Halmshauri ya
manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imeendelea kupokea fedha kwa ajili ya mpango
wa kunusuru kaya masikini kupitia mradi
wa TASAF awamu ya tatu lengo likiwa ni kupunguza umaskini kwa watu wasiojiweza.
Ofisa habari wa
manispaa ya Songea Albano Midelo alisema hadi kufikia mwezi Mei mwaka 2016 zaidi ya shilingi
bilioni moja na milioni 628 zilikuwa zimepokelewa ingawa mwezi Mei,2016
haikupolewa fedha yoyote kwa ajili ya kaya masikini.
Takwimu za mapokezi
ya fedha za TASAF awamu ya tatu kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa kunusuru
kaya masikini zinaonesha kuwa kuanzia Julai 2015 hadi Mei 2016 zaidi ya
shilingi bilioni 1.628 zilipokelewa na
zimeendelea kutolewa kwa kaya masikini za wakazi wa mitaa 95 ya manispaa ya
Songea.
Awamu ya tatu ya TASAF ilizinduliwa rasmi Agosti 2012
Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete ambapo Mpango wa kunusuru Kaya Maskini unatekelezwa
ili kujenga uwezo na kuwezesha kaya Maskini kuongeza kipato, fursa na uwezo wa
kugharamia mahitaji muhimu na kuboresha maisha.
Kwa mujibu wa Ofisa habari wa manispaa ya Songea,Katika
Halmashauri ya Manispaa ya manispaa hiyo uzinduzi wa TASAF awamu ya tatu
ulifanyika Januari 5 mwaka 2015 ambapo uzinduzi ulifanywa na mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu.
Amesema Katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka
2015/2016 kazi mbalimbali zimeendelea kufanyika ambazo ni kulipa kaya maskini
7,828 kati ya lengo la kaya 7,915 zilizopo kwenye mpango, ambapo kaya 88
hazikutokea siku ya malipo hivyo fedha zao kurudishwa TASAF Makao makuu
kulingana na utaratibu.
Ili kuhakikisha kuwa TASAF awamu ya tatu inafikia
,malengo yake mfuko umetoa mafunzo kwa Watendaji wa Kata, Wauguzi, Walimu wa
Shule za Msingi na Sekondari kuwajengea uelewa watumishi hao ili wasaidie
katika kuondoa umaskini hasa katika kufuatilia masharti ya elimu na afya.
Mfuko pia umelenga kutoa elimu kwa kaya maskini
(wananchi) kuhusu kilimo cha mazao mbadala ambayo hayatumii mbolea za viwandani.wananchi
hao masikini walifundishwa kilimo cha mazao ya maharagwe, karanga,
alizeti,ndizi, mtama.
Wananchi hao masikini walifundishwa kuandaa mbolea ya
asili. Mafunzo haya yalifanyika mwaka 2015 katika mitaa ya manispaa ya Songea
ikiwemo Mitaa ya Lilambo A, Mwanamonga na Sinai kata ya Lilambo,
Mitendewawa,Chandarua na Muhumbezi kata ya Mshangano,Mletele,Nonganonga na Mdundiko
kata ya Mletele, Tanga na Mlete kata ya Tanga,Ndilimalitembo, Mahilo na
Chemchem.
Hata hivyo Timu ya ufuatiliaji ya Wilaya na Mkoa
ilifanya ziara kwenye mitaa minne ya
Mwengemshindo,Luhira kati, Mitendewawa na Chandarua ili kusikiliza kero za
wanufaika wa kaya masikini na kuzitatua.
Uchunguzi umebaini kuwa mpango wa TASAF wa kuzinusuru
kaya masikini umeleta mafanikio ikiwemo
kuimarika kwa mahudhurio ya watoto shule za Msingi na Sekondari, kuongezeka kwa
mahudhurio ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kliniki na wanufaika
wengi kuanza kujiunga na Mfuko wa Afya wa Jamii.
Baadhi ya wakazi wa manispaa ya Songea wameipongeza
Serikali kwa kuanza mpango huo wa TASAF awamu ya tatu ambao wamesema utaleta manufaa kwa Kaya maskini na
kusisitiza tangazo la siku ya malipo liwe linatolewa mapema ili kila mnufaika
apate malipo kama inavyostahili, pia kwa Walengwa ambao watathibitika kuwa na
matatizo kwa siku za malipo, uandaliwe utaratibu maalum wa kuwalipa.
Katika hatua nyingine
Taarifa ya idara ya fedha ya manispaa ya Songea inaonesha kuwa matumizi ya fedha za maendeleo kuanzia Julai
2015 hadi Mei 2016 yalikuwa ni zaidi ya
shilingi bilioni nne na milioni 179.
Mchanganuo wa fedha
hizo unaonesha kuwa zaidi ya shilingi milioni 33 zilitumika kwa ajili ya
mipango,mfuko wa barabara zaidi ya shilingi milioni 560 na Benki ya Dunia zaidi
ya shilingi bilioni moja na milioni 581.
Matumizi mengine ni
maji zaidi ya shilingi milioni 72,mfuko wa jimbo zaidi ya shilingi milioni nne,mfuko wa afya
zaidi ya shilingi milioni 102,SEDP zaidi ya shilingi milioni 186 na mfuko wa
TASAF awamu ya tatu zaidi ya shilingi bilioni moja na milioni 638.
Halmashauri ya manispaa ya Songea katika mwaka wa fedha
wa 2015/2016 iliidhinishiwa na Bunge kukusanya na kutumia zaidi ya shilingi
bilioni 44 na milioni 937 kuanzia Julai 2015 hadi Mei 2016 ambapo mapato halisi yalikuwa ni zaidi ya shilingi bilioni 33 na
milioni 152 sawa na asilimia 73 ya makisio kwa mwaka.
Mwisho
Post a Comment