Ads (728x90)

Powered by Blogger.




Ansgar Cup ni moja ya mashindano yenye msisimko mkubwa mkoani Ruvuma, watu wengi wanaifahamu Ansgar cup kwa hoja za ukongwe wa mashindano, usimamizi, waamuzi pamoja na upinzani uliopo kwa timu shiriki toka Kata mbali mbali.

Kwa mwaka huu, timu ya Lilambo Fc imefanikiwa kunyakua ubingwa wa Ansgar Cup 2017 ngazi ya Tarafa mara baada ya kuifunga Peramiho (Afya Fc) bao 2-1 katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye dimba la Ansigar Peramiho B.

Timu ya Lilambo ilianza kuofiwa toka katika hatua ya makundi, kwa kuwa walikuwa wakitandaza kandanda safi la kitabuni, hivyo walikuwa wakibadilika katika kila mchezo kisha wakaingia fainali kwa kishindo baada ya kuifunga kilagano kwa jumla ya bao 3-0.

Katika mchezo huo wa fainali ambao ulikuwa wa vuta nikuvute mabao ya Lilambo Fc yalifungwa na Mohamed Msigwa pamoja Ibrahim Ally wakati lile la kusawazisha la Afya Fc lilifungwa na John Chihonda kwa mkwaju wa penati.

Mshindi wa kwanza ambaye ni Lilambo alipewa zawadi ya Kombe na  shilingi 400,000/=, mshindi wa pili ambaye ni Afya Fc  shilingi 300,000 huku washindi wa tatu Maposeni Fc wakiondoka na kitita cha shilingi 200,000/= (kwa michezo yote Soka na Pete). 

Mwaka huu zawadi ya mfungaji bora imechukuliwa na wachezaji wawili ambao ni Shabiru Kinunga (Peramiho) pamoja na Mohamed Msigwa (Lilambo) na wote waliondoka na  kifuta jasho cha shilingi 50,000/= baada ya kila mmoja kupachika bao sita. 

Kwa upande wa akinamama timu ya Afya Fc imechukua ubingwa katika mpira wa pete, wakati Lilambo Fc imeshika nafasi ya pili huku Maposeni Fc ikishika nafasi ya tatu. Michezo mengine ilikuwa ni kuvuta kamba, kukimbiza kuku pamoja na kukimbia ndani ya Magunia.

Fainali hiyo iliyohudhuriwa na Mdhamini wa Mashindano hayo  ambaye ni Mkurugenzi wa Hospitali ya Peramiho Dr. Bro. Ansgar Stuffe OSB ilifanyika  tarehe Nne Mwezi Juni katika uwanja wa Mdhamini huyo na kuzikutanisha timu ambazo zilionekana kufanana kiuchezaji toka Mpira wa miguu hadi wa Pete.

Aidha baadhi ya wachezaji  waliofanya vizuri katika mashindano hayo uenda wakapata fursa ya kwenda kufanya majaribio katika timu ya Mtibwa Sugar kutoka Tuliani Manungu (Morogoro) kwa kuwa Msemaji wa mtibwa Sugar Tobias Kifaru alihudhuria mashindano hayo na alihaidi kuondoka na baadhi ya wachezaji wenye uwezo. 

wasimamizi wa mashindano hayo walijitahidi kusimamia vizuri kwa asilimia kubwa kwa kuweka ulinzi wa kutosha, waamuzi wazuri n.k. lakini bado kuna mambo machache yanahitaji maboresho ili kuongeza ufanisi na ubora wa mashindano:

  Sare za Mashindano

Sare za viongozi wa mashindano ziandaliwe mapema ili waanze kuzitumia toka mwanzoni mwa ligi ili kuepusha matumizi ya sare za miaka ya nyuma. kama jina la mashindano ni ANSGAR CUP PERAMIHO 2017 wakati wasimamizi wa mashindano wamevaa sare zenye maandishi yanayosomeka ANSGAR CUP PERAMIHO 2016 huko ni kuwachanganya mashabiki na wapenzi wa Ansgar Cup.

Usajili wa wachezaji

Usajili wa wachezaji uwe wa uhakika kwa asilimia 100, ikiwezekana picha zinazowekwa kwenye kadi za wachezaji zisiwe za kubandika na gundi, ziwe za moja kwa moja ili kuepusha baadhi ya viongozi wa timu wenye tatizo la uaminifu kubandua picha hizo na kubandika picha za wachezaji mamruki.

   Ushangiliaji

Kama sheria inasema timu ikifunga bao mashabiki wasiingie uwanjani kuna haja ya kusimamia utaratibu huo kwa vitendo, wanaokiuka wachukuliwe hatua stahiki. Vile vile uzio wa uwanja ueshimiwe watu wasiingee hadi kwenye eneo la kuchezea (Pitch), pia eneo la jukwaa kuwa pawepo na ulinzi wa kutosha ili kulinda bechi la waamuzi, timu, waandishi wa habari na viongozi mbali mbali.

   Hat- Trick

Kutokana na ukubwa wa mashindano ingefaa mchezaji mmoja akifunga bao tatu yaani “Hat- Trick” kwenye mchezo husika basi aondoke na mpira wake kama sheria za soka zinavyosema. Tunaomba viongozi waboreshe suala hilo ili kuongeza chachu ya mashindano.

   Mapumziko

Sheria ya soka inasema baada ya dakika 45 timu zinatakiwa ziingie vyumbani na kupumzika kwa takribani dakika kumi na tano, sina uhakika kama Ansgar cup ilikuwa ikizingatia suala hilo. Naomba lifanyiwe kazi.

Kama muda wa kuanza ni saa nane kamili ni vyema kuanza muda huo, timu ikichelewa sheria zipo zifuate mkondo wake. Wapo mashabiki ambao wanakwenda sambamba na muda mechi ikichelewa kuanza ratiba zao zinaingiliwa.

Kata zilizojitosa katika mashindano ya mwaka huu ni Kata ya Peramiho, Litisha, Parangu, Kilagano, Lilambo, Maposeni, Mpandangindo pamoja a  Liganga ambapo mechi zote ngazi ya Tarafa zilipigwa kwenye uwanja wa Ansgar uliopo Peramiho B kwa kuwakutanisha mabingwa waliofanya vizuri katika Kata husika.

Ansgar cup ni moja ya ligi kongwe mkoani Ruvuma na imedumu kwa zaidi ya miaka 20, lengo kubwa la mashindano ya  ni kuibua vipaji kwa wachezaji, burudani baada ya kazi, kuongeza soko la biashara kwa wafanyabiashara wa tarafa ya Peramiho n.k. 

Baadhi ya wachezaji waliotokea Ansgar Cup ni pamoja Pato Ngonyani (Maji Maji, na Yanga), Anold Nguruchi na wengine wengi.


Post a Comment