Ads (728x90)

Powered by Blogger.


Na Albano Midelo

Kwa miaka mingi  mji wa Songea umekuwa unakabiliwa na mgawo mkali wa umeme hali ambayo imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika mji huo ambao ndiyo kioo cha Mkoa wa Ruvuma.


Mchawi mkubwa wa tatizo la umeme katika mji wa Songea ilikuwa kuendelea kutumia Jenereta chakavu ambazo zilikuwa zinatumia vipuli chakavu na changamoto ya mafuta ambayo yalikuwa yanakwisha mara kwa mara.


Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Agosti 2009 alifanya ziara katika Mkoa wa Ruvuma kwa lengo la kuangalia shughuli za kimaendeleo na changamoto zinazowakabili wananchi wa mkoa huo.

Siku ya kwanza ya ziara yake Rais Mstaafu Kikwete wakati anapita barabarani akitokea uwanja wa ndege wa Songea alishuhudia wananchi wakipiga kelele na kudai umeme huku wamewasha taa mchana  kutokana na hali halisi ya tatizo sugu la umeme wa kutoaminika katika mji wa Songea ambalo lilikwamisha shughuli za kijamii na kiuchumi.


Rais Mstaafu Kikwete alisikitishwa na kasi ndogo ya kushughulikia ufumbuzi wa tatizo la vipuri vya mashine za kufulia  umeme katika mji wa Songea hali liyosababisha kumwagiza Meneja wa TANESCO mkoa wa Ruvuma wakati huo injinia Monica Kebara  kufuatilia ili kujua vipuri vya mashine hizo vipo wapi na alitaka kupata ripoti ya vipuri hivyo na mwenendo  mzima wa matengenezo ili wananchi  wafahamu kila hatua.


Rais Kikwete hakuishia hapo, badala yake aliahidi kuileta mashine mpya ya kufua umeme ambayo aliamini ingeweza kumaliza tatizo la mgawo mkali wa umeme katika mji wa Songea hivyo mgawo mkali wa umeme kubakia kuwa historia.


Baada ya kufungwa mashine mpya ya Rais Kikwete aina ya  ABC yenye uwezo wa kuzalisha megawati 1.6  angalau tatizo la mgawo mkali katika mji wa Songea lilipungua kwa miaka takribani mitatu, ingawa matatizo ya mafuta na vipuri yaliendelea na kuathiri umeme katika mji wa Songea.


Hata hivyo baada ya miaka hiyo tatizo la mgawo mkali wa umeme liliongezeka kutokana na kile ambacho kilitajwa na TANESCO kuwa ni kuharibika kwa mashine kutokana na vipuri kuharibika.


Tangu mwaka 2016 tatizo la mgawo wa umeme katika mji wa Songea limebakia kuwa historia mara baada ya TANESCO Ruvuma kuanza kununua umeme wa maji kutoka Tulila mto Ruvuma.


Chanzo hicho kinamilikiwa na watawa wabenediktine wa Mtakatifu Agnes Chipole Jimbo Kuu Katoliki la Songea ambapo sasa tatizo la umeme katika mji wa Songea limebakia kuwa historia.


Akizungumza kwa niaba ya Mama Mkuu wa Shirika hilo, Sr.Richards Chiwinga(OSB) anasema wana mashine mbili ambazo zina uwezo wa kuzalisha megawatts tano ambapo TANESCO Ruvuma ndiyo wateja wao wakuu ambao wanawauzia umeme huo.


“Mji wa Songea unahitaji megawatts kati ya 3.5 hadi 4.5 hivyo tunabakiwa na ziada ya umeme, TANESCO wamezima majenereta yao chakavu ambayo yalikuwa yanasababisha mgawo wa umeme, hivi sasa wanatumia umeme wetu wa maji unaozalishwa toka hapa’’,anasisitiza Sr.Chiwinga.


Hata hivyo anasema ili kufanikisha mradi huo mkubwa wa umeme Shirika lilipata ufadhili toka kwa raia mmoja wa nchini Uswis anayefahamika kwa jina la Robert Fuchs ambaye alikopa mkopo toka Benki ya Dunia kiasi cha dola za Marekani milioni 30 ambazo zimetumika kujenga mradi huo na kwamba shirika linarudisha mkopo huo kidogo kidogo.


