Ads (728x90)

Powered by Blogger.



Image result for kunena kwa lugha

UTANGULIZI
Baadhi ya madhehebu ya Kikiristo yasiyo ya imani Katoliki hudai kuwa Makanisa yasiyoweza kudhihirisha “Karama ya Unenaji wa Lugha” hayo siyo Makanisa ya kweli na wala hayana Roho Mtakatifu, kwa kuwa Yesu aliwapa mitume karama hiyo katika Kanisa. Mafundisho ya imani Katoliki hutuambia kwamba mtu mwenye Roho Mtakatifu anakuwa na vipaji saba ambavyo ni Hekima, Akili, Elimu, Shauri, Nguvu, Ibada na Uchaji wa Mungu (Isaya 11:2).

Vile vile mtu huyo, huwa katika hali ya ukubali wa kuongozwa na Roho huyo wa Mungu. Mtu huyo mwenye Roho Mtakatifu huyadhihirisha na kuyaonyesha hayo katika matunda ya Roho ambayo ni tabia ya Kikristo yaani upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi (Gal 5:22-23).

Kunena kwa lugha ni ishara ya kuwa na Roho Mtakatifu (IKor 14:22) kwa baadhi ya watu tu (I Kor 12:30)  kama zilivyo karama nyingine tena ni kipawa kidogo na cha mwisho, kwa maana ni kipawa pekee kisichofaidia wengine moja kwa moja (I Kor 14:2,4-6,9,11,13,27,,28,39).

Kadiri ya mtume Paulo tunapaswa kutoka na kuomba vipawa vya kufaidiana na hasa “upendo” karama ambayo kila mmoja inampasa kuwa nayo (I Kor 12:31, 13:8, 14:1). Kanisa Katoliki hutusimulia kuwa, hapo mwanzo wa Kanisa waumini au watu walihitaji sana ili kuamini kweli wamepokea Roho Mtakatifu.

Siku hizi hatuhitaji sana  ishara ili kuamini (labda kwa wenye mioyo migumu sana)  ila tu kwa ajili ya kuondolewa vikwazo vinavyotuzuia kumpenda na kumtumikia Mwenyezi Mungu na kupata uokovu wa milele. Hata hivyo Kanisa Katoliki hutuambia kuwa baadhi ya wale walio katika Chama cha Karismatiki Katoliki hudhihirisha karama hii. Mimi binafsi naonelea si vizuri sana kung’ang’ania na kupendelea vitu tusivyovielewa vizuri wala kuthibitisha kuwa vimetoka kwa Mungu, bali mapenzi ya Mungu yatendeke.

Bado Kanisa Katoliki katika Mafundisho yake ya imani huvitambua na kuvikiri vipaji vyote vya Roho Mtakatifu walivypewa watu na vinavyofanya kazi kati ya watu au waumini. Aidha kadiri ya mafundisho Katoliki tunaambiwa kuwa ni balaa pia ni ufinyu, vile vile ni upotoshaji wa imani kwa waumini kama waamini wanakitambua kipaji kimoja tu cha unenaji wa lugha. Kwa sababu Roho Mtakatifu aliye Mungu ni tajiri wa vipaji. Huko ni kumdharau Mungu , hata kumkufuru na kumfanya kuwa fukara wa vipaji, hiyo pia ni dhambi.

Bado mafundisho ya imani Katoliki hutuambia kuwa wakati Yesu alipoanzisha Kanisa aliweka alama nne ili lijulikane kuwa la kweli nazo ni “Moja”, “Takatifu”, “La”, “Mitume” na kuweka alama za wokovu zinazoleta neema ili kutufikisha mbinguni  ambazo uitwa “Sakramenti Saba” nazo ni Ubatizo, Kipaimara, Ekaristi Takatifu, Kitubio, Mpako Mtakatifu, pia Daraja Takatifu na Ndoa.
Sababu hiyo Kanisa Katoliki linatuunganisha kutosikiliza lugha za upotoshaji au kuhangaishwa na vikundi vinavyopotosha dhana ya unenaji wa lugha na kufikiri Roho Mtakatifu hukaa kwa mtu mwenye kunena kwa lugha tu.


