Utangulizi
Kwa kawaida,watu
wengi hapa duniani wanatafuta kitu kimoja tu, nacho ni furaha. Lakini tatizo
lipo katika kutambua ipi ni furaha ya kweli
na njia ya kuipata furaha hiyo.
Wengi katika dunia hii wanaofikiri furaha hupatikana kwa
kuwa na mali
nyingi. Wengine wanafikiri kufikia kilele cha maendeleo ni furaha. Walio wengi
wanafikiri kuishi maisha marefu ni furaha, La hasha !.
Hao wote wamedanganyika kwani furaha inayopatikana katika
mambo hayo yote, yaonekana haiwaridhishi. Mara kwa mara tunaona wale wenye mali mengi,
ndio wenye mahangaiko zaidi, kuliko wale
ambao hawana. Wenye maendeleo ya juu ndio walioridhika zaidi kuliko wale wenye
maendeleo ya chini.
Itakuwa wamesahau usemi wa mtakatifu Augustino usemao: “Moyo wangu hautapumzika kwa
raha hadi utakapokaa katika wewe, Ee Bwana!”. Kile tu kisicho na mwisho ndicho
kitachompa mtu furaha ya kweli, vitu vingine vitamsaidia tu kupata furaha.
Mtunga Zaburi anatuambia: “furaha yangu imo katika Mungu
(Zab 104:34). Kazi yetu sisi wanadamu ni kulenga shabaha ya kuipata furaha hiyo
ya kweli ambayo ni kuunganika na Mungu aliye chanzo cha furaha yote.
Biblia na matumizi ya
neno ‘furaha’.
Katika Agano la Kale pamoja
na Agano Jipya hutumika maneno
mbali mbali ya kuonyesha aina nyingi za
furaha, ukunjufu,uradhi na shangwe. Furaha ni tabia ya Mungu, naye anataka iwe
tabia na alama ya wazi katika viumbe vyake, hasa kwa watu wake ( Ayu 38:7, Zab
16 :11,104:31, Lk 2:10,14,Yn 15:11, Flp
4:4)
Ukunyufu na furaha ni sehemu ya maisha ya kila siku anayotazamia kwa wanadamu. Mungu anataka watu
wamfurahie yeye na mambo yote aliyowapa
kwa uzima wao katika dunia hii (Kum 14:26,Mhu 5:18-19, 9:7-9, Lk 1:14,
15:22-24, Tim 6:17). Lakini mambo yote hayo ya kufurahia lazima yaunganishwa na
tabia safi na nidhamu
binafsi (Mit 24:16-21, Amo 6:4-7, Rum 13:13, 14:17, 1Thes 5:7-8, Pet 4:3).
Furaha kama alama ya
ibada ya hadhara katika Israeli ya Kale
Maonyesho ya furaha na ukunyufu yalikuwa ni alama ya ibada
ya hadharani katika Israeli ya Kale ( Kumb 12:5-7, Zab 81:1-3, 100:1-2,
150:3-6). Pia yalikuwa alama ya maisha ya Kanisa la kwanza ( Mdo 2:46-47, 5:41,
8:39, 13:52, Kol 3:16).
Furaha ya pekee kwa Wakristo ni kuunganika na Kristo kwa njia ya imani
Furaha katika maana ya pekee waumini katika upande wa Mkristo
wanayo, iwapo kwa imani yao huunganika sana na Yesu Kristo ( Yoh
15:4,11). Furaha ya namna hii ni zaidi
kuliko kujisikia kuwa na hali njema kama mambo yote yanakwenda vizuri. Furaha ya namana hii huwa ya muda mfupi (Mhu:1-11).
Furaha inayotolewa na Yesu Kristo haiwezi kuondolewa na hali
ya maisha ( Yoh 16:22-33, 17:13,Rum 15:13). Ni hali ya amani na nguvu inayomwenzesha mwamini afurahi hata katika matatizo na huzuni ( Hab
3:17-18, Mt 5:10-12, Zkor 6:10, kol 1:24, Yak 12).
