Watu wa Mataifa
mbalimbali hapa ulimwenguni wana mitazamo tofauti kuhusu hali ya mwanadamu
baada ya kifo “nchi ya wafu”. wenyeji wa Amerika (Red Indians) waliamini kwamba
baada ya kifo chake mtu uingia mahali pazuri pa kawaida.
Lakini baadhi ya
Waskandinavia wa zamani walifikiri kuwa nchi ya wafu kama mahali pa milo
mikubwa mikubwa na heri kwa jumla. Watu wa mashariki ya kati pia walikuwa na
wazo lao kuhusu peponi.
Tena uislamu una
mafundisho yake juu ya “Jaha” na ‘Jehanum”. Waafrika pia toka zamani wana
mawazo mbali mbali kuhusu “kuzimu” na hali ya wale waliokufa.
Katika makala haya
tutazame habari za wafu kiujumla kama linavyofundisha Kanisa Katoliki upande wa
ukristo wetu. Mafundisho hayo yatatusaidia
kuimarisha imani yetu, kuondoa hofu juu ya kifo na kupenda kufa katika
hali njema na baadaye kuishi na Mungu huko mbinguni milele yote.
Mahali
walipo wafu kadiri ya maandiko matakatifu
Katika imani ya Kristo
na mafundisho ya Kanisa Katoliki, ufufuko na hukumu ya mwisho zitatangulia
maisha ya milele.
Swali katika makala
haya ni wafu wako wapi baada ya kifo na kabla ya kiyama? Kwa sababu maalum
Agano la Kale halivutwi na swali la maisha ya baadaye. Hivyo tutachunguza jibu
la swali letu hasa katika Agano Jipya.
Ingawa Agano Jipya
halielezi habari hizi kwa uwazi, ila limetoa dokezo kadhaa. zaidi lakaza habari
za kiyama, hukumu ya mwisho na uzima wa milele.
Hata hivyo tujaribu kuchunguza swali hili kwa msaada wa dokezo hizo tunazozipata katika Agano Jipya.
Inawezekana ya kwamba
msomaji baada ya kusoma kifungu hiki atasema
“maelezo haya ni kufikirifikiri tu” Tunamkaribisha msomaji wa namna hii
atoe maelezo yake yeye mwenyewe.
Hapa tena lazima
tuache mlango wazi kwa tafsiri na mikazo mbalimbali kwa kila hali, swali letu
la kifungu hiki ndilo muhimu sana katika mazingira ya kiafrika na kwa mwanadamu
yeyote kwa jumla.
Agano
Jipya na habari za wafu
Mistari fulani ya
Agano Jipya yasema kwamba wafu wamelala usingizini (Taz. Mt 27:52, Yoh. 11:11,
Mdo 7:60, 13:36, 1 Kor 11:30, 15:6, 18, 20, 51, 1Thes 4:13-15).
Kutokana na mistari
hiyo, baadhi ya wataalam wa Biblia hudai ya kwamba kifo ni kifo cha mwili na
Roho pia (K.m Poul Athaus na Emil
Brunner).
Yaani hakuna sehemu
yeyote ya mtu iendeleayo kuwako baada ya kifo. Baada ya kifo mtu hubaki katika
ukumbuko wa Mungu tu. na katika
kiyama Mungu atamwumba upya kwa kufuata
ukumbuko wake.
Nguvu ya elezo hilo
ni kwamba lapatana na maoni ya utabibu na sayansi nyingine za leo kuhusu mtu,
jinsi alivyo kitu kizima.
Mtu hawezi
kugawanyika katika sehemu mbali mbali. Mwili na roho haviwezi kutengana. Kwa
kweli yaonekana wazi kwamba ni hivyo katika maisha yetu ya hapa duniani.
Kwa mfano magonjwa
mengi ya kimwili, vidonda vya tumbo, magonjwa mbalimbali ya moyo n.k. yana asili zao kwa upande wa roho ya mtu (Psycho-
Somatic diseases).