SIKUKUU YA PENTEKOSTE NA UNENEAJI WA LUGHA KWA MITUME

Sikukuu ya Pentekoste ilikuwa ni sikukuu ya shukrani ya Wayahudi kwa ajili ya mavuno ya nafaka. Iliadhimishwa siku ya Hamisini yaani majuma saba baada ya Pasaka. Wakati huo nafaka ilishavunwa katika Palestina. Sikukuu ya Pendekoste ya Kikristo inaadhimishwa kwa ukumbusho wa kujaliwa Mitume Roho ya Kimungu. “Mvumo wa Upepo” kutoka mbinguni ni ishara kwamba Roho inawashukia mitume  ambayo ni nguvu ya Mungu iliyo kubwa sana. “Ndimi za Moto” zinaonyesha kuwa nguvu hiyo inawahimiza mitume kusema na kuungama. Zile “lugha ngeni” ambazo wanazisema sio lugha za kigeni ila “maneno na sentensi za mafumbo ya lugha yao wenyewe zinazotangaza na kuyasifu matendo makuu ya Mungu”

Wasikilizaji wengine hawakufahamu yanayosemwa na mitume, kwa sababu hiyo walidhihaki na kusema kuwa mitume wamelewa (Taz. Mdo 2:15). Wengine wanaojaliwa na Roho walifahamu pia maana ya maneno ya mafumbo waliyoyasikia. Wayahudi wale kutoka nchi zote ni Wayahudi waliolelewa ugenini na kuja kuhiji Yerusalemu tangu siku nyingi. Kufahamu maneno ya mitume kwa lugha yao ilikuwa ni Miujiza, inaonyesha kuwa Mungu ameleta habari njema kwa ajili ya ulimwengu wote. Kumega mkate kulikotajwa hapo maana yake ni karamu katika shirika la kidugu au labda sherehe ya Ekaristi Takatifu.

MAANA YA KUNENA KWA LUGHA KADIRI YA KITABU CHA MATENDO YA MITUME NA NYARAKA ZA MTUME PAULO

(a)Maana ya Kunena kwa lugha
 Biblia inaposema kwamba “watu walinena kwa lugha” ina maana kwamba kusema kwao kulikuwa kwa maneno yasiyokuwa ya lugha yao wenyewe, wala hawakuelewa isipokuwa mtu mwingine alipotafsiri. Licha ya maelezo hayo rahisi kutoa maelezo maalumu kuhusu kunena kwa lugha ni vigumu kwa sababu ya aina tofauti za matumizi ya lugha katika Agano Jipya.

(b) Katika Kitabu cha Matendo ya Mitume
Kuzaliwa kwa Kanisa la Agano Jipya kulitokea mjini Yerusalemu siku ya Pentekoste kama tulivyosikia hapo awali, ambapo wanafunzi 120 walipokea Roho kama Yesu alivyowahaidia (Mdo 2:1-2, 1:4-5). Wakati wa tukio hilo wanafunzi walisema kwa lugha ambazo watu wenye lugha  nyengine waliweza kuelewa kama lugha ya nyumbani kwao (Mdo 2;4-11) .




Licha ya haya kuna sehemu mbili tu katika matendo ya mitume  ambapo mwandishi anaeleza kwamba watu walinena kwa lugha, lakini haifafanui kama kunena kwa lugha kule kulikuwa katika lugha zisizojulikana  au kulikuwa  na jambo jingine kabisa (Mdo 10:44-46, 19:1-6).