Dhambi miongoni mwa waumini huharibu mazoea ya
furaha ya Mungu.
Dhambi katika maisha ya waumini inaweza kuharibu mazoea ya
furaha ambayo Mungu aliwapa. Kwa sababu hii hawana budi kukataa dhambi pamoja na maelekeo yake ya kukata tamaa inayofuatana
na dhambi. Wanapaswa kufanya bidii ya moyo
mzima na siku zote kuwa watu wa furaha pasipo mashaka wakati wote (Flp
4:4,Thes 5:16-18)
Kukua kwa wakristo
katika maisha mapya
Kwa kadiri ya waumini wanavyokua katika maisha yao mapya katika
Kristo, ndivyo Roho wa Kristo anaekaa ndani yao,
anavyozidi kujenga tabia hiyo ya furaha ndani yao (Gal 5 :22). Furaha hiyo haiwezi kutengwa
na imani, upendo, amani na matumaini (Ram 5:1-5, 15:13, 1Thes 1:3, 6, Ebr
10:34).
Utimilifu wa furaha yao utakuwa kumkuta Yesu Kristo wakati
wa kurudi kwake, wakiingia pamoja nae katika furaha kamili ya wakati ujao (Isa
65:17-19, Mt 25:21, Yuda 24, Ufu 19:7-9). Matumaini haya yenye utukufu ni
sababu nyingine ya furaha yao
katika matatizo na mateso ya siku (Rum 5:2, 8:18, 24, I Pet 1:6-8, 4:13)
Hitimisho
Mpango wa maisha yetu ya kikristo
yamepimwa katika maandiko matakatifu.
Katika ukurasa ule ule mmoja 394 ya Biblia Takatifu , kitabu cha Nehemia au 2 Ezra, zimeandikwa habari hizi
katika sura ya 9: “Waana wa Israeli
wakawa wanakusanyika, walifunga wenye
kuvaa magunia na kujitia udongo vichwani…….wakaziungama dhambi zao na maovu ya Baba zao.
Wakasoma katika kitabu cha Torati ya Bwana Mungu wao, katika muda wa robo siku, na robo
nyingine wakaungama, wakamwabudu Bwana.
Lakini katika sura ya Nane kiongozi wao Ezra alikuwa
amewaambia: (Nehemia 8:10) siku hii ni
takatifu kwa Bwana wala msihudhunike, kwa kuwa “Furaha” ya Bwana ni nguvu zetu.
Mungu mwenyewe ni furaha. Kati ya nafsi tatu Roho Mtakatifu
hutajwa kama furaha ya Mungu. Mungu kwa asili
ni shangilio.
Alipoumba dunia mwisho wa kila siku , alionyesha furaha yake
yaani “Mungu akaona ya kuwa ni vyema “(Reje. Mwa 1:31). Dhambi ilipokuwa
imeingia ulimwenguni humu, Mungu
hakuweza kuendelea kusikitika , au aliweka upinde wa mvua kama alama
ya furaha “Mimi nauweka upinde wangu wa mvua mawinguni, nao ni ishara ya Agano,
kati yangu na nchi nami nitawaangalia, nipate
kukumbuka Agano la milele” (Mwa 9:13-16)
Bwana Yesu analikazia wazo hilo
akisema: Baba yetu aliye mbinguni huwangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio
na haki (Taz Lk 6:35).
Furaha ni ukamilifu mmojawapo wa Mungu, naye Yesu alisema:
ninyi mtakuwa watakatifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyomkamilifu.
Furaha ni ukamilifu mmoja wapo wa wakristu. Lakini msingi wa
kushiriki furaha hiyo ya Mungu ni kuzishika amri zake .“ kama
vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia ili furaha yangu iwe ndani yenu,
na furaha yenu itimizwe (Yoh 15:10-11).
Kat.George
Milinga
Parokia
ya Prahimo.
Post a Comment