Ads (728x90)

Powered by Blogger.


Na Albano Midelo

Dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabianchi hali ambayo inaifanya Sayari ya hii, kuwa njia panda.


Kutokana na hali hiyo viongozi wa nchi na serikali wa mataifa 150 duniani Desemba 2015 walifanya mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabia mjini Paris nchini Ufaransa, wakijitwisha dhamana ya mpango wa kihistoria wa kuepusha maafa ya ongezeko la joto duniani. 

Viongozi hao walipendekeza  mpango wa kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaofanywa na binadamu na kuepusha athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi ambazo zinaweza kuangamiza viumbehai wote duniani.

Katika mkutano huo ulioshirikisha watu zaidi ya 900 walifikia makubaliano ya kupunguza joto duniani, baada ya jitihada za msukumo wa awali wa viongozi wa dunia kutoonesha mafanikio ya kutosha. 

Miongoni mwa vikwazo vilivyokwamisha makubaliano ya awali ni  nafasi ya mataifa mawili makubwa yenye kuelezwa kufanya uchafuzi mkubwa wa mazingira China na Marekani kufanya jitihada ndogo katika utekelezaji wa jitihada za ustawi wa mazingira.

China imeahidi kutekeleza majukumu yake katika makubaliano yaliyowekwa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi licha ya kuwa Marekani haitoshiriki katika makubaliano hayo.

Akizungumza nchini Ujerumani Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang amekaririwa na vyombo vya habari vya kimataifa akisema kuwa nchi yake, inataka kuwa nchi ya kupigiwa mfano katika harakati za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo hatma ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi imeingia dosari mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu baada ya Rais wa Marekani Donald Trump  kutangaza nia ya kujiondoa katika makubaliano ya Paris ya mwaka 2015 kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Nchi saba tajiri (G7) zenye maendeleo makubwa ya viwanda na demokrasia zimekutana katika mkutano wa kilele huko Sicily nchini Italia na kwamba Kati ya viongozi wa G7 ni viongozi sita tu ndiyo wamekubaliana kuunga mkono mfumo wa makubaliano ya Paris
Marekani ambalo ni Taifa kubwa lenye viwanda vingi limekataa kuunga mkono Mkataba wa mabadiliko ya tabianchi ya Paris, yaliyotiwa saini miaka miwili iliyopita ili kupunguza hali ya joto duniani.

Kwa mujibu wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani, Kansela wa Ujeruamani, Angela Merkel amemkosoa Rais Trump wa Marekani kwa kutounga mkono makubaliano ya Paris.

“Mjadala mzima wa mabadiliko ya tabianchi ulikuwa mgumu nashangaa kuona ni kwanini Rais Trump pekee ndio hajakubaliana na makubaliano hayo’’,anasema Kansela Merkel.

Rais Mstaafu wa Marekani Barack Obama mwaka 2015 aliunga mkono makubaliano ya Paris licha ya Bunge la taifa lake kukaidi, na nchi ya China imeahidi kudhibiti uzalishaji wa hewa chafu kwa kiwango kikubwa ifikapo 2030.

Licha ya Rais Trump kujiondoa kwenye Mkataba wa Paris lakini kimsingi mataifa mawili ya Marekani na China yanaongoza kwa  kuchafua zaidi mazingira duniani, ambapo takwimu zinaonesha kuwa China inafanya uchafuzi wa mazingira kwa kutoa asilimia 30 ya hewa chafu duniani na Marekani asilimia 16.

Mataifa makubwa 20 yametangaza jitihada za kuongeza bajeti yake ya kufanya utafiti maradufu katika nishati mbadala. Bilionea mkubwa mfanyabiashara katika tasnia ya teknolojia wa Marekani Bill Gates amekwishaonesha azma ya kuunga mkono kazi hiyo ya tafiti.

Rais Mstaafu wa Ufaransa François Hollande,amekaririwa na vyombo vya habari akisema hali ya baadaye ya binadamu iko hatarini na kuonya kuwa serikali zitalaumiwa iwapo viongozi watashindwa kufanya  maamuzi muhimu  kwa kuwa kuongezeka kwa joto la Dunia kunaweza kuangamiza viumbehai wote duniani.

Tanzania tayari inaathirika na uwepo wa mabadiliko ya tabianchi ikiwemo  ukame wa muda mrefu unaojirudia rudia ambao unaambatana na athari kubwa katika kilimo, usafirishaji, nishati, biashara na sekta mbalimbali za uchumi wa jamii. 

Hivi sasa zaidi ya asilimia 70 ya majanga yote ya asili katika Tanzania yanatokana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame na mafuriko. Mifano ya matokeo ya mabadiliko ya tabianchi ipo mingi ikiwemo mafuriko yaliyotokea Dar es salaam Desemba 21 hadi 23 mwaka 2011 na kuua zaidi ya watu 40, yakiharibu nyumba nyingi na miundo mbinu. 