Vile vile tukio fulani la kimwili huweza kugusa roho ya mtu
kwa mfano akigongwa kichwani vibaya na gari barabarani, akili yake yaweza
kuharibika. Katika maisha roho haiwezi kutenganishwa na mwili, wala mwili
kutenganishwa na roho.
Agano
Jipya na suala la uwepo wa nafsi ya mtu mahali fulani
Lakini tukumbuke
kwamba hapa hatushughuliki na habari za maisha wa uhai, bali ni kifo na hali ya
baadaye. Kudai ya kuwa katika Agano Jipya kulala (usingizini) kwa maanisha kifo
cha mwili na roho labda ni sawa.
Mtu aliyelala bado
yupo au yuko, ila kwa hali nyingine
katika Agano Jipya neno kulala lilikihusu kifo hukaza habari za kufufuka
kama kuamka kuliko habari za kifo cha mwili na roho.
Elezo hilo la kifo
cha namna hii haliwezi kukubarika nasi
hasa kwa sababu ya dokezo za aina nyingine za Agano Jipya.
Agano Jipya hudokeza
wazi ya kutosha kwamba baada ya kifo na kabla ya kiyama mtu huendelea kuwako
kwa njia fulani.
Yesu aliwaonya
wanafunzi wake “msiogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho (Mt 10:28). Daktari
Luka akisimulia juu ya binti wa Yairo, asema: “Roho yake ikamrejea , naye mara
hiyo akasimama” (Lk 8:55). Stephano alipigwa kwa mawe, aliomba na kusema:
“Bwana Yesu, pokea roho yangu” (Mdo 7:59, tazama pia (Lk 23:46).
Pia tukumbuke pia juu
ya Bwana wetu Yesu Kristo wakati kabla ya kufa kwake msalabani alivyomwahidi
yule mhalifu wa pili aliyesulibiwa pamoja naye na kusema: “leo hivi utakuwa
pamoja nami peponi (Lk 23:43).
Pia tukumbuke hapa
mfano wa Yesu juu ya yule tajiri na Lazaro (Lk 16:19-31) Paulo Mtume naye kwa
upande wake aliugua katika mateso mengi: “Tuna moyo mkuu, nasi tunaona ni
afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana” (2 Kor 5:8, Taz pia
Flp 1:23).
Anasisitiza kwamba
hata mauti haiwezi kutengana na upendo wa Mungu (Rum 8:38-39). Mwandishi wa
waraka kwa waebrania ataja wingu kubwa la mashaidi ambalo hutuzunguka (Ebr
12:1
Na katika (1Petro
3:18-19) na 4:6 twapata habari za Yesu jinsi alivyowahubiri roho waliokaa kifungoni.
Mistari hiyo ni msingi wa Biblia kwa kukiri kwa wakristo katika ibada kuhusu
Kristo: “Akashuka kuzimu”.
Ufunuo 6:9-11 kwa
upande wake yataja habari za roho za wale waliochinjwa kwa ajili ya neno la
Mungu na ushuhuda wao.
Katika kifo mwili
hufa na sehemu nyingine ya mtu hutengana nao. Twaweza kuiita sehemu hiyo kwa
maneno mbalimbali: “roho”, “Nafsi” n.k. Jambo muhimu hapa sio neno fulani
litumikalo.
Jambo kuu ndilo ya
kwamba kutokana na mafundisho ya Agano Jipya kwa njia fulani mtu huendelea kuwako
baada ya kifo cha kimwili (kwa upande wa Agano la kale Taz dokezo la Zab
49:14-15, 73:24, 139, Mhu 12-:7, Eze 26:20, 32:17-32).
Baadhi ya watheolojia
hukataa maelezo hayo kama wazo la dini nyingine ama wazo la kifilosofia.
Wengine hudai kwamba maelezo hayo ni mabaki ya imani ya zamani kuhusu roho
(Animism).
Lakini tusisahau ya
kwamba mawazo ya fulani ya dini nyingine na Filosofia na hata maoni ya zamani
ambayo watu wengine huyaita “Primitive” yaweza kuwa kweli (Taz mfano wa Mungu
na ufahamu wa asili kuhusu Mungu uk. 9-13).
