Ads (728x90)

Powered by Blogger.





Moja ya siku ambazo hazitasahaulika na Wanaparokia ya Peramiho ni siku ya Tarehe 16, Novemba mwaka huu 92016), siku ambayo ilikuwa maalumu ya kuhitimisha kilele cha Jubilei ya mwaka wa Huruma ya Mungu ambayo ilipambwa kwa vifijo, shangwe na Nderemo.

 Siku hiyo ambayo ilitangazwa na Baba Mtakatifu Francis, mnamo tarehe 15, Desemba 2015 ikiwa ni sikukuu ya kukingiwa Mama Bikila Maria dhidi ya dhambi ya asili, mwisho wake na tarehe 20, Novemba 2016, ikiwa ni sikukuu ya Yesu Kristo Mfalme inayoadhimishwa na Wakristo wote duniani ikiongozwa na Papa.

Waumini toka vigango vyote ya Peramiho wakiongozwa na Mapadre, Makatekista pamoja na viongozi wao walihudhuria maandamano hayo yaliyong’oa  nanga katika viwanja vya michezo vya shule ya ufundi Peramiho, huku wakiimba nyimbo za kumsifu Mungu na baadaye walinyunyizwa maji ya baraka toka kwa Paroko wa Kanisa la Peramiho.

Sakramenti ya kitubio au toba ni sehemu ya maisha ya Mkatoliki, hivyo siku hiyo adhimu ya kumsifu Mungu,  kabla ya Misa takatifu waumini walipata fursa ya kutubu dhambi zao ili kujisafisha kabla ya hitimisho la mwaka wa huruma.

Katika Misa ambayo iliongozwa na Naibu Askofu wa Jimbo kuu la Songea, Padre Kamilius Haule akisaidiana na Padre Stefano Komba OSB, Damas Chale pamoja na Mseminari Fredrick Mwabena OSB,alifafanua haya katika mahubiri yake:

“Wanaperamiho kuweni na huruma kama Baba alivyokuwa na Huruma (Lk 6:36), napongeza utaratibu mzuri uliowekwa na Parokia ya Peramiho katika kuhitimisha mwaka wa huruma kwa amani na upendo”

“Swali la kwanza katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki huuliza: tupo duniani kwa kusudi gani? Jibu, ni tupo duniani ili tumjue Mungu, tumpende, tumtumike na tufikie ufalme wake wa mbinguni. Ndio maana tunamwita ni Mungu Mfalme, hata Bwana wetu Yesu Kristo huitwa ni Mfalme kwa kuwa yeye ni mwokozi wetu”

“Mungu alimuumba mtu kwa mapendo  yake na huruma yake tu: mtu angeweza kuumbwa kitu kingine kama vile Nguruwe hata Mdudu lakini ameumbwa kuwa mtu kwa sababu ya huruma yake”

“Mtu ukiwa na mali,watoto au kazi nzuri; uwe ni Mtawa, Padre, Daktari au Mwanandoa usijivune bure, maana yote hayo ni kwa huruma ya mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na dunia na viumbe vyote vinavyoonekana na visivyoonekana”

“Mungu alimuumba mtu kwa mapendo yake: kupumua kwetu na kutenda kwetu kupo ndani ya Mungu mwenye huruma. Binadamu hana lolote lile, leo yupo kesho hayupo, mwanadamu ameumbwa na Mola, bila yeye hawezi kufanya lolote, binadamu ni wakuagizwa na kutekeleza” alifafanua Haule kisha akaendelea.

Sakramenti ya Ubatizo

“Tuwabatize watoto wetu katika Kanisa ili wapate Sakramenti ya Ubatizo, kwa kuwa Kanisa linamzaa mtoto kiimani kwa ubatizo, baada ya kuzaliwa kimwili toka kwa Baba na Mama”

Sakramenti ya kitubio

“Waumini waungame dhambi zao katika Sakramenti ya kitubio kupitia kwa Padre kwani mpango huo uliwekwa na Mungu kwa ajili ya wokovu. Watu wasifuate upotoshaji wa madhehebu  kwa kuwa Padre aliwekwa na Yesu na si Malaika ambaye hajui hali halisi ya ubinadamu ulivyo, tuongee na Mungu kupitia kitubio na sala ili tufike Mbinguni vinginevyo tutaenda motoni”.

“Watu wengi wanaona aibu kuungama dhambi zao kwa Padre, mbona daktari unamwonesha hata sehemu za siri ili kupona ugonjwa wako? Sembuse dhambi kwa Padre ambayo ni mbaya zaidi ya ugonjwa?”

“Tusifungwe na shetani ambaye nia yake ni kutupeleka motoni, Adam alipata mke baada ya kutoka usingizini ni huruma ya Mungu, tufungue mioyo yetu kupokea huruma ya Mungu na kuwasaidia wengine wenye shida ya uokovu” alisisitiza Haule.

Adhimisho hilo la kufunga mwaka wa huruma liliambatana na matukio mbali mbali ikiwemo tukio la ubatizo kwa watu 34, Kipaimara watu 62 huku Ndoa  Nane zikifungwa kwa kufuata taratibu zote za Kanisa.

Vile vile kulikuwa na tukio la wanajubilei wa ndoa pea moja ambao walitimiza miaka 40, Jubilei ya miaka 60 pea moja na Jubilei ya miaka 50 pea moja,  kisha watu wawili walimshukuru mungu kwa kutimiza miaka 60 akiwemo Paroko wa Kanisa la Peramiho Padre Joseph Ndimbo.

Imeandaliwa na

Kat. George Millinga na

Alex Mapunda,

Peramiho.


Post a Comment