“Namna gani mbona hamwelewi vijana!...... ” ni Maneno ya mzaha au
masihara toka kwa aliyekuwa Abate wa tatu wa Abasia ya Peramiho,
Emeritus Lambert (Helfried) Dorr (OSB) akiwa darasani na wanafunzi wa
utawa, mwaka 2006 (Peramiho).
Uwezo wake wa kupandikiza elimu kwa
wanafunzi wengi aliowahi kuwafundisha katika maisha yake wakiwemo
wanafunzi wa Likonde pamoja na Abasia ya Peramiho, utakumbukwa daima
bila kificho, kwani waswahili wanasema “Kizuri kinajiuza, kibaya
kinajitembeza”.
Safari ya maisha ya Padre Lambert ilianza mwaka
1936 katika kijiji cha Gerolzahn kwenye jimbo la Freiburg huko nchini
Ujermani. Mwaka 1956 alifanikiwa kufunga nadhiri za muda baada ya
kuaminiwa utawani.
Alipata fursa ya kupadirishwa Juni 29, 1960
baada ya kufuzu mafunzo yake vizuri. Alikuja Afrika (Afrika Mashariki)
katika viunga vya Peramiho (Tanzania) mwaka 1964.
Akiwa mkoani
Ruvuma alianza na kazi ya kufundisha katika Seminari ya Likonde huko
Mbinga, kisha Mwaka 1970 alirudishwa Peramiho na aliendelea na kazi yake
ya kufundisha katika Seminari ya Peramiho, wanafunzi wa utawa na kazi
yake mama ya kutangaza neno la Mungu.
Desemba 08, 1976
alichaguliwa kuwa Abate wa tatu wa Abasia ya Peramiho lakini Kabla ya
hapo alikuwa Priori wa Abasia hiyo hiyo ya Peramiho.
Kijiti cha
Uabate alikipokea toka kwa Abate Eberhart Spiess OSB, huku Abate wa
kwanza wa Abasia ya Peramiho akiwa ni Gallus Steiger OSB.
Lambert
alipewa nafasi ya kuwa Abate wa Abasi ya Peramiho isyokuwa na kikomo,
lakini yeye baada ya kufanya kazi hiyo kwa miaka 30, mnamo mwaka 2006
aliamua kustaafu na kupisha nguvu mpya kwenye kiti hicho.
Kabla
ya yeye kurudi Ujerumani mwaka 2015, baada ya kustaafu alienda kupumzika
katika Monasteri ya Tororo (Uganda) kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu
kisha mwaka 2008 akarudi Peramiho.
Awali Abate Lambert alipanga
kuwa akifa azikwe Tanzania katika makaburi ya Abasia ya Peramiho hata
hivyo kutokana na kusumbuliwa na mguu wake wa kushoto kwa muda mrefu
madaktari walimshauri kwenda kupata matibabu nchini kwake Ujerumani kwa
kuwa Tanzania hakuna hospitali inayoweza kumtibu.
“wakati wowote
kabla ya mwisho wa mwaka huu natarajia kurudi nyumbani kwangu Ujerumani
kwa ajili ya matibabu ya mguu wangu wa kushoto hivyo kwa kuwa matibabu
hayo ni endelevu siwezi kurudi tena Tanzania’’,alisema Abate Lambert
mwaka 2015.
Januari 04, 2015 akaagwa rasmi na waumini wa Parokia
ya Peramiho katika kipindi ambacho wengi wao bado walikuwa wakiuhitaji
msaada wake.
Abate Lambert alikuwa mwalimu wa somo la Historia ya
Kanisa katika Seminari ya (Likonde) Kigonsera tangu mwaka 1964
amewafundisha viongozi mbalimbali wa Kanisa na serikali wakiwemo Askofu
Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Songea Mhashamu Norbert Mtega.
Kabla
ya roho yake kuhitimisha safari yake ya hapa duniani Oktoba 22, 2017;
mapema mwaka huu, akiwa nchini Ujerumani alipelekwa kwenye nyumba ya
Wagonjwa katika Monesteri ya Munsterschwarzach kwa ajili ya matibabu
zaidi. Hakika kazi ya Mungu haina makosa, Pumzika kwa amani Abate
Lambert!