Wafu
wapo wapi?
Mpasa sasa Biblia
imetupa nuru ya kutosha lakini sasa tujaribu kujibu swali hili. Tulichunguza
kwa kutokana na dokezo kadhaa tu.
Labda peponi (Lk
23:43) ama kuzimu (Lk 16:23), ni hali maalumu kuliko mahali penyewe hasa. Katika
theologia kuita hali hiyo “hali ya katikati” maana yake ni hile hali ya
katikati ya kifo na kufufuka.
Inaonekana katika
hali hiyo ya katikati mtu huwa katika hali ya unafsi ule ule, ambao alikuwa nao
duniani humu Lk 16:22-23) yaani, Paulo bado ni Paulo, yule tajiri ni mtu yule
yule na Lazaro ni Lazaro.
Licha ya kutambua
unafasi wake mtu awafahamu watu wengine pia (Lk 16:23) kwa njia fulani huwezi
kufahamu hata maisha ya wale waishio duniani (Lk 16:22-24). Hali hizo mbili
huzitangulia ufufuko kwa uzima na ufufuko kwa hukumu (Lk 16:26, Yoh 5:28-29).
Kuhusu wale
wasiosikia habari njema, Mungu labda
huwapa nafasi hiyo huko kuzimu maneno ya Lk 16:26 kuhusu shimo kubwa
hayapingani na uwezekano huo.
Tukisoma sura nzima
ya 16 ya mwinjili Luka, twaona kwamba yule tajiri alikuwa mojawapo ya
mafarisayo. Kwa hiyo bila shaka alijua mapenzi ya Mungu.
Basi ikiwa maelezo
hayo ni sawa, katika kiyama ule unafsi utavikwa mwili mpya. Kwa maneno mengine
utalinganishwa na mwili wa roho ama mwili wa mbinguni (1Kor 15:40,44).
Hitimisho
Kamati
inayoshughulika na maelezo ya imani katika Kanisa Katoliki na kutoa mawaidha
ambayo hutiwa sahihi na Papa kuhusu hali ya wanadamu baada ya kufa hutuelekeza
mambo yafuatayo ili imani yetu iweze kudumu na kuimarika na kutembea katika
mwanga juu ya imani upande wa kifo.
Mafundisho
ya Kanisa Katoliki kuhusu wafu:
(A) Wakristo
wanasadiki ya kuwa wafu watafufuka.
(B) Ufufuko
wamhusu mtu mzima.
(C) Baada
ya kifo nafsi ya kibinadamu hudumu yaani huendelea kujijua mwenyewe kama nafsi
(Mimi), kuwa na dhamiri na utashi. Kwa kifupi mwanadamu aliyekufa huitwa roho
(lihoka).
(D) Madhehebu
ya mazishi na ibada kuhusu marehemu huwa na maana halisi wala haifai kuvipuuza.
(E) Kadiri
ya maandiko matakatifu sisi wakristu tunangojea kurudi kwa Bwana katika
utukufu.
(F) Kuchukuliwa
kwa Bikra Maria mbinguni humaanisha kutukuzwa kwa sisi sote.
(G) Tunasadiki
ya kuwa wenye haki wanakuwa na heri pamoja na Kristo na wasio na haki walainiwa
milele wasiweze kumwona Mungu.
Pia
tunasadiki kwamba wenye haki waweza kusafishwa kabla ya kumtazama Mungu uso kwa
uso, kwa upande mmoja sisi wakristo tunayo imani thabiti ya kuwa tutadumu
kuishi ndani ya Kristo baada ya kufa.
Kwa
upande mwingine twajua pia yakuwa maisha yetu yatengenezwa mbali na hali ya
hapa duniani. Tutakuwa pamoja na Kristo tukimwona Mungu.
Katika kueleza imani
hiyo lazima kuepa mambo yote mawili: tusitoe habari za kitoto (kama malaika
wadogo wenye mabawa) wala tusiibomoe imani kwa maneno yasiyoeleweka.
Post a Comment