“Utalii kwa wote - wote wawezeshwe” hii
ni kauli mbiu ambayo kila nchi mwanachama wa shirika la Utalii Dunia (UNWTO)
inaendelea kutumia hadi hapo itakapotolewa nyingine itakayoanza kutumika Septemba mwaka huu na Tanzania ni moja ya nchi
yenye vivutio vingi vya utalii duniani na ipo katika orodha ya nchi zilizopo
katika umoja huo.
Tanzania tumebarikiwa kuwa na vivutio
vya asili (god given) pamoja na vile vya kuanzishwa (Man made) ambavyo
vinaingiza fedha nyingi za kigeni toka kwa watalii wanaotembelea hapa nchini
toka kila pembe ya dunia. Hatuna budi kumwomba Mungu mara nyingi kadiri tuwezavyo
kwa kutupatia raslimali hadhimu ambazo ni hazina kubwa katika sekta ya Utalii
na zenye tija kwa vizazi vijavyo.
“Lugari Zoo” iliyopo katika Kijiji cha
Tugutu wilayani Mbinga, Mkoani Ruvuma ni
moja ya kivutio cha Utalii cha Kutengenezwa kilichoanzishwa na Mwanajeshi
Mstaafu Samweli Ndomba, baada ya yeye kutambua umuhimu wa utalii kwa watanzania
na mapenzi yake toka moyoni katika Sekta ya Utalii duniani.
Lugari zoo yenye takribani hekta 127, ilianzishwa
mwaka 2013 na hadi kufikia hivi sasa ina
umri wa miaka minne. Watalii wengi toka maeneo tofauti ambao wanatembelea
Lugari Zoo wanapata fursa hadhimu ya kuona Ndege wa aina mbalimbali kama Tausi,
Peakoc,vecharine, Kuku, Bata, njiwa aina tofauti na wengine wengi wakiwemo
ndege ambao asili yao ni Mbinga.
Lakini wapo pia Wanyama wanaokula
majani pamoja na wale walao nyama, kati yao pia wapo wanyama wakali na wanyama
wapole. Wanyama wakali wamewekwa kwenye vibanda vya chuma kwaajili ya usalama
huku wale ambao sio wakali wapo kwenye wigo wa kawaida. yapo makundi ya wanyama
tofauti tofauti toka nchi mbali mbali kama vile Chui, Simba, Swala, Ngamia,
Pundamilia, Fisi n.k.
Aidha
Mandhari mazuri yaliyopambwa na bustani za maua, picha zuri bila kusahau
mabwawa yenye Samaki n.k, vinatoa chagizo kwa watalii wanaotembelea Lugari Zoo
kwenda mara nyingi kadiri wawezavyo na wakati mwingine baadhi ya watalii
wakienda Lugari Zoo hawatamani kurudi makwao. Neno “Zoo” maana yake ni bustani
ya wanyama.
Katika ziara ya kiutalii iliyofanyika
hivi karibuni huko Lugari Zoo na baadhi ya wafanyakazi wa Abasia ya Peramiho
(Prokura) kwa lengo la kupumzisha hakiri mwanzoni mwa mwaka 2017, Msimamizi
mkuu wa Kampuni hiyo Samwel Samwel Ndomba ambaye amerithi jina la Baba yake
Mzee Samwel alifafanua yafuatayo kuhusu Lugari zoo:
“Asili ya jina Lugari zoo limetokana na
jina la kijiji alichotokea Mmiriki Mzee
Ndomba ambaye ni Baba yangu mzazi, lengo la kutumia jina hilo ni kuenzi kijiji
alichotokea pamoja na kukuza jina la kijiji chake ”
“Kabla ya yeye kustaafu kazi ya jeshi
nakumbuka aliniambia kuwa kutokana na mapenzi yake katika Sekta ya Utalii
Duniani lazima angeanzisha kitu chochote kinachohusiana na mambo ya utalii
ambapo baada ya kustaafu ameamua kutekeleza kwa vitendo kwa kuanzisha Lugari
Zoo ikiwa ni fahari kwake pia kwa wanaruvuma”
“Lugari Zoo tuna makundi ya aina
tofauti tofauti ya wanyama pamoja na ndege toka maeneo tofauti duniani, kwa
waliobahatika kutembelea hapa bila shaka ni mashahidi wa hilo, toka
tulipoanzisha hadi kufiki hivi sasa watu kutoka sehemu tofauti wamepata fursa
ya kutembea hapa Lugari Zoo, wakiwemo wale wa nje ya Tanzania” anasimulia
Samweli Ndomba kisha anaendelea.
