuandaa vijana wa miaka 13 chini ya Malinzi kwa ajili ya mwaka 2019, kambi yao iliwekwa Mwanza kwenye shule ya Allience lakini nayo imeingia doa baada ya uongozi wa juu wa TFF kukabiliwa na mashitaka”.

Ushabiki kwa Simba na Yanga

“Sijawahi kushabikia Simba wala Yanga ingawa ndugu zangu ni wanazi wa timu hizo mbili, mimi ni shabiki wa Majimaji! Azam wananiamini kusafiri nao kwa kuwa mimi sio mtu wa Simba wala Yanga. Wakati nikiwa mchezaji niliwahi kuzifunga timu zote mbili; niliifunga Yanga nikiwa na Lipuli na nikaifunga Simba nikiwa na Majimaji”.

Anahitimisha  James Mhagama ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 45, ameoa na ana watoto watatu.

Mhagama alikuwa jasiri sana lakini anamweshimu sana Said Mwamba Kizota kutokana na umahiri wake wa kucheza mpira pamoja na faulo nyingi uwanjani.
 

Mhagama ni Mjumbe wa TFF kanda ya nane (Njombe & Ruvuma), vile vile ni mwakilishi wa vilabu TFF toka mkoani Ruvuma.


Post a Comment