Ads (728x90)

Powered by Blogger.





Image result for MUNGU


Utangulizi
  
Kwa  kawaida,watu wengi hapa duniani wanatafuta kitu kimoja tu, nacho ni furaha. Lakini tatizo lipo katika kutambua ipi ni furaha ya kweli  na njia ya kuipata furaha hiyo.

Wengi katika dunia hii wanaofikiri furaha hupatikana kwa kuwa na mali nyingi. Wengine wanafikiri kufikia kilele cha maendeleo ni furaha. Walio wengi wanafikiri kuishi maisha marefu ni furaha, La hasha !.

Hao wote wamedanganyika kwani furaha inayopatikana katika mambo hayo yote, yaonekana haiwaridhishi. Mara kwa mara tunaona wale wenye mali mengi, ndio  wenye mahangaiko zaidi, kuliko wale ambao hawana. Wenye maendeleo ya juu ndio walioridhika zaidi kuliko wale wenye maendeleo ya chini.

Itakuwa wamesahau usemi wa mtakatifu  Augustino usemao: “Moyo wangu hautapumzika kwa raha hadi utakapokaa katika wewe, Ee Bwana!”. Kile tu kisicho na mwisho ndicho kitachompa mtu furaha ya kweli, vitu vingine vitamsaidia tu kupata furaha.

Mtunga Zaburi anatuambia: “furaha yangu imo katika Mungu (Zab 104:34). Kazi yetu sisi wanadamu ni kulenga shabaha ya kuipata furaha hiyo ya kweli ambayo ni kuunganika na Mungu aliye chanzo cha furaha yote.

Biblia na matumizi ya neno ‘furaha’.

Katika Agano la Kale pamoja  na Agano Jipya  hutumika maneno mbali mbali ya kuonyesha  aina nyingi za furaha, ukunjufu,uradhi na shangwe. Furaha ni tabia ya Mungu, naye anataka iwe tabia na alama ya wazi katika viumbe vyake, hasa kwa watu wake ( Ayu 38:7, Zab 16  :11,104:31, Lk 2:10,14,Yn 15:11, Flp 4:4)

Ukunyufu na furaha ni sehemu ya maisha ya kila siku  anayotazamia kwa wanadamu. Mungu anataka watu wamfurahie yeye na mambo yote aliyowapa  kwa uzima wao katika dunia hii (Kum 14:26,Mhu 5:18-19, 9:7-9, Lk 1:14, 15:22-24, Tim 6:17). Lakini mambo yote hayo ya kufurahia lazima yaunganishwa na tabia safi na nidhamu binafsi (Mit 24:16-21, Amo 6:4-7, Rum 13:13, 14:17, 1Thes 5:7-8, Pet 4:3).

Furaha kama alama ya ibada ya hadhara katika Israeli ya Kale

Maonyesho ya furaha na ukunyufu yalikuwa ni alama ya ibada ya hadharani katika Israeli ya Kale ( Kumb 12:5-7, Zab 81:1-3, 100:1-2, 150:3-6). Pia yalikuwa alama ya maisha ya Kanisa la kwanza ( Mdo 2:46-47, 5:41, 8:39, 13:52, Kol 3:16).

 Furaha ya pekee kwa Wakristo ni kuunganika na Kristo kwa njia ya imani

Furaha katika maana ya pekee waumini katika upande wa Mkristo wanayo, iwapo kwa imani yao huunganika sana na Yesu Kristo ( Yoh 15:4,11). Furaha ya namna hii  ni zaidi kuliko kujisikia  kuwa na hali njema kama mambo yote yanakwenda  vizuri. Furaha ya namana  hii huwa ya muda mfupi (Mhu:1-11).

Furaha inayotolewa na Yesu Kristo haiwezi kuondolewa na hali ya maisha ( Yoh 16:22-33, 17:13,Rum 15:13). Ni hali ya amani  na nguvu inayomwenzesha mwamini  afurahi hata katika matatizo na huzuni ( Hab 3:17-18, Mt 5:10-12, Zkor 6:10, kol 1:24, Yak 12).