Katika kila tukio inaonekana kulikuwa na sababu maalumu inayofanya watu waseme kwa lugha, maana katika kila tukio mambo yakiwa ya kawaida mpaka wakati huo  yaliachwa, kunena kwa lugha kulikuwa ni ishara ya ajabu kwamba watu waliohusika walikuwa wamepokea Roho  Mtakatifu nao waliingizwa katika Kanisa kwa jinsi ile ile ambayo wanafunzi wa kwanza kabisa walifanywa kuwa Kanisa siku ile ya Pendekoste.

(c) Katika Nyaraka za Mtume Paulo
Lugha za kigeni zilizonenwa katika mikutano ya kawaida ya Kanisa zinaoonekana kama zilikuwa na makusudi tofauti. Zilikuwa karama au kipawa ambacho Roho Mtakatifu aliwapa watu fulani ili wakitumie walipomsifu Mungu ( IKor 12:10, 30, 14:2). Watu waliagizwa watumie kipawa kile kwa sharti moja tu, yaani kama tu mwingine aliweza kutafsiri  maneno yake  katika lugha ya kawaida ya waabudu, ili wote waliokuwepo waweze kupata manufaa. Jambo hili linadokeza kwamba iwapo kunena kwa lugha kama tunavyosoma katika matendo ya mitume kulikuwa tukio lisilozuilika, kunena kwa lugha kwa Wakorinto kulikuwa chini ya utawala wa msemaji (IKor 14:13, 27-28). Pia watu walionena kwa lugha katika Kanisa waliweza kufanya hivi kama mtu mmoja tu alisema kwa wakati mmoja na kwa ujumla wasiweze zaidi ya wawili au watatu (IKor 14: 27)

Inaonekana kuwa lugha zilizonenwa hivyo katika Kanisa zilifuatana na lugha  zilizojulikana. Wakristo Wakorintho ambao bado walishawishiwa na tabia za wakati wa zamani walipokuwa wakiabudu sanamu labda walivutwa sana na lugha hizo nao walifikiri kwamba watu  waliozitumia walikuwa wakristo wa hali ya juu na wa kiroho zaidi kuliko wengine. Lakini hali yenyewe ilipita kiasi cha kutotawalika na watu walisema maneno yasiyokuwa ya kawaida au walimkufuru Bwana. Kufuatana na maneno ya Mtume Paulo, jambo hilo lilikuwa uthibitisho kwamba watu wale walionena kwa lugha, si lazima walisema kwa uongozi wa Roho Mtakatifu (I Kor 12:1-3, I Yak 4:1-3).

Ingawa Mtume Paulo aliruhusu kipawa cha kunena kwa lugha alikuwa na uangalifu sana katika kuwatia watu moyo kutafuta kipawa kile. Zaidi akiwahimiza watafute vipawa vile vilivyotangaza neno la Mungu na hivyo viliwajenga wasikilizaji wake (I Kor 12:28-31, 14:3-5). Maneno yoyote yaliyonenwa katika Kanisa yalipaswa kuwa na maana kwa wasemaji, kwa sababu ilikuwa vigumu kwamba yeye ajengwe  kiroho kama hakuelewa maneno aliyosema
(IKor 14 :13-15).

Tamaa ya Wakorinto ya kupata mambo ya ajabu ilionyesha hali yao ya kutokukomaa kiroho, na kutumia vibaya kwa kipawa cha kunena kwa lugha kulileta aibu kwa Kanisa (IKor 14:20-25) kama ilivyo kwa vipawa vyote vya Roho Mtakatifu, Kipawa cha kunena kwa lugha kilitolewa kwa baadhi ya watu tu katika Kanisa, nacho kiliweza kutumiwa vibaya au kuigwa kinyume cha ukweli (IKor 12:3, 7, 10, 30 ,13:1).