Malengo ya Lugari Zoo
“ Tofauti na kujiingizia kipato, Lugari
Zoo tunaiboresha kila mwaka ili kuifanya iwe ya kimataifa kwa lengo la kutoa
huduma bora kwa watu wote, binadamu wanaitaji muda wa kupumzika na kuburudika
baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu, maeneo ya kitalii kama Lugari Zoo ni sehemu moja wapo ya kupumzika”
Wakazi wa mbinga
“ Ni mara chache kwa nabii kukubarika
nyumbani kwa kuwa watu wengi wanaokuja hapa ni wageni kuliko wenyeji,
inawezekana bado hawana elimu ya kutosha kuhusu maana ya utalii na hawajui faida
ya kupumzisha hakiri. Uwezi kuamini kuna watu wanakaa wilayani Mbinga lakini
hawajui kinachoendelea hapa ndani, nawakaribisha wakazi wote wa Mbinga pamoja
na maeneo yote ya Tanzania hapa Lugari Zoo, waje wajione wenyewe mazuri ya
hapa”
Chakula cha wanyama
“Wanyama wanaitaji chakula bora na
kingi ili waweze kuishi, wastani kwa siku tunatumia laki mbili na kidogo
kwaajili ya chakula cha ndege na wanyama, pia ili kupunguza gharama
tunalazimika kuchanganya nyama na dona kwa wanyama kama jamii ya fisi na
kuwafanya waendane na mazingara yetu tofauti na mazingira ya polini ya kula nyama
tu (kwa kuzingatia maelekezo ya daktari wetu wa mifugo), Wanyama kama Chui
anakula kilo nane (8) za nyama kwa siku ambapo kwa wiki anakula mara nne (4)
8*4*7000=Tshs.224000/= hiyo ni gharama ya chakula cha Chui kwa wiki”
Changamoto
“Daktari akimwacha mgonjwa katika hali
zuri, baada ya muda mfupi akamkumta amefariki lazima imuume, hata kwa upande
wetu tunapambana na tatizo la vifo vya wanyama hasa vile vya ghafla tunaumia
sana tukikuta Sungura au Mamba amepoteza maisha. Tuna madaktari wa mifugo ambao
wanawafanyia uchunguzi mara kwa mara kwaajili ya usalama wao”
“Siku zingine watalii wanaweza
wakapungua na siku zingine wanakuwa wengi na ili kujihakikishia kupata watalii
wengi kila siku tunaendelea kuboresha hudama zetu mara kwa mara ili kuendana na
wakati tulionao”
Usalama
“Ulinzi ni mkubwa mno kwa usalama wa
wanyama na kwa Raia wanaokuja na wanaoishi karibu na Lugari Zoo, tuna walinzi
watano wenye silaha na mabanda ya wanyama ni imara hasa yale ya wanyama wakali
kama Simba, chui n.k. vile vile tunaendelea kuimarisha kutokana na mahitaji na
wakati” anafafanua Samwel Ndomba Mtoto wa Mzee Ndomba Mmiriki wa Lugari Zoo.
Kuwaongoza watalii ni moja ya kazi
ngumu inayoitaji umakini mkubwa kwa kuwa watalii wengi ni watu wa aina tofauti,
wapo waliosoma, wasiosoma, walevi, watoto, viziwi, wazee na hata wadadisi hasa
wale wanaojifanya wanajua vitu ambavyo hawavijui, hizo ni moja ya changamoto
ambazo wanakabiliana nayo wafanyakazi wa Lugari Zoo.
“Kuwaudumia wanyama na kuwaelekeza
watalii inaitajika taaluma ya hali ya juu kwa kuwa wanakuja watu wa aina
tofauti na wenye uelewa tofauti wa vitu. Lakini tunapata sana shida kwa wale
ambao wanakuja ili kutupima au kutuchezea hakiri lakini kwa kuwa tuna mafunzo
bora na uzoefu wa kutosha, kila mmoja anapata kile anachokiitaji kwa usahihi”
anafafanua kiongozi wa watalii wa Lugari Zoo Richard Kawanga.
Dunia kote idadi ya watu wanaosafiri nje ya nchi yao kwa
ajili ya utalii iliongezeka kwa asilimia 4.4 mwaka 2015 na hivyo kuvunja rikodi
mpya kwa mwaka wa sita mfululizo.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii UNWTO lilisema kwenye
taarifa yake kuwa idadi ya watalii ilifikia bilioni 1.2 mwaka 2015 na ongezeko
hilo limechangia pakubwa katika ukuaji wa uchumi na uzalishaji wa ajira kwenye
maeneo mengi ya dunia, kuna matarajio makubwa ya ongezeko la watalii hasa barani
Asia na Pasifiki huku watalii wengi wanatarajiwa kutokea katika nchi za China,
Marekani na Uingereza.
Matarajio kwa Afrika na Mashariki ya Kati hayako thabiti kwa
sababu ya vitisho vya usalama na ukosefu wa takwimu sahihi kuhusu usimamizi wa
vivutio vya utalii vilivyopo pamoja na idadi ya vivutio vyote kwa kila nchi
usika.
Bustani ya wanyama ya Lugari ipo kwenye orodha ya vivutio
vya kitalii ambavyo vinakuza kipato cha serikali ya Tanzania ambapo kutokana na
amani, utulivu pia usalama uliopo Tanzania Serikali inatakiwa kuwa makini zaidi
katika sekta ya utalii kupitia sera ya uwekezaji ili kuvuna fedha nyingi zaidi
kupitia utalii. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Lugari Zoo, Amina
Post a Comment