 Dhambi miongoni mwa waumini huharibu mazoea ya furaha ya Mungu.

Dhambi katika maisha ya waumini inaweza kuharibu mazoea ya furaha ambayo Mungu aliwapa. Kwa sababu hii hawana budi kukataa dhambi  pamoja na maelekeo yake ya kukata tamaa inayofuatana na dhambi. Wanapaswa kufanya bidii ya moyo  mzima na siku zote kuwa watu wa furaha pasipo mashaka wakati wote (Flp 4:4,Thes 5:16-18)

Kukua kwa wakristo katika maisha mapya

Kwa kadiri ya waumini wanavyokua katika maisha yao mapya  katika Kristo, ndivyo Roho wa Kristo anaekaa ndani yao, anavyozidi kujenga tabia hiyo ya furaha ndani yao (Gal 5 :22). Furaha hiyo haiwezi kutengwa na imani, upendo, amani na matumaini (Ram 5:1-5, 15:13, 1Thes 1:3, 6, Ebr 10:34).

Utimilifu wa furaha yao utakuwa kumkuta Yesu Kristo wakati wa kurudi kwake, wakiingia pamoja nae katika furaha kamili ya wakati ujao (Isa 65:17-19, Mt 25:21, Yuda 24, Ufu 19:7-9). Matumaini haya yenye utukufu ni sababu nyingine ya furaha yao katika matatizo na mateso ya siku (Rum 5:2, 8:18, 24, I Pet 1:6-8, 4:13)


Hitimisho

Mpango wa maisha yetu ya    kikristo yamepimwa katika  maandiko matakatifu. Katika ukurasa ule ule mmoja 394 ya Biblia Takatifu , kitabu cha  Nehemia au 2 Ezra, zimeandikwa habari hizi katika sura ya 9: “Waana wa  Israeli wakawa wanakusanyika,  walifunga wenye kuvaa magunia na kujitia udongo vichwani…….wakaziungama dhambi zao na  maovu ya Baba zao.

Wakasoma katika kitabu cha Torati ya Bwana Mungu  wao, katika muda wa robo siku, na robo nyingine wakaungama, wakamwabudu Bwana.

Lakini katika sura ya Nane kiongozi wao Ezra alikuwa amewaambia: (Nehemia  8:10) siku hii ni takatifu kwa Bwana wala msihudhunike, kwa kuwa “Furaha” ya Bwana ni nguvu zetu.

Mungu mwenyewe ni furaha. Kati ya nafsi tatu Roho Mtakatifu hutajwa kama furaha ya Mungu. Mungu kwa asili ni shangilio.

Alipoumba dunia mwisho wa kila siku , alionyesha furaha yake yaani “Mungu akaona ya kuwa ni vyema “(Reje. Mwa 1:31). Dhambi ilipokuwa imeingia ulimwenguni  humu, Mungu hakuweza kuendelea kusikitika , au aliweka upinde wa mvua  kama alama ya furaha “Mimi nauweka upinde wangu wa mvua mawinguni, nao ni ishara ya Agano, kati yangu na nchi  nami nitawaangalia, nipate kukumbuka Agano la milele” (Mwa 9:13-16)

Bwana Yesu analikazia wazo hilo akisema: Baba yetu aliye mbinguni huwangazia jua lake waovu  na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio na haki (Taz Lk 6:35).

Furaha ni ukamilifu mmojawapo wa Mungu, naye Yesu alisema: ninyi mtakuwa watakatifu  kama Baba yenu wa mbinguni  alivyomkamilifu.

Furaha ni ukamilifu mmoja wapo wa wakristu. Lakini msingi wa kushiriki furaha hiyo ya Mungu ni kuzishika amri zake .“ kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo  nimewaambia ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe (Yoh 15:10-11).


                                                                        Kat.George Milinga
                                                                        Parokia ya Peramiho.









Post a Comment