Kwa hiyo Paulo alitilia mkazo kwamba uthibitisho wa kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha ya mtu haukuwa kunena kwa lugha bali kama maisha yake mtu huyo yalionyesha matunda ya Roho ambayo ni Tabia ya Kikristo (Gal 5:22-23)

HITIMISHO
Maandiko yasema tuvitafute vipaji vilivyo vya maana (IKor 12:31) kati ya vyote UPENDO kikiwa kipaji bora zaidi kwa vile kinajenga Kanisa, kinawatia moyo na kuwafariji watu na kinadumu hataMbinguni (IKor 13:1-13) ni kwa sababu ya upekee wake huo, Mungu akakiweka kama amri kuu na kuwa kitambulisho cha Wakristo popote watakapokuwa (Mt 22:34-40, Mk 12:28-34, Lk 10:25-28, Yn 13:35).

Tusiangaike mno na karama ya unenaji wa lugha kana kwamba ni muujiza wa kuweza kuingilia mbinguni. Kanisa hutuambia kuwa wetu wengine wa Mungu kama Yohana Mbatizaji hakunena kwa lugha na watu wengine wamefika mbinguni bila kipawa hicho.

Aidha kipawa cha lugha za kigeni kilikuwa muhimu sana wakati huo wa mwanzo wa Kanisa kwa vile lugha za kuwaunganisha watu zilikuwa haba. Leo Biblia imetafsiriwa katika lugha zaidi ya 1200 tofauti. Je Roho mtakatifu atoe ufunuo kwa lugha ipi zaidi?, je kati ya lugha hizo 1200 kuna mtu anaweza kusema haielewi yoyote amlazimishe Roho Mtakatifu amsemeshe kwa lugha nyingine?

Mtume Paulo husema kipawa hicho cha unenaji wa lugha kinawafaa wasioamini na siyo walioamini tayari (Taz IKor 14:22). Hapa ndipo mtume Paulo anaposisitiza kwamba unenaji wa lugha usioeleweka unawafaa wasioamini, na kuchora picha kwa kuwafikirisha Wakorintho kwamba wanaponena watu wengi lugha za kigeni huja picha ya wendawazimu na sio picha ya watu wenye akili timamu. Paulo anasema afadhali aseme maneno matano yenye kueleweka kuliko kusema maneno 10,000 yasiyoeleweka na yeyote (IKor 14:19).

Kanisa Katoliki hutufundisha kupitia maneno hayo ya mtume Paulo kuwa kama watu wanapong’ang’ania kipaji cha unenaji wa lugha tu wanawarudisha wanadamu nyuma kabisa kifikra. Watu kama hao watafundwa na kutumiwa na shetani na wanavutwa wasogee mbele hadi kuwatapeli wenzao wavitumainie na kuvingojea kutoka kwao vipaji vya unenaji wa lugha kwa mfululizo wa kawaida  kila siku wanapokutana kusali. Watu hao ili waweze kuwakidhia wengine  matamanio hayo “hufanya mazoezi” kujikamua machozi na kulia hadi wafuzu. Wakifuzu watawaghilibu wengine kwa kufanya hivyo kwenye mikutano ya hadhara. Hapo ndipo inapotokea dhambi nzito ya kuwatapeli watoto wa Mungu ambao haki yao uishi katika ukweli.

Iwapo wengine wanaodhani kunena kwa lugha ni alama pekee ya kujazwa na Roho Mtakatifu, wengine wanasema alama yake ni ni kuanguka chini. Dhana hiyo ni batili kabisa kwani haina msingi wowote kibiblia. Ikumbukwe kuwa kujazwa na Roho Mtakatifu sio lazima kuashiriwe na kunena kwa lugha isiyoeleweaka au kuanguka chini. Biblia inatuonyesha Yesu alijazwa na Roho Mtakatifu na  kutenda kazi kwa Roho Mtakatifu  (Lk. 4:1 -15) lakini hakunena kwa lugha za kigeni, bali alituachia urithi wa maneno yanayoeleweka.
Kat. George Milinga
Parokia Peramiho


Post a Comment