Akizungumzia historia ya mradi wa umeme wa Tulila, Sr.Veritas Ndumbili (OSB) ambaye ni mtaalam wa umeme wa maji anabainisha kuwa ujenzi wa bwawa hilo ulianza tangu mwaka 2010 ambapo kampuni ya kutoka nchini  China ndiyo ilishinda tenda ya kujenga mradi  huo.
Hata hivyo Sr.Ndumbili anabainisha kuwa ujenzi kamili wa mradi huo ulianza mwaka 2012 na kwamba shughuli za ujenzi huo zilikamilika Septemba 2014 na kwamba tayari kampuni hiyo imekabidhi mradi huo kwa shirika hilo.


“Kazi iliyobaki ni yetu sisi, hadi sasa tuna mashine mbili zenye uwezo wa kuzalisha megawati tano, lengo ni kuzalisha umeme megawati 7.5, kwa hiyo tutaongeza mashine moja yenye uwezo wa kuzalisha megawati 2.5’’,anasisitiza Sr.Ndumbili.


Anasema bwawa la Tulila lina ukubwa wa meta za ujazo milioni 1.14, likiwa na urefu wa meta 750 toka usawa wa bahari na usawa wa maji (level) ni meta 748 na kwamba maji yakizidi kiwango hicho yanamwagika.


Kulingana na Sr.Ndumbili, Shirika katika eneo hilo la Tulila, linamiliki eneo lenye ukubwa wa ekari 1000 ambapo wanatarajia pia kuweka maeneo mazuri kwa ajili ya fukwe kupigia picha, kufanyia pikiniki na kuogelea  lengo likiwa ni kufungua  milango ya utalii kwa wageni wa ndani na nje ya nchi katika eneo hilo.


Changamoto kubwa inaoukabili mradi huo wa maji ni magugu maji ambayo yanasababisha mashine kujizima  hivyo ili kukabiliana na hali hiyo Shirika limemwajiri kijana ambaye kila siku anaingia kwenye bwawa kuondoa magugumaji hayo.


Hata hivyo Sr.Ndumbili anaitaja changamoto kubwa ambayo inahatarisha uzalishaji wa umeme kuwa endelevu ni uwepo wa Mwekezaji katika shamba la kahawa eneo la Lipokela ambaye anatumia maji ya mto Ruvuma kumwagilia anasababisha upungufu wa maji unaoweza kuathiri uzalishaji wa umeme.


“Kwa kweli Mwekezaji huyo amekuwa anatusababishia tukose maji hapa,tunaomba serikali itusaidia, yeye anatumia maji mengi sana, kwa mfano mwezi Mei mwaka huu maji yalikata ghafla hapa, tulimfuata Mwekezaji, kumbe alikuwa ameingiza maji kwenye mitambo yake tulivyompigia kelele ndipo alifungulia, siku ya pili maji yakaanza kushuka kwetu’’, anasema.


Anasisitiza kuwa ni vema serikali imtafutie Mwekezaji huyo eneo la chini zaidi ili awekeze kwenye kilimo chake kwa sababu kuna siku watashindwa kuzalisha umeme  na kuleta matatizo kwa watumiaji wa umeme katika mji wa Songea na vijiji vya wilaya za Songea na Mbinga.


Mahitaji ya umeme katika mji wa Songea ni kilowatts 4300 hivyo basi kutokana na umeme wa maji unaozalishwa Tulila, TANESCO Ruvuma imefanikiwa kumaliza kabisa tatizo la mgawo wa umeme katika mji wa Songea. 


Hata hivyo TANESCO kwa kushirikiana na ufadhili wa serikali ya Sweden, imeaanza utekelezaji wa mradi wa umeme wa Gridi ya Taifa kutoka Makambako hadi Songea ambao unatarajia kufika mjini Songea mwaka 2018. 


Taarifa ya Wizara ya Nishati na Madini inaeleza kuwa ujenzi wa mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa Gridi kutoka Makambako hadi Songea ambao utahusisha pia kujenga mifumo ya kusambaza umeme vijijini katika Wilaya za Ludewa, Namtumbo na Mbinga ni hatua muhimu ya kuleta maendeleo endelevu katika mikoa ya Kusini.


Sera ya Serikali katika umeme ni kuhakikisha wananchi wengi wanapata nishati ya umeme, ingawa takwimu hivi sasa zinaonesha kuwa wananchi wanaopata nishati ya umeme nchini imepanda toka asilimia 10 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 67 mwaka 2017.




Post a Comment