Matukio mengine yaliyotokea Kilosa Mkoa wa Morogoro, Singida, Kilimanjaro,Geita na Mbozi Mkoa wa Mbeya katika miaka ya 2006 na 2008 na mkoa wa Kagera mwaka 2016.

Watalaam wanasema ongezeko la joto duniani linalosababisha kuibuka kwa magonjwa mapya kwa mamilioni ya watu, hasa yale yanayoenezwa na vimelea na bacteria (vectorborn diseases) ikiwemo magonjwa kama malaria katika maeneo yenye baridi na milima ambako kwa asili hayakuwepo. 

Takwimu za Wakala wa Hali ya Hewa Tanzania, zinaonesha kuwa Wastani wa Joto kwa  mwaka katika mikoa ya  Mbeya na Iringa limeongezeka kwa nyuzi joto mbili za sentigredi katika kipindi cha miaka 50 iliyopita (1963 – 2007). 

Kwa upande mwingine, ongezeko la joto angani na upungufu wa mvua, vimeendelea kuchangia uyeyukaji wa barafu au theluji katika mlima Kilimanjaro. Inakadiriwa kuwa tangu 1912 hadi  mwaka 2015, takribani kati ya asilimia tano hadi 85 ya kiwango cha theluji katika mlima Kilimanjaro tayari imeyeyuka na kupotea. 

Inakadiriwa kuwa, kama hali ya hewa itaendelea kama ilivyo sasa, kiwango cha theluji kilichobaki katika mlima Kilimanjaro kitakwisha na kupotea kabisa hadi kufikia mwaka 2020. 

Mabadiliko ya tabianchi pia yamesababisha kuongezeka kwa usawa wa kina cha bahari, ambapo tayari kuta za kuzuia maji ya bahari zimeharibiwa na kusababisha maji kuingia maeneo ya watu katika sehemu za Pangani (Tanga) na Kunduchi Dar es Salaam). 

Ongezeko la joto pia limesababisha uzamaji wa maeneo na baadhi ya visiwa katika bahari ya India kama  vile kisiwa cha Maziwe na Fungu la Nyani na uharibifu wa maisha katika mfumo wa bahari ikiwemo mimea inayolisha na kutumika kama mazalia ya samaki kwa viumbe wa baharini. 

Tafiti mbalimbali zinazohusu mwelekeo wa joto wa muda mrefu katika ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa, zinaonesha ongezeko la joto katika maji ya kina kirefu kati ya nyuzi joto za sentigredi 0.2 mpaka 0.7 kuanzia mwanzoni mwa 1900.

Shughuli mbalimbali za binadamu zinasababisha ongezeko la viwango vya hewa ukaa inayoongeza joto kama vile carbon dioxide, methane,nitrogen dioxide, na chlorofluorocarbons.

Wataalam wa mazingira wanasisitiza kuwa udhibiti wa muda mrefu wa ongezeko la viwango vya hewa ukaa katika anga ni wa muhimu kwa sababu ndivyo vinavyosharabu mionzi inayotoka duniani na kuinasa ili kuongeza joto la dunia mpaka kiwango kinachoruhusu maisha kuendelea. 

Upunguzaji wa hewa ukaa  kwa mujibu wa wataalam ni jambo la  lazima kwa kila sekta ili kuwezesha uwezo wa mataifa yote kustahimili na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. 

Mfumo asilia wa ekolojia unatoa fursa muhimu wa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa kwa haraka na kutunza uwezo wa sayari dunia kuhimili mabadiliko ya tabianchi.Ongezeko kubwa la hewa ukaa angani linasababisha mabadiliko ya tabianchi yenye uwezo wa kuangamiza nchi mbalimbali duniani. 

Watalaam wanasema mfumo wa nishati wa dunia unahusika kwa zaidi ya nusu ya hewa ukaa yote inayozalishwa duniani. Sehemu kubwa ya hewa joto hizi ni hewa ukaa (CO2) na methane. Sehemu kubwa ya uzalishaji wa hewa joto hizi unatokana na matumizi ya mafuta ya petroli katika aina zake zote kama chanzo cha nishati. 

Kuongezeka kwa hewa ukaa angani kunasababisha kuongezeka kwa joto la anga ambalo wataalam wameridhika linahusika na mabadiliko ya tabianchi na kuleta madhara makubwa katika mazingira. 

Uchomaji na ukataji wa Misitu kwa ajili ya malisho, makazi na shughuli zingine za kiuchumi ni chanzo kingine kikubwa cha uzalishaji wa hewa ukaa angani, vitendo hivyo vinachangia takribani asilimia 16 ya uzalishaji wa hewa ukaa yote duniani. Hii ni sawa na hewa ukaa yote inayozalishwa na magari yote duniani, malori, meli, matreni na ndege vikiunganishwa pamoja.

Mwandishi ni Mchangiaji wa gazeti hili mawasiliano yake ni albano.midelo@gmail.com,Simu 0784765917.


Post a Comment