Moja ya watu ambao wameshtushwa na kifo chake ni Mwanafunzi wake Mtawa Fredrick Mwabena OSB aliyekuwa mwanafunzi wake wa Utawa toka mwaka 2006 hadi 2009 na amefafanua yafuatayo:
“Abate Lambert
Dorr OSB, Apumzike kwa Amani. Babu na Mwalimu Wangu, wenyewe tulizoea
kumwita Walking Encyclopedia maana alikuwa msomi wa kweli kweli”.
“Kazi yake ya kuiendeleza Abasia ya Peramiho itakumbukwa daima hasa
kuanza kuwapokea watawa wazalendo/Africans, 1982 suala ambalo halikuwepo
kabla yake na kipindi hicho kilikuwa kigumu sana kwa watawa wazungu na
waafrika kukaa nyumba moja lakini yeye alifanikiwa kuukata mzizi huo wa
fitina”.
“Lambert alipenda watu wasome, kuna kipindi kuna Mtawa
mmoja aliomba kwenda kusoma lakini utawala ulimcheleweshea majibu yake,
akaamua kujifungia ndani siku tatu. Taarifa zilipomfikia Abate Lambert
siku ya pili yake akapewa ruhusa ya kwenda shule”.
“Lambert
alikuwa mtu wa Sala, alikuwa mtu wa masihara, aliwapenda watu wa aina
zote bila kuwabagua, alikuwa muwazi, vile vile alikuwa mshauri wa mambo
ya taaluma hapa Tanzania”.
“Aidha namkumbuka Lambert alikuwa na
sauti nzito sana, hapo Kanisani kwetu zile maiki hazikuwa na msaada
kwake alikuwa na uwezo wa kuongea kwa sauti kubwa mno.
Mwisho alikuwa mpenzi sana wa kuvuta Kiko” alisimulia kwa masikitiko makubwa, Bro. Frederick Mwabena OSB.
Vile vile Kat. George Milinga alifafanua kwamba kifo cha Abate Lambert
kimeliachia Kanisa pengo kubwa mno kwa kuwa amelifanyia mambo mengi
mazuri:
“Yeye ametunza yatima wengi sana, nyumba nyingi za kitawa
Kenya, Tanzania na Uganda zilijengwa na kufunguliwa wakati wa uongozi
wake”.
“Alitumia fedha nyingi katika ujenzi wa Makanisa mfano
Kanisa la Mbinga Mharule na kuwasaidia Mapadre na Makatekista na
wakristo wengine; aliupenda upadre wake, utawala wake na mtu wa kutoa
mahubiri yenye ujumbe mzito
”.
”.
“Yeye alikuwa msomi na mwandishi wa vitabu vingi vya historia, vile vile alikuwa mwalimu wa somo hilo. Alikuwa mwanzilishi wa watawa waafrika wa kiume ambao tunawaona. Kabla yake walikuwepo watawa Wabenediktine Wamisionari wazungu tu!”.
“Yeye hakupenda makuu, aliishi na waafrika vizuri bila majivuno na alikuwa baba wa wote” anasisitiza mzee Milinga”.
Abate Lambert Yeye ni Msomi wa hali ya juu, alisoma Seminari Kuu ya
Saint – Etienne na Voicebook, vile vile alipokuwa kwenye maandalizi ya
kuja Afrika yeye na Padre Bonifaz Dinkel walipata fursa ya kwenda
kusomea (Historia ya Kanisa) nchini Canada.
Atazikwa tarehe 27,
2017 siku ya Ijumaa huko Ujermani, wakati nchini Tanzania Tarehe 26,
siku ya Alhamisi, Kanisa la Abasia ya Peramiho litafanya Misa maalum ya
kumwombea.
“Kwa Maana huyu alionekana anampendeza Mwenyezi Mungu, akachukuliwa”
SOLI DEO HONOR ET GLORIA-KATIKA YOTE MUNGU PEKE YAKE ATUKUZWE.
Post a Comment